• HABARI MPYA

  Monday, October 21, 2013

  MSUVA AITWA OFISINI NA WAZIRI WA KIKWETE

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  WAZIRI wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara amemuita mchezaji chipukizi, James Msuva ofisini kwake kwa lengo la kumsaidia zaidi kumuendeleza kisoka, baada ya kuonyesha kipaji kikubwa katika michuano ya Kombe la Umoja na Amani, iliyomalizika mwishoni mwa wiki, Dar es Salaam.
  Dk Fenella alimuambia mdogo huyo wa winga wa Yanga, Simon Msuva awasiliane na Msaidizi wake ili kupata mwongozo wa kufika wizarani baada ya fainali ya michuano hiyo, ambayo kijana huyo mwenye umri wa miaka 16, alifunga mabao yote mawil,i Baruti FC ikishinda 2-0 na kutwaa Kombe. 
  Nataka kucheza Ulaya; James Msuva akihojiwa na Televisheni ya Taifa, TBC1 Jumamosi Uwanja wa Ubungo Msewe

  Michuano huyo iliyoandaliwa na Waziri huyo wa serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ilifikia tamati Jumamosi kwenye Uwanja wa shule ya Msingi Ubungo Msewe, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa Baruti FC kuibuka mabingwa, baada ya kuwafunga Kimara United mabao 2-0 katika fainali, Msuva akifunga mabao yote hayo kipindi cha pili.
  Ulikuwa mchezo mkali uliovuta mashabiki wengi uwanjani, wa rika tofauti na jinsia zote pia, ambao kwa hakika walifurahishwa na kile kilichofanywa na Dk Fenella- kuandaa mashindano hayo.
  Vijana wadogo walicheza soka ya kuvutia kana kwamba wanafundishwa na walimu waliobobea, kumbe ni makocha wa mtaani tu wasio na mafunzo ya kitaaluma.
  Hongera kijana; Dk Fenella akimpigia makofi ya pongezi James Msuva, baada ya kumpa zawadi ya ufungaji bora, Sh. 200,000


  James Msuva kulia

  Shujaa; James Msuva akiwa amebebwa na mashabiki

  Fundi kama kaka; James Msuva akimiliki mpira

  Pamoja na kufungwa, Kimara United ilionyesha upinzani na ndiyo iliyocheza vema zaidi kipindi cha kwanza, kabla ya kuja ‘kutepeta’ dakika 20 za mwisho na kuwaachia Kombe wapinzani wao.
  Pamoja na kuwa shujaa wa fainali, Msuva mdogo pia aliibuka mfungaji bora wa mashindano hayo kwa kufikisha jumla ya mabao saba na kuzawadiwa jumla ya Sh. 200,000, wakati mabingwa Baruti FC walipewa Kombe, Sh. Milioni 2 na seti ya jezi.
  Washindi wa pili, Kimara United walipewa Sh. Milioni 1, seti ya jezi na mipira miwili na washindi wa tatu katika mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 32 za Manispaa ya Kinondoni, walipewa Sh. 500,000 na mipira miwili.
  Simon Msuva kulia akiichezea Yanga, huyu ndiye kaka wa James
     

  James anayemfuatia Simon Msuva kuzaliwa, amehitimu Kidato cha Nne katika sekondari ya Makongo, Dar es Salaam na pamoja na kuchezea Barudi FC kama timu ya mtaani, pia kwa sasa yupo katika akademi ya Wakati ya Ujao, iliyoasisiwa na kocha wa zamani wa Simba, Mholanzi Ronny Mintjens. 
  James alisema matarajio yake ya baadaye ni kucheza soka ya kulipwa Ulaya ila ikitokea timu ya hapa Tanzania ikavutiwa na kipaji chake atajiunga nayo kujiendeleza. “Kucheza Simba, Yanga au Azam naweza kama kupita njia tu, lakini malengo yangu mimi ni kucheza Ulaya,”alisema. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSUVA AITWA OFISINI NA WAZIRI WA KIKWETE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top