• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 28, 2013

  HONGERA MALINZI NA SAFU YAKE YOTE MPYA, LAKINI CHONDE CHONDE ATUACHIE WAMBURA WETU OFISINI

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) usiku wa kuamkia leo limepata uongozi mpya, kufuatia uchaguzi Mkuu uliofanyika kuanzia asubuhi ya jana katika ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam.
  Jamal Emil Malinzi amerithi kiti cha beki wa kati wa zamani wa Pan Africans, Yanga na Nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Leodegar Tenga ambaye hakugombea tena baada ya kuongoza bodi hiyo kwa awamu mbili.
  Malinzi, Katibu wa zamani wa Yanga SC, amemshinda aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa TFF katika awamu ya pili ya Tenga, Athumani Nyamlani kwa kura 20, yaani 72 kwa 52  wakati Wallace Karia ameshinda nafasi ya Makamu wa Rais kwa kupata kura 67 dhidi ya 52 za Nassib Ramadhani na Imani Madega sita.   
  Kamati mpya ya Utendaji TFF

  Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera) aliyepata kura 102 za ndiyo na 17 za hapana. Kanda namba 2- Mara na Mwanza, mshindi ni Vedastus Lufano aliyepata kura 51 dhidi ya Jumbe Odessa Magati (11), Mugisha Galibona (24), na Samwel Nyalla (39).
  Epaphra Swai ndiye mshindi wa Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu kwa kura 63 dhidi ya Mbasha Matutu aliyepata 61. Kanda namba 4- Arusha na Manyara mshindi ni  Omali Walii Ali aliyepata kura 53 dhidi Elley Mbise (51), Ally Mtumwa (19).
  Kanda namba 4- Kigoma na Tabora, mshindi ni Ahmed Idd Mgoyi aliyepata kura 92 dhidi ya 28 za Hamisi Yusuf Kitumbo.
  Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo ameshinda Kanda namba 6- Katavi na Rukwa kwa kura 73 dhidi ya Ayubu Nyaulingo aliyepata 52. Ayoub Shaibu Nyenzi ndiye mshindi wa Kanda namba 7- Iringa na Mbeya kwa kupata kura 59 na kuwapiku David Samson Lugenge (8), John Exavery Kiteve (12) na Lusekelo Elias Mwanjala (46).
  Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma inawakilishwa na James Patrick Mhagama aliyepata kura 93 dhidi ya 31 za Kapteni mstaafu Stanley William Lugenge. Athuman Kingombe Kambi ndiye mshindi wa Kanda namba 9- Lindi na Mtwara kwa kura 84 akiwazidi Francis Kumba Ndulane (30) na Zafarani Mzee Damoder (11).
  Hussein Zuberi Mwamba ametetea ujumbe wa Kanda namba 10- Dodoma na Singida kwa kura 63 akiwapiku Stewart Masima (58) na Charles Komba (4). Geofrey Irick Nyange ameshinda Kanda namba 11- Morogoro na Pwani akipata kura 78 dhidi ya Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na Twahil Twaha Njoki (2).
  Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani, Khalid Abdallah Mohamed ndiye aliyeibuka kidedea kwa kura 69 dhidi ya 54 za mpinzani wake Davis Elisa Mosha.  Kidao Wilfred Mzigama ameshinda Kanda namba 13- Dar es Salaam kwa kupata kura 60 dhidi ya wapinzani wake Muhsin Said Balhabou (50), Omar Isack Abdulkadir (10) na Alex Crispine Kamuzelya (4).
  Boniface Wambura ni mchapakazi, anatekeleza majukumu yake zaidi ya vizuri, anastahili kuendelea na nafasi hiyo


  Sasa uongozi mpya unatarajiwa kuingia ofisini Jumamosi na Malinzi amesema anataka kufungua ukurasa mpya katika soka ya Tanzania akianzia kwa kuwasamehe wale wote waliokuwa wamefungiwa kwa tuhuma mbalimbali chini ya Tenga, isipokuwa tu waliokutwa na hatia za kuhusika na rushwa na upangaji wa matokeo.
  Tunaamini, kama alivyosema Malinzi jana kwamba hata rais wa nchi akichaguliwa huwa anatoa misamaha- na pia hufanya mabadiliko ya safu za uongozi kwa kiasi kikubwa.
  Tunatarajia mabadiliko ya waajiriwa wa safu mbalimbali za kitaalamu pale TFF, lakini tunaomba yawe mabadiliko yenye tija na si kumuondoa mtu ambaye amekuwa akifanya kazi yake vizuri na kuingiza mtu ambaye hatakwenda kufanya kwa ubora wa yule aliopo.
  Kwa mfano sisi Waandishi wa Habari, mtu ambaye tunafanya naye kazi ni Boniface Wambura, hakika huyu bwana amekuwa akitekeleza majukumu yake zaidi ya inavyompasa kiasi kwamba wengi wetu tumejenga imani kubwa na yeye.
  Wambura ni mwadilifu, mwajibikaji, ana nidhamu ya kazi. Si mtu wa makundi na anafanya kazi yake pia kwa ushirikiano na usawa kwa watu wote. Tunaona kabisa, kama mabadiliko yatatokea yeye hayastahili kumkuta. Hatuwezi kuuingilia uongozi mpya katika maamuzi, lakini tunaweza kutoa ushauri tu, kwa mabadiliko yoyote, Boniface Wambura aachwe aendelee kufanya kazi za TFF, ni mtu sahihi. Pongezi kwa Malinzi na safu yake yote, kila la heri katika utawala wao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HONGERA MALINZI NA SAFU YAKE YOTE MPYA, LAKINI CHONDE CHONDE ATUACHIE WAMBURA WETU OFISINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top