• HABARI MPYA

    Wednesday, October 23, 2013

    MALINZI AZINDUA KAMPENI ZA KURITHI KITI CHA TENGA TFF LEO, AAHIDI MAMBO MAKUBWA SOKA YA TANZANIA

    Mgombea Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi akizungumza Waandishi wa Habari katika uzinduzi wa kampeni zake kuelekea uchaguzi Mkuu wa shirikisho hilo.
    "Ndugu zangu,
    Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetulinda na kutuwezesha kufika
    hapa tulipo.
    Tarehe 19 Novemba 2009 Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati anazindua ziara ya Kombe la FIFA la
    dunia uwanja wa Taifa, Dar Es Salaam pamoja na mambo mengine alisema, namnukuu:
    ‘‘Kwa Watanzania wenzangu tuichukulie ziara ya Kombe la Dunia nchini mwetu
    kama ni changamoto kubwa kwetu inayotutaka tufanye vizuri zaidi katika soka ili
    tulingane na heshima hii tuliyopewa. Hasa ni changamoto kwa viongozi wa soka wa
    ngazi zote pamoja na wachezaji na wapenzi wa mpira wa miguu nchini. Kuja kwa
    kombe hili ni deni kwetu na kulilipa kwetu sisi ni kuzinduka, tuendeleze kiwango
    chetu cha soka nchini ili na sisi siku moja TUSHIRIKI FAINALI ZA KOMBE
    HILI (msisitizo ni wa kwangu). Hili jambo linawezekana. Wapo wenzetu Afrika
    wameweza, kwa nini sisi tusiweze? Wao ni watu kama sisi, maadam wameweza na
    sisi tutaweza.
    Lakini ili tuweze hatuna budi kuiga mfano hususani waliyofanya wenzetu na
    wanayoendelea kufanya kuendeleza mpira wa miguu. Twende tukajifunze kutoka
    kwao. Lakini hata kabla ya kwenda huko, yapo mambo hatuna budi kuyafanya.
    Naomba nitaje baadhi yake:


    1. Tuimarishe Uongozi, utendaji na uendeshaji wa vilabu vya mpira. Mchezaji
    hufundishwa kucheza mpira katika Klabu yake. Hapo ndipo hufundishwa
    maarifa ya kucheza mpira na vipaji kuendelezwa. Hebu tujiulize hali ya
    vilabu vyetu vya soka ikoje. Je vinaongozwa vizuri? Vinaendeshwa vizuri?
    Jibu tunalijua sote kuwa ni hapana. Lazima suala hili tulitafakari kwa makini
    na kulipatia jawabu. Tukishindwa kupata jawabu muafaka na mambo
    yakaachwa kuendelea yalivyo, mpaka mwisho wa dunia hatutakuwa tunasogea
    popote.
    2. Tupate walimu wenye uzoefu kufundisha timu zetu. Hii ndiyo njia ya uhakika
    ya kukuza na kuendeleza vipaji na hivyo kupata wachezaji bora.
    3. Tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka umri mdogo.
    Vilabu viwe na timu za watoto na vijana. TFF isaidie kuanzishwa kwa shule
    za mchezo wa mpira wa miguu kwa watoto na vijana. Mashuleni wapatikane
    walimu wa michezo walio wazuri kufundisha.
    4. TFF ionekane zaidi ya ilivyo sasa katika mipango ya kuendeleza soka
    mashuleni, vijijini, mitaani na vilabuni. TFF ikiwa na mipango na kuisimamia
    na kuwabana wadau kuitekeleza itasaidia. Vinginevyo TFF itabakia
    kusimamia Ligi Kuu, kutoa adhabu kwa wachezaji na kusimamia timu ya
    Taifa. Hiyo haitoshi.’’
    Mwisho wa kunukuu.
    Ndugu zangu wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, wadau na wapenzi wa mpira wa Miguu Tanzania
    tujiulize kuanzia kipindi hicho cha 2009 hadi leo hii katika haya maagizo ya Mheshimiwa Rais Jakaya
    Mrisho Kikwete tumetekeleza yapi zaidi ya kuwa wasindikizaji katika medani ya kimataifa? Kipindi
    chote cha miaka minane iliyopita Serikali imetoa sapoti kubwa katika sekta ya mpira wa miguu kwa
    kulipia walimu wa timu za Taifa na kuhimiza makampuni kama NMB,Serengeti Breweries,Airtel,Coca
    Cola na sasa Tanzania Breweries kudhamini timu zetu za taifa na mashindano mbali mbali,matunda
    yake yako wapi? Ndo kwanza tunazidi kuporomoka kwenye viwango vya FIFA. Iweje miaka ya
    nyuma timu zetu za Taifa zilifanya vizuri wakati zinaweka kambi Salvation Army, leo zinakaa hotel za
    nyota tatu mafanikio mbona hatuyaoni? Kama TFF imeondolewa gharama za kulipa makocha, kuweka
    timu kambini, kununua vifaa vya timu, dawa, posho ,malazi pamoja na usafiri wa timu iweje leo TFF
    ishindwe kutumia vyanzo vyake vya mapato zikiwemo fedha toka FIFA na CAF kwa ajili ya
    kuanzisha na kuendeleza programmu ya vijana ya kitaifa? Kwa mujibu wa mtandao wa FIFA kati ya
    mwaka 2008 na 2012 TFF imepokea toka FIFA msaada wa jumla ya dola za kimarekani milioni moja
    na lake nane na nusu (yapata shilingi bilioni tatu za kitanzania), hizi fedha zimefanyia nini? Kwa nini
    timu za vijana hazina udhamini? Ipi timu yetu ya taifa iwe ya wanaume wakubwa (senior team) ,
    wanawake au za vijana inayoweza leo hii kujivunia mafanikio? Iko wapi ligi ya wanawake? Katika
    hili tusilaumu Chama cha mpira cha wanawake, wakiwezeshwa wanaweza.Tutapataje timu mahiri ya
    Twiga stars bila ligi ya wanawake? Katika ngazi ya klabu, hasa zinazoendeshwa kwa mfumo wa
    kijamii kama Toto Africa, Coastal Union, Yanga, Simba,Mbeya City n.k. hadi leo hii pamoja na
    rasilimali za vilabu hivi ni klabu ipi imeweza kusimamia na kujiendesha yenyewe tokana na vyanzo
    vyake yenyewe? Tuendelee kujiuliza:
    Ø Ni walimu wangapi wa mpira tumewaendeleza kufikia kiwango cha kukabidhiwa majukumu ya
    kufundisha Taifa Stars. Fursa za mafunzo tunazopewa na FIFA na CAF tunazitumiaje? Je
    tumeweza kuwa na angalau kocha mmoja anayefundisha mpira nje ya nchi kama ilivyo kwa
    akina Sam Timbe ( wa Uganda), James Sianga ( wa Kenya) Jack Chamangwana ( wa Malawi)
    na wengine ambao waliweza kufundisha mpira Tanzania kwa ufanisi?
    Ø Ni refa gani tumemuendeleza akafikia kiwango cha kuchezesha mashindano ya fainali za dunia
    au AFCON au Klabu bingwa ya Africa? Refa wa mwisho kuchezesha fainali za Mataifa Africa
    (AFCON) ni Omar Abdulkadir huko Burkina Faso mwaka 1998.
    Ø Ni program ipi ya vijana ya kuibua vipaji na kuviendeleza tuliyo nayo? Wale vijana wa Copa
    Cocacola 2007 waliopelekwa kwa mbwembwe Brazil waliishia wapi? Tuna rekodi
    zao?Tunajua wako wapi na wanafanya nini? Na hawa walioshinda majuzi Afrika Airtel Rising
    Stars tumewatangenezea program gani ya maendeleo?
    Ø Tunaelewa matatizo ya vilabu vya mpira hususani uhaba wa vifaa na pesa za uendeshaji, je
    vilabu vyetu TFF inavisaidiaje katika kuendeleza programu zao za vijana?Au kazi yetu ni kudai
    kila klabu iwe na timu ya under 20 bila kujali gharama za uendeshaji wa timu hizi?
    Ø TFF hadi sasa imebuni, kusimamia na kutekeleza program endelevu ipi ya kuendeleza soka
    mashuleni, vijijini, mitaani au vilabuni? Au mpaka tusubiri Airtel rising Star na Copa
    Cocacola? Siku wakubwa hawa wakisusa itakuwaje?
    Ø Ziko wapi juhudi za kuhimiza upatikani wa vifaa vya kufundishia mpira watoto (kama mipira
    size 3/4) pamoja na kuimarisha miradi ya kuendeleza vijana ?
    Ø Hivi timu zetu za Taifa zinatumia mfumo upi wa uchezaji? Au kila kocha wa taifa tunayemleta
    anakuja na mfumo wake? Wenzetu wameweza kubuni mifumo ya uchezaji ya timu zao za
    Taifa na wameushirikisha katika mfumo wa ufundishaji wa watoto. Lini Mwalimu wetu wa
    Taifa alikaa na walimu wa vilabu (angalau vya Premier League) ili kujadili ufundishwaji wa
    mpira nchini, hii ikiwa ni pamoja na kujadili masuala yahusuyo mbinu, lishe, huduma za afya
    na ukakamavu wa mwili? Hivi mchezaji akitoka katika klabu yake ambako amezoea kula dona
    na maharage ukampeleka kambi ya Timu ya Taifa akapewa prawns, kuku na samaki kwa siku
    nne za kambi itamsaidia kumbadili siha? Ng’ombe hanenepeshwi siku ya mnada.Uratibu wa
    programu za vilabu ni muhimu.
    Ø Raha ya mpira ni kelele na hoi hoi za mashabiki. Wataalam wa mpira wanasema umoja wa
    mashabiki wa mpira ni sawa na mchezaji wa 12 uwanjani. Zipo timu ambazo kihistoria
    zilikuwa ni za kijamii na zilihamasisha sana ligi ya Taifa, na kuiongeza hamasa na
    ushindani,Mbeya City ni mashahidi. Leo hii ziko wapi timu kama Ushirika ya Moshi, Bandari
    ya Mtwara, Kariakoo Lindi, Balimi Bukoba, Reli Kiboko ya vigogo, Kahama United, Mirambo
    ya Tabora, Tukuyu Stars, Nyota Korogwe, African Sports ya Tanga,Ujenzi Rukwa,Mji
    Mpwapwa n.k. TFF imefanya juhudi gani kufufua ushidani huu kwa kushirikiana na vyama
    vya Mikoa na Wilaya?
    Ø Wapo wachezaji wastaafu waliojitolea kwa moyo mmoja kuiletea heshima nchi yetu. Leo hii
    tunasikia kina Alfonce Modest na Jellah Mtagwa wanalalamika hawana msaada, na hao ndio
    wale waliojitolea hadharani kutoa kilio chao. TFF hadi leo hii imewahi kuandaa mpango gani
    endelevu wa kuwasaidia wachezaji wastaafu? Shirikisho la mpira barani Afrika CAF
    wameanzisha ISSA HAYATOU TRUST FUND kusaidia wachezaji wastaafu waishio katika
    mazingira magumu,sisi tumechukua hatua gani katika hili?
    Ø Iweje mpake leo hakuna mashindano yoyote ya wanawake ya kitaifa yawe ya ligi au ya
    mtoano,angalau kwa ngazi ya kanda ? TFF itawezaje kuibua vipaji vipya vya timu ya taifa ya
    wanawake TWIGA Stars bila mashindano ya aina hii?
    Ø Vilabu vya mpira, hususani vya Ligi Kuu, vimegeuka kuwa kisima cha watu kuchota fedha.
    Haiyumkiniki vilabu ambavyo vinaweka timu kambini, kuihudumai kuanzia malazi, posho,
    vifaa, madawa na usafiri mwisho wa mechi jumla ya pesa wanayopewa inakuwa chini ya nusu
    ya mapato yote ya mechi. Hayo maendeleo ya mpira ambayo yametakiwa yaanzie ngazi ya
    vilabu yatapatikanaje? Vilabu vimegeuka vitega uchumi vya watu wengine wakati vyenyewe
    vinataabika na kujiendesha kwa mateso makubwa.
    Ya kusema ni mengi, kwa leo tuishie hapa.

    Nini matokeo ya hali hii? Takwimu hazidanganyi. Matokeo ya hali hii ni timu za Taifa kushuka
    viwango katika orodha ya FIFA siku hadi siku. Viwango vya timu za taifa vinapimwa kwa kuangalia
    uwiano wa matokeo ya timu ya wakubwa (senior) pamoja na yale ya timu nyingine za vijana za nchi
    husika. Miaka ya mwanzo ya tisini tulishawahi kupanda hadi nafasi ya 65, leo hii kila kukicha tuko
    kwenye 120.Kuporomoka huku kutaendelea hadi lini?
    Ndugu zangu, tujiulize wapi tumetoka, tuko wapi na tunataka kuelekea wapi? Jibu ni rahisi, kama
    alivyoagiza Mh Rais Kikwete,tujipange upya, tubuni mkakati wa uendelezaji wa mpira, tuandae
    program endelevu yenye malengo yanayopimika na kwa pamoja tukishirikiana na Serikali, FIFA
    CAF na CECAFA,Halmashauri, Taasisi zisizo za kiserikali, Sekta binafsi, Vyombo vya habari na
    wadau wengine wote wa mpira wa miguu tutaweza kufanya vizuri na kuifanya Tanzania isifike
    duniani kote. Katika kutimiza azma hii sharti tuanzie kwa kuleta mabadiliko ya uongozi wa juu wa
    TFF, tupate kiongozi ambaye sio sehemu ya mapungufu ya TFF,hakuna njia ya mkato.Mimi Jamal
    Emil Malinzi,nimejipima na ninaamini nina uwezo wa kutosha wa kubuni, kuratibu na
    kusimamia mabadiliko haya nikiwa Rais wa TFF.
    Ndugu zangu, siku zote si vyema kukosoa bila kueleza njia mbadala ya kufuata ili kutatua tatizo. Hapa
    tunazungumzia mpira wa miguu na namna ya kuunasua toka kwenye janga la kushuka kiwango na
    timu zetu za Taifa kuendelea kugeuzwa kichwa cha mwenda wazimu ambacho hadi majuzi vibonde
    Gambia wamejifunzia kunyoa.
    Ili tuweze kuukwamua mpira wetu ni vyema tukakumbushana kuwa ili mpira uendelee unahitaji vitu
    vinne:
    1. Vipaji;
    2. Walimu;
    3. Vifaa;
    4. Viwanja
    1. Vipaji
    Tanzania ni nchi yenye watu zaidi ya milioni 44. Nchi ya Cape Verde yenye watu 500,000 tu
    imeweza pamoja na uchache wake kuvumbua vijana 11 ambao wameweza kuifikisha nchi yao
    fainali za Africa 2013 Afrika Kusini na majuzi nusura waende kombe la dunia kama sio tatizo
    la utunzaji kumbukumbu. Sayansi ya uibuaji vipaji (scouting) ni muhimu na si kila mtu
    anaijua. Watafutwe wanaoijua, watufanyie kazi ya kutuibulia vipaji vipya, na katika hili ni
    sharti mpira wa ushindani uchezwe nchini kote ili vipaji vionekane.
    2. Walimu
    Mpira ni sayansi,mpira ni taaluma. Kipaji bila mwalimu wa kukiendeleza ni bure. Vijana
    mpira wanaanza kuucheza wakiwa wadogo hususani wakiwa shule za msingi. Huko ndiko
    Taifa linahitaji kusambaza walimu wenye taaluma ya kufundisha mpira ngazi ya awali.
    Wakishakuzwa kimpira ni lazima wawepo walimu wa kutosha kuwaendeleza ngazi ya
    wakubwa na Taifa. Leo hii Uingereza ina walimu 1100 wenye leseni daraja A,Ujerumani wapo
    5500 na Hispania 12,000,Tanzania tunaye mmoja tu,kwa mtaji huu tutafika kweli?Kwa mujibu
    wa ripoti ya TFF nchi nzima ya Tanzania ina walimu wa mpira wa madaraja yote elfu mbili tu
    na mia tano kati yao wako Dar es salaam. Hawa walimu 2000 ndio wanategemewa
    wawafundishe mpira vijana wa Kitanzania zaidi ya milioni kumi walio katika umri wa
    kufundishwa mpira!
    3. Vifaa
    Wachezaji, walimu wa mpira, madaktari na waamuzi wote wanahitaji vifaa vya msingi ili
    mpira uchezwe. Nchini mwetu vijana walio wengi wanacheza pekupeku, jezi ni upande mmoja
    kucheza kifua wazi, mpira ni wa kuviringisha matambara, refa anavaa suruali, filimbi ni mluzi,
    magoli hayana nyavu, n.k. Hii ndiyo hali halisi ya uchezwaji wa mpira maeneo mengi
    Tanzania hasa vijijini ambako ndiko kunapaswa kuwa chimbuko kubwa la vipaji.
    Gharama za vifaa vya michezo ziko juu mno, mfano mpira mzuri unaofaa kuchezewa kwenye
    ardhi ngumu (rough surface) bei yake ni shilingi laki tatu, shule ipi ya msingi itaweza
    kuununua huu mpira? Kuna baadhi ya vyombo vya habari majuzi viliripoti kuwa kuna
    mchezaji alifunga hat trick ngazi ya Ligi Taifa akanyimwa mpira kisa ni wa thamani kubwa.
    Mamlaka husika, hasa za kodi zinapaswa kuliangalia hili, ili upatikane unafuu katika bei za
    vifaa vya michezo maana karibia vyote vinaagizwa toka nje. Lakini pia vifaa vya michezo vya
    misaada vinavyopatikana kutokana na miradi mbalimbali ya TFF ni juu ya TFF kuhakikisha
    vinafikishwa vijijini pia kupitia vyama vya mikoa na wilaya.
    4. Viwanja
    Wilayani Ngara mkoani Kagera kuna uwanja wa mpira unaitwa ‘’Uwanja wa Changarawe’’ na ni
    kweli uwanja huo umejaa changarawe. Beki akikaba kwa mtindo wa kuteleza ardhini ‘sliding tackle’
    basi nyama ya paja anaiacha pale chini. Hii ndiyo hali halisi ya viwanja vyetu vingi nchini, kama vipo
    ni vibovu sana maana maeneo mengi viwanja vya mpira hakuna vimechukuliwa na wajanja wachache
    na kugeuzwa makazi na majengo ya biashara. Tunahitaji viwanja vyenye ubora ili vijana wetu
    wafundishwe mpira wa kisasa kwa ufanisi, mpira wa kupiga pasi ya chini. TFF kwa kushirikiana na
    vyama vya Mikoa na Wilaya sharti wawe mstari wa mbele katika kulipigania hili.
    AHADI YANGU
    Endapo nitachaguliwa kuwa Rais wa TFF, kwa kushirikiana na viongozi wote wa TFF kuanzia ngazi
    ya vilabu, Wilaya, Mikoa na Kamati ya Utendaji Taifa na kwa kuhusisha kwa karibu Vyama vya
    kimataifa vya FIFA na CAF, Serikali, Halmashauri,Taasisi zisizo za kiserikali, Vyombo vya habari,
    Sekta binafsi, Mashirika ya umma na wadau wa mpira wa miguu Tanzania ninaahidi kuenzi mafanikio
    ya awamu inayomaliza muda wake , kustawisha utulivu katika uendeshaji wa mpira, na kufanya
    jitihada za kubuni, kuboresha na kustawisha maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania. Jitihada kubwa
    zitawekwa kwenye maeneo makuu yafuatayo:
    1. Ufundi (Technical)
    1.1 Muundo wa Idara ya Ufundi
    Katiba ya TFF imeainisha wazi kuwa TFF ndiye msimamizi mkuu wa mpira wa miguu
    Tanzania, hivyo jukumu la kuleta maendeleo ya mchezo huu kwa kiasi kikubwa linaiangukia
    TFF.Ni kwa msingi huu basi asilimia kubwa ya rasilimali za TFF lazima iwekezwe katika
    kuleta maendeleo ya mpira. Kwa mfumo wetu wa uendeshaji, kichocheo kikuu cha maendeleo
    ya mpira ni idara ya ufundi ya TFF. Hivyo idara hii ya ufundi inapaswa kuwa ndiyo idara
    mama ya TFF ambayo inapaswa kuongoza kwa matumizi ya fedha, idadi ya waajiriwa na
    matumizi ya rasilimali nyingine za TFF . Kwa sasa pale TFF hali sivyo ilivyo. Iwapo
    nitachaguliwa nitapendekeza jukumu la kwanza la Kamati ya utendaji liwe ni kurekebisha na
    kuboresha mfumo wa uendeshaji wa idara ya ufundi. Nitapendekeza idara ya ufundi iendelee
    kuongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi na chini yake awe na wakurugenzi wasaidizi wa vitengo
    watatu Mkurugenzi Msaidizi (ufundi), Mkurugenzi Msaidizi (Elimu na Mafunzo) ambaye kwa
    sasa anaitwa Education officer, na Mkurugenzi Msaidizi (Maendeleo ya mpira).
    Kitengo cha Ufundi kitahusika na kubuni na kusimamia shughuli zote zinazohusu maendeleo
    ya Timu za Taifa kuanzia za wakubwa hadi za vijana. Hii itakuwa ni pamoja na kuandaa
    mitaala ya taifa (national football curriculum) ya ufundishaji wa mpira Tanzania kuanzia umri
    wa miaka mitano hadi watu wazima. Walimu wa Timu za Taifa wataripoti kwake.
    Kitengo cha Elimu na Mafunzo kitahusika na kubuni na kuratibu kozi zote na mafunzo yote
    yanayohusiana na mpira kama vile kozi za Marefa, Makocha, Madaktari, Makamisaa,
    Watawala, Waandishi wa Habari za Michezo, n.k.
    Kitengo cha Maendeleo ya mpira kitahusika na kubuni,kuratibu na kusimamia mpango wa
    maendeleo ya vijana (grassroot) na kutafuta vipaji (scouting). Kitengo hiki kitafanya kazi kwa
    kushirikiana kwa ukaribu na idara za Serikali hasa idara za Elimu,Vijana na TAMISEMI,
    Halmashauri,Mashirika ya umma,Sekta binafsi pamoja na Taasisi nyingine za kijamii.
    Wakuu wa vitengo hivi wataajiriwa kwa kufuata vigezo makini na bila upendeleo wala
    kujuana.
    1.2 Ujenzi wa Kituo cha Mpira (Football Centre of excellency)
    Hiki ni Kituo Maalum cha mafunzo ya mpira wa miguu. Katika kituo hiki kunakuwa na kila
    aina ya miundo mbinu, viwanja vya kufundishia mpira, vituo vya tiba,madarasa ,maabara za
    utafiti,hosteli n.k Kituo hiki pia kinakuwa ndio sehemu kuu ya kuweka kambi za timu za Taifa
    na kutoa mafunzo ya ufundi yakiwemo ya ukocha, urefa, utawala na tiba. Wenzetu wa Senegal
    na Ethiopia kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira Africa CAF wameweza kujenga vituo hivi
    na matokeo yake tunayaona.Cameroon pia wana kituo hiki.
    Pamoja na gharama zake kuwa kubwa, cha muhimu hapa ni kuweka nia, kutafuta ardhi kwa
    kushirikiana na Serikali na kuanza ujenzi taratibu.Kwa kuwa klabu ya Sunderland ya Uingereza
    na kampuni ya kufua umeme ya Symbion wameonyesha nia ya kushirikiana naSerikali kujenga
    kituo cha michezo itakuwa vyema iwapo TFF itashirikiana na taasisi hizi muhimu ili kufikia
    azma ya kujenga kituo hiki cha kisasa. Iwapo nitachaguliwa nitasimamia uanzishwaji wa mradi
    huu muhimu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kulikomboa soka letu.
    Aidha uwanja wa Karume yalipo makao makuu ya TFF utazungushiwa jukwaa ili mechi
    ambazo sio kubwa zifanyike pale, Hii itaiongezea TFF mapato na vilabu pia.
    1.3 Timu Kupanda Daraja
    Ili kuongeza ushindani na kupanua mpira uchezwe kona zote za nchini ( to spread the game)
    ,mtindo wa kucheza kikanda ili kupata timu za kupanda daraja kuu utakuwa ni wa kudumu na
    utaimarishwa kwa kutafutiwa udhamini na kuboreshwa viwanja kwa kushirikiana na wamiliki
    wa viwanja hivyo. Usimamizi wa mashindano ngazi hii utaimarishwa na kusimamiwa kwa
    karibu zaidi ili timu itakayopanda daraja iwe imepanda kwa haki na hivyo kuleta ushindani
    Ligi Kuu.
    Hata hivyo waraka uliotolewa na TFF ukiagiza mikoa ichezeshe ligi ili kupata bingwa wa
    mkoa utafutwa kwa sababu hautekelezeki kutokana na hali ya uchumi na uhalisia wa jiografia
    ya mikoa ya Tanzania. Mathalani Mkoa wa Mtwara ukichezesha ligi ya mkoa (kwa maana ya
    nyumbani na ugenini) ina maana bingwa wa Wilaya ya Masasi atasafiri vipi akacheze
    Newala au Mkoani Lindi bingwa wa Liwale atasafiri vipi akacheze na bingwa wa Kilwa ,
    Pwani bingwa wa Mafia atasafiri kwa gharama za nani akacheze Bagamoyo na wa Kibaha
    akacheze Utete? Pamoja na nia njema ya TFF uhalisia hauruhusu. Kama Mwenyekiti wa chama
    cha mpira mkoa wa Kagera nalijua hili, hakuna haja ya TFF kuwa inatoa maelekezo ambayo
    hayatekelezeki, hasa ukizingatia kuwa TFF hakuna msaada wanaopeleka kusaidia mikoa na
    wilaya ziandae mashindano yao.Vyama vya mikoa na wilaya viachwe viendelee kutumia
    ubunifu wao kupata mabingwa wao kulingana na hali halisi ya mazingira yao.
    1.4 Kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani
    Wataalam wa kandanda wanasema kuwa ili mchezaji awe katika kiwango bora inabidi acheze
    kwa mwaka kimashindano wastani wa mechi 40. Ligi yetu kuu,Vodacom premier
    league,inatoa fursa kwa mchezaji kucheza michezo 26 kwa mwaka iwapo anapangwa kila
    mechi.Hii haitoshi. Namna pekee ya kurekebisha hali hii ni kuongeza idadi ya mashindano kwa
    mwaka.Hili litafanyika kwa kufufua kombe la Taifa (Taifa cup) na kuanzisha kombe la
    shirikisho (kama FA cup ya Uingereza). Kombe la shirikisho litashirikisha timu zote nchini
    kuanzia ngazi ya kata,tarafa,wilaya,mkoa hadi Taifa na bingwa wake atawakilisha nchi katika
    kombe la shirikisho la Afrika CAF confederation cup (kama ilivyo Kenya kwa sasa).
    1.5. Mpira wa Wanawake
    Hadi sasa hatuna mfumo imara na unaoeleweka wa kuendeleza soka la kinamama. Mpira wa
    wanawake umeanzia Wilaya ya Kinondoni, ukakulia Wilaya ya Kinondoni na umegotea
    Wilaya ya Kinondoni ambako kuna timu zenye majina kama Mburahati Queens na Sayari
    Queens. Mpira wa wanawake sharti usambae nchi nzima, na ili kufanikisha azma hii lazima
    yaanzishwe mashindano ya kitaifa ya wanawake ikiwemo Ligi ya taifa ya wanawake. Hii
    itaendana na juhudi za kuongeza makocha, waamuzi na makamisaa wanawake na kutafuta
    udhamini kwa timu ya Taifa ya wanawake TWIGA STARS.
    1.6 Maandalizi ya Vijana (Grassroot Programme)
    Mpango endelevu wa maendeleo ya soka la vijana sharti uandaliwe, uratibiwe na kusimamiwa
    kwa makini. Program madhubuti ya maendeleo ya mpira wa vijana lazima ibuniwe ,iratibiwe
    na kusimamiwa kwa usatadi mkubwa.Mradi huu lazima ulenge ,kwa hatua,kufikia hatua ya
    kuingiza timu zetu fainali za kombe la Afrika la vijana chini ya umri wa miaka 17 na 20,fainali
    za olimpiki, fainali za Afrika wachezaji wa ndani CHAN,fainali za Afrika AFCON na mwisho
    fainali za kombe la dunia.Hii itakuwa ni pamoja na kujiwekea utaratibu wa mzuri wa
    kuhakikisha vijana wetu wanapata fursa ya kucheza mpira nje ya nchi ili kujiongezea
    umahiri.Na hii ni kwa wanawake na wanaume.
    Mpango huu ni lazima ushirikishe Serikali Kuu (hasa Wizara zenye dhamana ya Michezo,
    Elimu na Halmashauri), Taasisi zisizo za kiserikali,mashirika ya umma,sekta binafsi na
    TFF,CAF na FIFA. Ushirikishwaji wa Serikali na Halmashauri katika program hii ni muhimu
    sana kwa kuwa ndio wasimamizi na wamiliki wa shule nyingi za msingi ambako ndiko vijana
    wetu wanakoanzia kucheza mpira. Mpango kazi huu lazima uonyeshe:
    1. Nini tunataka kufanikisha.
    2. Utaratibu utakaotumika.
    3. Nguvu kazi inayotakiwa na sifa zake.
    4. Mwongozo wa kufuatilia kupima ufanisi wa programu.
    5. Kupambanua gharama za mpango na taratibu za uchangiaji wake.
    Hatua muhimu katika kufanikisha program hii zitakuwa ni:
    -Kufundisha walimu wa walimu (instructors), hawa ndio watakuwa chachu ya kupata
    walimu wa mpira mashuleni na mitaani.
    -Walimu wa walimu (instructors) kufundisha walimu wa kutosha wa michezo mashuleni na
    mitaani
    -Kwa kushirikiana na wamiliki wa shule kuhakikisha viwanja vya kuchezea vinakidhi
    viwango
    -Kutafuta na kusambaza vifaa vya michezo mashuleni hasa mipira ya saizi muafaka kwa
    mujibu wa viwango vya kimataifa.
    -Kupata shule angalau moja kila mkoa itakayopokea watoto wenye vipaji maalum vya
    kucheza mpira, pale ambapo wazazi hawataweza kuwalipia karo vijana hawa basi TFF
    ihakikishe karo zao zinapatikana,huo ndio uwekezaji katika mpira.
    -Kuandaa mashindano mbali mbali yatakayoshirikisha shule hizi ili kupata timu za taifa za
    vijana wa umri mdogo wa kike na wa kiume.
    -Kuhakikisha timu hizi za umri mdogo zinapata fursa ya kushiriki mashindano mbali mbali
    ya kimataifa
    - Kupata vikosi vizuri vya timu za taifa za vijana wa umri mdogo ambao watakua pamoja,
    hao ndio watajenga msingi imara wa timu za Taifa za wakubwa kwa miaka ya baadae.
    Itakuwa ni muhimu sana program hii iendane vizuri na ratiba nyingine za mashindano ya
    kitaifa kama Umitashumta, Umisseta, Airtel rising star, Copa Coca Cola n.k.
    - Kuanzisha mashindano ya kitaifa ya kombaini za shule za sekondari na ya kombaini za
    vyuo vikuu. Wachezaji mahiri wa timu ya taifa kama Leodeger Chilla Tenga (Rais wa
    TFF) na Leopold Tasso Mkebezi (meneja wa Taifa stars) waliibukia kwenye
    mashindano kama haya Mkebezi akiwa beki wa kombaini ya sekondari za
    Bukoba,Ihungo,Kahororo na Nyakato.
    Aidha vituo vya michezo (sports academies) ambavyo tayari vipo vitatengenezewa utaratibu
    wa usajili na kuwekewa utaribu wa kuviendesha.
    Ili kuondoa ulalamishi wa vituo vya mafunzo (Academies) kulalamikia malipo pindi mchezaji
    akisajiliwa timu kubwa, vituo vyote vya vijana vitasajiliwa na vijana wao wote wataingizwa
    kwenye kumbukumbu za TFF (data base) kwa majina, saini na picha,hii itasaidia kuzuia sakata
    kama la Mbwana Samata na klabu yake ya utotoni ya Mbagala maana kumbukumbu za TFF
    zitakuwa ndio jibu la maswali yote.
    1.7 Tiba
    1. Tutaimarisha usalama uwanjani. Tutahimiza kila uwanja zinakochezwa mechi za ligi kuwe na
    gari la wagonjwa na chumba cha dharura (emergency room).
    Katika kuimarisha usalama tutahakikisha vifaa muhimu vya dharura kama vifaa vya hewa
    (oxygen) na vifaa vya kushtua moyo (defibulator) vinakuwepo. Kwa sasa hapa Tanzania
    uwanja pekee wenye vifaa hivi ni Uwanja wa Azam Chamazi. Ni jambo la kusikitisha kuona
    hata uwanja mpya wa Taifa hauna chumba cha tiba dharura (emergency room) na kibaya zaidi
    makato ya uwanja hayaendi kuanzisha huduma hii muhimu wakati viongozi mbalimbali wa
    kitaifa wanahudhuria mechi uwanjani.
    2. Mradi wa Goal Project wa FIFA unatoa pesa za tiba na mradi huu uliweka lengo la kuwa na
    chumba cha kliniki pale uwanja wa Karume. Tutakifufua chumba hiki, tutakiwekea vifaa na
    kuhakikisha huduma ya kliniki kwa wanamichezo iliyokuwa ikitolewa na madaktari kila
    Jumapili inarudishwa. Posho itatafutwa ili madaktari watoa huduma angalau wapate nauli na
    maji ya kunywa.
    3. Wakati wa kujadiliana mikataba na wadhamini mbalimbali tutahakikisha kipengele cha
    huduma za afya kinaingizwa katika mikataba. Udhamini utatafutwa kwa ajili ya vipimo vya
    wachezaji kabla ya league (pre-league medical test) kama vile vipimo vya uvumilivu (Yo-Yo
    test) na vipimo vya moyo (cardiac tests). Hii ni kwa ajili ya usalama wa wachezaji na
    waamuzi.
    4. Hadi leo chama cha Madaktari Tanzania, TASMA hakina ofisi. Hii ni aibu kwa chama chenye
    hadhi na umuhimu wa kipekee kama hiki. Tutahakikisha TASMA inapata ofisi yake pamoja
    na chumba maalum cha kliniki.
    5. Huduma ya afya lazima iwe sehemu maalum ya mfumo wa idara ya ufundi. Ni muhimu timu
    ya madaktari wa Timu ya Taifa (National Medical team) ijulikane ni kina nani na wapewe
    mikataba ya kazi. Hii tutalipigania.
    6. Majeraha ya michezo huwa yanahitaji utaalam wake wa tiba. Tutaiomba Serikali itupe
    ushirikiano ili kipatikane kitengo maalum cha kutibu majeraha ya wanamichezo (sports
    injuries wing) katika baadhi ya hospitali zetu wakati tunajiandaa kuwa na kitengo cha tiba
    (Rehabilitation Centre) katika kituo cha michezo kitakachojengwa.
    7. Ili kuimarisha uwezo wa madaktari wetu kutoa huduma za afya kwa wanamichezo,
    tutahakikisha madaktari wengi kadiri iwezekanavyo wanapata kozi za msingi,kati na juu
    (preliminary,intermediate and advanced). Nafasi hizi zitatolewa bila upendeleo wala kujuana.
    8. Utoaji wa ushauri nasaha kwa wachezaji utaongezeka hasa kuhusu masuala ya ukimwi na
    madhara ya madawa ya kuongeza nguvu na ya kulevya.
    1.8 Waamuzi
    Imepita miaka zaidi ya 15 toka Tanzania itoe mwamuzi wa kimataifa wa kuchezesha fainali kubwa
    (mara ya mwisho AFCON 1998), hii si sawa. Utaratibu uliopo sasa wa kuwapata na kuwaendeleza
    waamuzi ama una mapungufu au haufai kabisa hivyo budi utafutwe utaratibu ulio mzuri zaidi katika
    kupata waamuzi bora, tafiti zitafanywa ili kubaini ni njia zipi za kisayansi za kuwapata waamuzi bora
    (Top referees).Semina za mara kwa mara za CAF na FIFA ni nzuri lakini hazitoshi, TFF lazima
    iwekeze kwa kutoa mafunzo zaidi ya waamuzi kwa gharama zake.
    Aidha mradi wa maendeleo ya mpira kwa vijana (grassroot) utahusisha pia mafunzo ya uamuzi wa
    mpira kwa vijana kama kinavyofanya kituo cha Jenerali Twalipo.
    Utaratibu wa kutoa adhabu kwa waamuzi wanaosemekana wameboronga uwanjani nao unahitaji
    marekebisho ya haraka sana. Uamuzi wa mpira ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine,mwamuzi
    akikosea ni vyema akakosolewa na mwamuzi mwenzie ambaye ni mwandamizi,na kama ni
    kuadhibiwa aadhibiwe na jopo la waamuzi wenzie waandamizi lakini wastaafu na sio mtu mwingine
    ambaye hajawahi kupuliza filimbi.
    1.9 Makocha
    Kumekuweko na utamaduni usiofaa katika soka la Tanzania miaka ya karibuni wa kuona kuwa
    makocha wa kigeni ndio bora zaidi na wanastahili mikataba, mishahara minono na marupurupu
    ilhali makocha wazawa wanageuzwa ‘deiwaka’, jambo hili ni baya sana, ajira ziheshimiwe kwa
    msingi wa taaluma na sio kwa msingi wa nchi atokayo mtu.
    Makocha wetu wazalendo wana uwezo mkubwa kama wakipewa nyenzo kama wanazopatiwa
    wageni, kama malipo mazuri, mikataba ya muda mrefu, vitendea kazi na kuheshimiwa program
    zao bila kuingiliwa na viongozi.Iwapo nitachaguliwa ninaahidi:
    - Kuwaendeleza makocha kimafunzo ndani na nje ya nchi kwa wale wenye uwezo na
    utashi wa kufanya hivyo.
    - Kushawishi taasisi za elimu nchini kama vyuo vikuu kufundisha taaluma ya ukocha
    - Kuhakikisha walimu wa mpira wa timu zetu za Taifa wanakuwa na mikataba stahiki, hii
    ni pamoja na benchi zima la ufundi.
    - Kuwajengea uwezo makocha wetu wazalendo ili nao wapate fursa ya kufundisha mpira
    nje ya nchi.
    - Kuanzisha tuzo za kila mwaka za makocha wazalendo ambao wamefanya vizuri katika
    ufundishaji wa soka la vijana la wanawake na wanaume.
    - Kuhakikisha utaratibu wa leseni za CAF unazingatia vigezo vya kitaaluma, uzoefu na
    ushiriki wa kocha mhusika katika ufundishaji. Makocha ambao wanafundisha (active
    coaches) watapewa kipaumbele katika kupata kozi za kupanda madaraja kuliko wale
    wanaofungia vyeti makabatini.Leseni za CAF ni muhimu katika kumfanya mwalimu wa
    mpira atambulike kimataifa.
    - Kuhakikisha kanuni za ligi zinasimamiwa vyema ikiwemo kanuni itakayomlazimisha
    kila mwalimu wa ligi kuu na daraja la kwanza awe mwanachama wa TAFCA (chama
    cha makocha nchini), walimu wa kigeni watapewa uanachama wa muda.
    1.10 Timu za Taifa
    Timu zetu za Taifa, ziwe za wakubwa au za vijana ndio kioo cha mpira wa Tanzania. Jitihada
    zote lazima zifanyike kuhakikisha tunakuwa na timu nzuri za Taifa kuanzia za wakubwa
    (wanawake/wanaume) hadi za vijana. Pamoja na jitihada zitakazofanyika kuboresha idara ya
    ufundi kama ilivyoanishwa hapo juu lakini pia yafuatayo ni mambo ya ziada yatakayofanyika.
    (a) Kuandaa fainali za Afrika za umri chini ya miaka 17 (U-17) mwaka 2019
    Hadi sasa hakuna nchi ambayo imekwisha pata uenyeji wa mashindano haya. Uenyeji huu
    unatolewa na Shirikisho la vyama vya mpira Afrika CAF.Hii ni changamoto kwetu
    Watanzania kuomba uenyeji huu.Tukipewa fursa hii itatusaidia sana kutusukuma tuanze
    kuandaa programu ya nguvu ya miaka mitano ya kupata timu yetu itakayocheza katika
    fainali hizi kama wenyeji. Aidha kama nchi tutalazimika kuboresha miundo mbinu yetu
    hususani viwanja vyetu vya mpira, jambo ambalo litatusaidia siku za usoni. Ninaamini
    uwezo wa kuandaa mashindano haya kama nchi tunao. Nikichaguliwa nitalisimamia hili.
    (b) Nidhamu
    TFF itaandaa Kanuni za Nidhamu (code of ethics) kwa wachezaji, walimu na viongozi wa
    Timu za Taifa mara wawapo ndani na nje ya uwanja. Hii itasaidia kujenga nidhamu ya
    timu. Kanuni hizi zitaendana sambamba na kanuni za maadili za TFF.
    (c) Walimu
    Ni vyema siku za usoni timu zetu zote za Taifa zikafundishwa na makocha wazawa.
    Utaratibu utafanyika kuhakikisha makocha wasaidizi ambao ni wazawa wanaendelezwa
    kufikia kiwango hicho, hii itakuwa ni pamoja na kuwapatia fursa za mafunzo ndani na nje
    ya nchi.
    (d) Zanzibar
    TFF kwa kushirikiana na Chama cha Mpira Zanzibar ZFA tutahakikisha kunakuwa na
    mahusiano ya karibu ya walimu wa timu za Taifa Zanzibar na Bara ili kuhakikisha timu
    bora ya Taifa inaundwa na vijana wa pande mbili za Muungano. Aidha jitahada za Zanzibar
    kuwa mwanachama kamili wa CAF na FIFA zitaendelea kuungwa mkono.
    2. Utawala
    Inabidi tuendeleze utamaduni wa kuendesha shughuli za TFF kitaasisi (to have a corporate
    culture).Nguzo muhimu za uendeshaji shirikisho kitaaluma ni pamoja na kujenga nidhamu ya
    wafanyakazi,heshima kwa uongozi,utunzaji wa kumbukumbu,ukarimu kwa wageni,umakini
    katika manunuzi na utunzaji wa fedha pamoja na kufanya kazi kwa malengo na kuhakikisha
    malengo hayo yamefikiwa.
    Maeneo yafuatayo yataboreshwa ili kuongeza ufanisi:
    2.1 Ofisi za Mikoa na Vyama Shiriki
    Kwa kuzingatia vyama vya Mikoa kuwa ndio muendelezo mkuu wa shughuli za TFF Mikoani,
    ni muhimu ofisi za mikoa zikawa kielelezo cha ufanisi wa utendaji wa TFF. Ofisi za Mikoa
    zitaboreshwa hasa kwa kupewa vitendea kazi hususani vifaa vya mawasiliano.
    Vyama shiriki hadi sasa havina ofisi zenye hadhi ya vyama hivi, tutahakikisha tunaondoa aibu
    hii. Aidha kutokana na mapato ya TFF sehemu ya mapato haya itatengwa kwa ajili ya ruzuku
    ya kupeleka kwenye vyama vya Mikoa na vyama shiriki ili isaidie kupunguza makali ya
    kuendesha vyama vyetu.
    2.2 Ofisi ya Rais
    Kutakuwa na ofisi ya Rais wa TFF. Ofisi ya Rais wa TFF (office of the President) lazima
    iimarishwe na iwe sehemu itakayoweza kukabiliana na changamoto za maendeleo ya mpira
    wa miguu. Rais wa TFF ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za mpira wa nchi hii,lazima
    awe na mahali stahili pa kufanyia kazi kulingana na hadhi yake.Hii itakuwa ni pamoja na
    kuwa na wasaidizi wenye uweledi wa kutosha katika shughuli za kila siku za kuongoza
    shirikisho.
    Ofisi za TFF makao makuu uwanja wa Karume zitakarabatiwa na kuongeza nafasi ya
    kufanyia kazi.
    2.3 Maslahi
    Maslahi ya wafanyakazi wa TFF yataboreshwa ili kuwaongezea motisha. Hii itakuwa ni
    pamoja na kuwapa fursa ya kuhudhuria mafunzo mbalimbali.
    2.4 Vilabu vya Mpira
    Vilabu vitasaidiwa kupewa mwongozo wa kujiendesha kwa ufanisi zaidi. Aidha utaratibu wa
    mgawanyo wa mapato ya milangoni utatazamwa upya kwa lengo la kuhakikisha vilabu
    vinapata mgao mkubwa kuliko iliyo sasa. Hii ni kwa kuzingatia gharama kubwa wanazoingia
    vilabu katika kuandaa timu ikiwemo malazi, usafiri, vifaa, posho, dawa, mishahara n.k.
    2.5 Wachezaji wastaafu
    Hii ni hazina ya Taifa,kustaafu kwao kucheza mpira sio mwisho wao wa kuchangia maendeleo
    ya mpira wa nchi yetu.Jitihada zitafanyika kuanzisha mfuko maalum (Trust Fund) ambao
    utachangiwa na wachezaji wenyewe wanapokuwa bado dimbani pamoja na TFF, hii ni kwa ajili
    ya kuwasaidia hapo baadae wanapokuwa na matatizo hasa ya ugonjwa. Aidha chama cha
    wachezaji wastaafu (SPUTANZA) kitapewa ofisi na kitaimarishwa ili kiwe kiungo muhimu
    kati ya wachezaji na TFF.Wachezaji watahimizwa watumie chama hiki kutatua matatizo yao na
    chama kitapewa fursa kikanuni ya kuwa mtetezi mkuu na msimamizi wa maslahi ya wachezaji.
    2.6 Mikataba
    Utaratibu wa TFF kuingia mikataba na wadhamini mbalimbali utarekebishwa ili kuongeza
    uwazi. Ipo mikataba ambayo imesainiwa na TFF ambayo imesababisha vyama vya mikoa na
    wilaya, pamoja na uhaba wao wa pesa, wahangaike kutafuta fedha za zaida kuandaa timu zao
    kwa ajili ya mashindano yanayobeba jina la mdhamini kwa kuwa fedha anayotoa mdhamini
    haikidhi uendeshaji wa mashindano yenyewe.
    Aidha vipengele tata vinavyokandamiza maslahi ya vilabu katika baadhi ya mikataba
    inayosainiwa kati ya TFF na wadhamini vitarekebishwa kama sio kuondolewa kabisa kwa
    maslahi ya ustawi wa mpira wetu. Haki za vilabu katika matangazo ya biashara yahusuyo
    mpira zitalindwa kwa nguvu zote.
    2.7 Utaratibu wa Mashindano
    Yapo mashindano ya vijana kama Umiseta na Umitashumta yanayoandaliwa na Serikali. Kuna
    wakati mashindano kama haya yanafanyika sambamba na mashindano yanayoandaliwa na TFF
    kama vile Copa Coca Cola. Yote haya ni mashindano ya vijana, na washiriki wanakuwa ni
    vijana toka shule hizo hizo. Kwa nini tugombee fito wakati tunajenga nyumba moja? Ni
    vyema kalenda ya mashindano ya vijana kitaifa ikaandaliwa kwa pamoja kati ya Serikali na
    TFF.
    2.8 Usajili wa Vyama vya Mpira vya Wanawake
    Usajili huu haujakamilika nchini nzima hususani ngazi ya wilaya. Juhudi zitafanyika
    kukamilisha zoezi hili ili mpira wa wanawake uenee kote Tanzania.
    2.9 Kitengo cha habari
    Kitengo hiki kitaboreshwa kwa kuongezewa nyenzo za kufanyia kazi na kukipatia fursa zaidi
    za mafunzo. Aidha majukumu yake yataongezwa ili pia kishughulikie mahusiano ya
    kimataifa.Hivyo kama nikichaguliwa nitapendekeza mkuu wake aitwe ‘Afisa habari na
    mahusiano ya kimataifa’.
    3. Masoko na Uwekezaji
    Mpira unaendeshwa kwa fedha nyingi. TFF ili iweze kujiendesha kwa ufanisi ni lazima iwe na
    vyanzo vya uhakikika vya mapato. Ili kufanikisha azma hii kitengo cha masoko na uwekezaji
    kitahakikisha kwamba:
    1. TFF inatengeneza utaratibu mzuri wa kuuza bidhaa zake ndani na nje ya nchi kwa kupitia
    uuzaji wa kawaida na wa mtandao.Mikataba itaandaliwa ili kudhibiti uuzwaji holela wa
    bidhaa za TFF.
    2. Vyumba vya Maduka vinajengwa kuzunguka uwanja wa Karume na kukodishwa.
    3. Jengo la kitega cha uchumi litajengwa kwenye ardhi ya Uwanja wa Karume.Pia jukwaa la
    watazamaji litajengwa uwanja wa Karume ili mechi ambazo sio kubwa ziweze kufanyika
    pale, hii itaviongezea vilabu mapato.
    4. Juhudi za kuboresha ukusanyaji, usimamizi na mgawanyo wa haki wa mapato ya milangoni
    yatokanayo na ligi yetu utaboreshwa ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya kupitia njia
    mbali mbali zikiwemo za udhamini mbadala kwa vilabu.Aidha jitihada ambazo tayari
    zimekwisha anza za kuunda bodi ya kuendesha ligi na uanzishwaji wa utaratibu huru wa
    kuendesha ligi zitaendelezwa ili kuongeza ufanisi,kuinua mapato ya vilabu na kuongeza
    msisimko wa ligi.Ninaunga mkono juhudi hizi.
    5. Viwanja vingi vya mpira nchini vinamilikiwa aidha na Halmashauri,Serikali kuu
    au vyama vya siasa.Viwanja hivi vingi viko katika hali mbaya kuanzia nyasi ,hali
    ya uzio,vyumba vya kubadilishia nguo,mageti,vifaa vya kuzimia moto n.k.ni
    vyema TFF na vyama vya mikoa kwa kupitia utaratibu wa PPP (Public Private
    Sector Partnership) vikaingia ubia na wamiliki wa viwanja hivi ili TFF na
    washirika wake wachukue jukumu la kuviboresha,kuvisimamia na kuviendesha ili
    kuhakikisha vinakuwa katika viwango stahili kwa mujibu wa kanuni za FIFA na
    CAF.Hii itaongeza usalama wa wachezaji na watazamaji na kuinua mapato
    yatokanayo na viwanja hivi
    Ushiriki wa wadau
    Kwa sasa taswira ya mpira wa miguu inawafungia nje wadau wengi ambao kama wangepewa fursa
    ya kushiriki nao wangetaka wachangie maendeleo ya mpira wa miguu.Juhudi kubwa inabidi zitumike
    kurudisha imani hii ili kuleta hisia za umoja wa kitaifa katika kuendesha mpira wetu (sense of
    belongingness) .Ni muhimu taasisi muhimu za kitaifa zishirikishwe katika sekta hii ya mpira wa
    miguu ,hii ni pamoja na taasisi kama Tacaids,Mashirika ya utalii kama TANAPA na TTB,Umoja wa
    wafanyabiashara kama TPSF,CTI na TCCIA ,Kituo cha uwekezaji TIC n.k.Ushirikiano huu utasaidia
    kujenga jina la Tanzania pale tunapoandaa michuano ya kimataifa na pia kuhamasisha vijana wetu
    waepuke maisha hatarishi kama vile kujihusisha na ngono isiyokuwa salama,madawa ya kulewa
    (kutumia na kusafirisha),ulevi wa kupindukia n.k.
    HITIMISHO
    Ndugu zangu,nihitimishe kwa kusisitiza kuwa maendeleo ya mpira Tanzania kwa hapa
    yalipofikia yanahitaji ubunifu,ujasiri na msukumo mpya ili tuweze kuunyanyua mpira wetu na
    kuupa mwelekeo mpya,mwelekeo wa matumaini ,mwelekeo wa kulipeleka soka letu katika
    kushinda vikombe vikubwa barani mwetu Afrika na Duniani.
    Shime wapiga kura nipeni fursa hii ya kuwa Rais wa TFF ili kwa pamoja tukishirikiana na
    wadau wote muhimu katika sekta yetu tuweze kulisikuma gurudumu hili ili hatimae soka iweze
    kuiletea nchi yetu sifa na kuwapa raha mamilioni ya watanzania wapenda mpira.
    Pamoja tutaweza
    Chagua MALINZI
    Chagua MABADILIKO
    Mungu ibariki Afrika
    Mungu ibariki Tanzania
    Jamal Malinzi
    Mgombea nafasi ya Urais
    TFF
    2013
    Mpira ni afya, mpira ni burudani, mpira ni ajira kwa vijana!
    MAELEZO BINAFSI YA JAMAL EMIL MALINZI MGOMBEA URAIS TFF
    Tarehe ya kuzaliwa : 08 Agosti, 1960
    Elimu: 1974-1977 : Sekondari O-Level
    Mwanza Secondary School
    1978-1981 : A-Level
    Ilboru High School
    1980-1981 : JKT – Ruvu
    Operesheni TIJA
    1981-1985 : Chuo Kikuu Dar Es Salaam
    Digrii ya Uhandisi (Upper 2nd Class)
    1986-1993 : Ajira -Coopers and Lybrand
    Tanzania Industrial Research
    and Development Organization
    1993-Hadi Leo : Mjasiriamali
    Mkurugenzi – Cargostars Limited
    Michezo : Nimekuwa promota wa mchezo wa ngumi za kulipwa
    kuanzia kipindi cha 1995-2001. Baadhi ya mabondia
    wangu walifikia kiwango cha kimataifa hadi kusaini
    mkataba na Promota maarufu duniani Don King.
    : Nimekuwa Seneta wa Yanga na baadae nikawa
    Mkurugenzi na mwisho nikawa Katibu Mkuu wa Klabu
    ya Yanga kati ya mwaka 1999 na 2005.
    : Nimekuwa Mkurugenzi na Msimamizi Mkuu wa Timu ya
    Mkoa wa Dar Es Salaam ya Mzizima United. Timu hii
    ndiyo ya mwisho kushinda Kombe la Taifa mwaka 2007
    ikiwa timu moja ya Mkoa wa Dar Es Salaam.
    : Nimekuwa mjumbe wa Baraza la michezo la mkoa wa
    Dar es salaam 2009-2011
    : Nimekuwa Mwenyekiti wa kamati ya mashindano mkoa
    wa Pwani 2009-2011
    : Hadi sasa mimi ni mwenyekiti wa Chama cha mpira wa
    miguu mkoa wa Kagera
    : Kikampuni, Kampuni yetu ya Cargostars Limited ina
    uzoefu wa muda mrefu wa kudhamini michezo
    mbalimbali. Kwa kipindi cha miaka saba Cargostars
    Limited iliidhamini mbio za marathon za wabunge.
    Aidha Cargostars Limited ina rekodi ya kudhamini
    michezo mingine kadhaa ikiwemo mpira wa miguu,
    ngumi, Tennis na Golf,".
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI AZINDUA KAMPENI ZA KURITHI KITI CHA TENGA TFF LEO, AAHIDI MAMBO MAKUBWA SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top