• HABARI MPYA

  Wednesday, October 23, 2013

  SIMBA SC YAREJEA KILELENI LIGI KUU RA

  Na Mahmoud Zubeiry, Tanga 
  SIMBA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara licha ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo. 
  Matokeo hayo yanaifanya Simba SC itimize pointi 20 baada ya kucheza mechi 10, sawa na Azam na Mbeya City, lakini Wekundu wa Msimbazi wanapaa kileleni kutokana na wastani wao mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
  Simba SC ina mabao 12 baada ya kutoa mabao ya kufungwa, wakati Azam ina mabao tisa (GD) na Mbeya City mabao sita.
  Beki wa Coastal Union, Juma Nyosso kulia akipambana na mshambuliaji wa Simba SC, Amisi Tambwe Uwanja wa Mkwakwani leo.

  Katika mchezo wa leo, Uwanja wa Mkwakwani, timu zillicheza sawa vipindi vyote, lakini zilishindwa kutengeneza nafasi za maana za kufunga mabao. 
  Simba SC ilipata pigo dakika ya 33 baada ya kipa wake namba moja, Mganda Abbel Dhaira kuumia alipogongana na Haruna Moshi ‘Boban’ na kutoka dakika mbili baadaye, nafasi yake ikichukuliwa na kipa aliyepandishwa kutoka Simba B msimu huu, Abuu Hashim.
  Mashabiki wa Coastal walidhani kutoka kwa Dhaira ungekuwa ufunguo wa kupata mabao kwao, lakini dogo Abuu Hashim alionyesha umahiri mkubwa kudaka krosi na michomo ya aina zote, akilinda vyema lango la Wekundu la Msimbazi.
  Burudani ilikuwa pale mshambuliaji wa Simba SC, Mrundi Amisi Tambwe alipokuwa akikutana na beki wa Coastal Union, Juma Nyosso ambaye alipania kumzuia mchezaji huyo wa zamani wa Vital’O ya Burundi asifunge. 
  Lakini mara nyingi Tambwe alifanikiwa kumtoka Nyosso tena kwa ustadi wa hali ya juu na kuwafanya mashabiki wa Simba wampe shangwe zake. 
  Haruna Moshi ‘Boban’ naye alikuwa anasababisha starehe kwa mashabiki kila alipokutana na beki Mrundi, Kaze Gilbert wa Simba SC. Kaze alikuwa mwisho wa machachari ya Boban hii leo, kwani alifanikiwa kumtibulia mipra mara kadhaa.
  Coastal hii leo iliongozwa na wachezaji wake zamani, beki Joseph Lazaro na mshambuliaji Razack Yussuf ‘Careca’ baada ya kumtimua Mzanzibari, Ahmed Morocco.
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Abbel Dhaira/Abuu Hashimu dk35, Nassor Masoud ‘Chollo’/Edward Christopher dk67, Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, William Lucian ‘Gallas’, Said Ndemla, Amisi Tambwe, Amri Kiemba/Zahor Pazi dk46 na Ramadhani Singano ‘Messi’.
  Coastal; Shaaban Kado, Mbwana Hamisi, Othman Tamim, Marcus Raphael, Juma Nyosso, Jerry Santo, Daniel Lyanga/Uhuru Suleiman dk77, Chris Odula, Yayo Lutimba, Haruna Moshi ‘Boban’ na Kenneth Masumbuko/Pius Kisambalae dk86.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAREJEA KILELENI LIGI KUU RA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top