• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 24, 2013

  DHAIRA HAJAUMIA SANA JANA MKWAKWANI, KUREJEA LANGONI SIMBA NA AZAM JUMATATU TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, Tanga
  KIPA wa namba moja wa Simba SC, Abbel Dhaira amesema kwamba hakupata maumivu makubwa jana pamoja na kutoka nje kipindi cha kwanza timu hiyo ikimenyana na wenyeji Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kutoka sare ya bila kufungana.
  Maana yake, Mganda huyo atakuwa tayari kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu wa Wekundu hao wa Msimbazi Jumatatu dhidi ya Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Abbel Dhaira akitoka nje kabla ya mapumzik jana Uwanja wa Mkwakwani, lakini amesema hajaumia sana maana yake atarejea kwenye mechi na Azam Jumatatu

  “Sijaumia sana, ni maumivu madogo ya kichwa baada ya kugongana na mchezaji wa Coastal. Ila kwa jinsi nilivyokuwa najisikia pale, ilikuwa hatari kwa timu yangu kuendelea kusimama langoni. Sikuwa najisikia vizuri, nilihitaji japo dakika 30 za kupumzika, isingewezekana,”alisema Dhaira.
  Kipa huyo aligongana na mshambuliaji wa Coastal Union, Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 33 na kutibiwa kwa dakika mbili kabla ya kutoka nje akimpisha kinda, Abuu Hashimu, aliyepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana ya klabu hiyo, Simba B.
  Simba One; Abbel Dhaira atarejea kazini Jumatatu Uwanja wa Taifa

  Abuu, aliyeiwezesha Simba B kutwaa Kombe la Banc ABC Sup8R mwaka jana, alilinda vyema lango la Wekundu wa Msimbazi na kumalizia dakika 55 na ushei bila kuruhusu nyavu za timu hiyo kutikiswa.
  Matokeo hayo yanaifanya Simba SC itimize pointi 20 baada ya kucheza mechi 10, sawa na Azam na Mbeya City, hivyo kurejea kileleni mwa ligi hiyo kutokana na wastani wao mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
  Simba SC ina mabao 12 baada ya kutoa mabao ya kufungwa, wakati Azam ina mabao tisa (GD) na Mbeya City mabao sita.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: DHAIRA HAJAUMIA SANA JANA MKWAKWANI, KUREJEA LANGONI SIMBA NA AZAM JUMATATU TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top