• HABARI MPYA

  Monday, October 21, 2013

  BRANDTS AWAITA WACHEZAJI YANGA SC MAKANJANJA

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  KOCHA Mkuu wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam, Mholanzi Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts,  amesema kwamba wachezaji wake ni makanjanja (unproffessionals) na ndiyo maana jana walikubali kutoka kuongoza kwa mabao 3-0 hadi kulazimishwa sare ya 3-3 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Akizungumza baada ya mchezo huo, beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi, aliyerithi mikoba ya Mbelgiji Tom Saintfiet Oktoba mwaka jana, alisema kwamba ni uzembe kutoka kuongoza kwa 3-0 hadi mapumziko na kutoa sare ya tatu.
  Wachezaji pasua kichwa; Kocha wa Yanga SC Ernie Brandts jana baada ya Simba SC kusawazisha mabao akikuna kichwa

  “Nafikiri sare tuliyopata tumejitakia wenyewe, wakati nimeona kipindi cha kwanza tumecheza vizuri sana, tumepata nafasi nyingi, tulikuwa tayari kiasi cha kutosha. Katika dakika 10 za mwisho tayari mchezo waliokuwa wanacheza wachezaji wangu ungeona ulikuwa wa kijinga, walifanya vitu vya kipumbavu, walikuwa wanacheza kwenye kiungo tu, wanakaa na mipira wanafanya mbinu fulani,”.
  “Kisha nikakasirika sana, tuliporudi vyumbani, wachezaji fulani wakawa wanapayuka, aaah tatu bila, tatu bila, ni ukanjanja sana, hivyo nikawaambia, kama hamtaelekeza akili zenu mchezoni, wanaweza wakafunga  bao moja, la pili na la tatu. Niliwaambia katika chumba cha kubadilishia nguo, waulize wachezaji wangu,”. 
  Ungekuwa ushindi mnono; Hamisi Kiiza akishangilia baada ya kufunga bao la tatu, Yanga ikaongoza 3-0

  Brandts alimaiza kila kitu jana, lakini hakuiepuka sare na Simba SC

  “Na ndicho kilichotokea kipindi cha pili, wamerudi uwanjani, wakapoteza mwelekeo na Simba SC wakarudisha mabao yote. Haya ni matunda ya kukosa umakini, lakini bado tulipata  nafasi nzuri kipindi cha pili, mwishowe nimesikitishwa sana, kwa sababu ni ukanjanja sana,” alisema.
  Brandts alisema kwamba hali iliyojitokeza jana Uwanja wa Taifa si mara ya kwanza katika timu yake, kwani mara kadhaa makosa kama hayo yamekuwa yakifanyika hata katika mechi zilizopta, ila jana waliruhusu mabao mengi ambayo ni mbaya kwa timu kama Yanga.
  Brandts alisema lawama ni za wachezaji wote, kwa sababu iliyokuwa inacheza ni timu na akasema angeweza kushinda hata mabao sita iwapo wachezaji wake wangecheza kwa umakini.
  “Huwezi kuzuia kwa asilimia 95, lazima ucheze kwa uangalifu na umakini, kama hutafanya hivyo huwezi kupata matokeo mazuri. Kama walivyocheza kwenye mechi (iliyopita) na Kagera Sugar (Bukoba, Yanga ilishinda 2-1). Wachezaji walicheza kwa uangalifu na umakini,”alisema.
  Brandts alisema katika mazoezi ya timu hiyo kila siku anafanyia kazi kila idara na wazi matokeo ya jana yalitokana na vijana wake kulewa sifa baada ya kuongoza mabao 3-0.
  Pamoja na matokeo hayo, Yanga ikiwa na pointi 16 ndani ya mechi 10 ilizocheza, inazidiwa pointi nne na Azam na Mbeya City zinazoongoza ligi na tatu na Simba SC walio nafasi ya pili, Brandts amesema bado ana matumaini ya kutetea ubingwa.
  “Bado nina matumaini ya kutetea ubingwa, kwa sababu ligi bado mbichi, haiishi wiki ijayo, tunakwenda kufanyia kazi mapungufu yetu baada ya mchezo huu (na Simba SC) na kisha tunaendelea na mapambano kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu,”alisema.
  Hadi mapumziko, tayari Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza mawili, lakini kipindi cha Simba SC ikasawazisha kupitia kwa Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BRANDTS AWAITA WACHEZAJI YANGA SC MAKANJANJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top