• HABARI MPYA

    Wednesday, October 23, 2013

    BRANDTS ALIZEMBEA KUZIBA UFA YANGA, NANI ALAUMIWE UKUTA KUDONDOKA?

    MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga Jumapili, ambayo iliisha kwa sare ya kufungana mabao 3-3 imezua mijadala mingi na mipana- kiasi cha hadi makocha kuingia kwenye mtego wa kishabiki kwa kutoa maelezo ambayo huwezi kuyaita ya kitaalamu. 
    Jumapili, Yanga iliongoza 3-0 ndani ya dakika 45, lakini ndani ya dakika 60, tayari matokeo yalikuwa 3-1.
    Kwanza, nataka niwakumbushe kilichotokea watani hao walipokutana Novemba 9, mwaka 1996 katika mchezo wa iliyokuwa Ligi ya Kuu ya Muungano, Simba SC iliongoza kwa mabao 3-1 hadi dakika ya 60, mwishowe Yanga ikapata sare ya 4-4. 

    Thomas Kipese ‘Uncle Thom’ alitangulia kuifungia Simba SC dakika ya saba, Edibilly Lunyamila akasawazisha kwa penalti dakika ya 28, Ahmed Mwinyimkuu akaifungia Simba SC la pili dakika ya 43 na Wekundu wa Msimbazi wakaenda kupumzika wanaongoza mabao 2-1 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
    Kipindi cha pili, Dua Saidi akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 60 na wengi wakaamini Yanga imekwisha na sana inaweza kupewa kipigo kama cha miaka miwili iliyotangulia, Julai 2, mwaka 1994 cha mabao 4-1, mabao ya Simba yakifungwa na George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani na Dua Saidi Yanga, wakati la Yanga lilifungwa na Constantine Kimanda.
    Hapana, haikuwa hivyo- Mustafa Hozza alijifunga dakika ya 64 katika harakati za kuokoa na Yanga ikazinduka na kupata mabao mawili zaidi, wafungaji Said Mwamba 'Kizota' marehemu dakika ya 70 na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ dakika ya 75. Hapo, watu wakaamini pia, Simba SC imekwisha, ikitoka kuongoza kwa 3-1 hadi kulala 4-3, lakini haikuwa hivyo, kwani Dua Saidi akaisawazishia Simba SC dakika ya mwisho kabisa.
    Kwa kurejea sare hii ya 1996, sare ya Jumapili huwezi kuiita haijawahi kutokea, huwezi kuiita ya ajabu- Oktoba 20, mwaka huu Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-1 ndani ya dakika 60 na Novemba 9, Simba walikuwa mbele kwa mabao 3-1 ndani ya dakika 60.  
    Bila shaka nimeweka sawa hilo, ili ‘wazee wa rekodi’ waweke rekodi zao sawa na kama walikwishawapotosha wasomaji wao, basi watafute namna ya kuwapa ukweli, kiungwana tu.

    Nini kiliwaponza Yanga kupokonywa tonge mdomoni?
    Kuelekea mchezo huo, wengi walikuwa wanaamini Yanga inaundwa na wachezaji wazoefu zaidi, waliokaa pamoja kwa muda mrefu na Simba SC ndiyo inaundwa undwa- hivyo wana Jangwani walipewa nafasi ya kushinda mechi.
    Yanga walicheza vizuri dakika 30 za kipindi cha kwanza na baada ya kuongoza kwa mabao 3-0, wakaanza kucheza mpira wa dharau, wakigongeana pasi zisizo na maana na mbwembwe nyingi- na kama Simba SC wangekuwa makini, wangeweza kuanza kupunguza mabao hata ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
    Mabadiliko yaliyofanywa na Simba SC kipindi cha pili, kuwaingiza chipukizi Said Ndemla na William Lucian ‘Gallas’ kuchukua nafasi za Abdulhalim Humud na Haroun Chanongo yalikuwa yenye tija sana.
    Kipindi cha kwanza Simba ilizidiwa katika kiungo kwa sababu ilikuwa ina watu wawili tu pale katikati, Jonas Mkude na Humud, wakati Yanga walikuwa wana watu watatu, Frank Domayo, Athumani Iddi ‘Chuji’ na Haruna Niyonzima. Chanongo alikuwa anacheza pembeni zaidi sawa na Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Lakini Simba SC ilipoongeza watu katikati kwa kupunguza winga mmoja, mpira ukawa rahisi upande wao na taratibu mambo yakaanza kubadilika, kwa sababu Wekundu wa Msimbazi walikuwa wana watu pale katikati ambao wana nguvu mpya, huku viungo wa Yanga wakionekana kupungukiwa nguvu na kasi baada ya kucheza sana kipindi cha kwanza.
    Lakini pia, kwa kawaida Yanga ni timu ambayo imekuwa ikimudu kucheza kwa kasi nzuri dakika 45 za kwanza tu katika mechi zake zote za msimu huu na kipindi cha pili huwa wanaomba mpira uishe, hii ni kuanzia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam Agosti 17, mwaka huu wakishinda 1-0, bao pekee la Salum Telela.
    Katika mechi ya Ligi Kuu na Azam pia, Yanga iliongoza 2-1, ikalala 3-2. Mechi nyingine zote jamani, tumeona, Yanga inakufa kabisa kipindi cha pili, hata ile waliyoshidna 2-1 na Kagera Sugar Bukoba, ambao ulikuwa mchezo wa mwisho kabla ya kucheza na Simba, ingawa mikoani huwa wanasingizia viwanja vobovu.  
    Haikuwa ajabu baada ya Simba SC kutawala sehemu ya kiungo ikafanikiwa kupata mabao matatu kipindi cha pili- na ingeweza kupata zaidi kama si mchecheto wao wenyewe tu.
    Hata mabeki wa Simba SC, baada ya kuisoma Yanga kwamba ‘imekufa’ wakaanza kupata ujasiri wa kupanda kusaidia mashambulizi na ndiyo maana mabao mawili yalifungwa na walinzi wa kati wa timu hiyo, Kaze Gilbert na Joseph Owino.  Yanga wakapoteana kabisa, wakabaki na staili moja tu ya kushambulia, Chuji awapigie mipira mirefu Simon Msuva na Mrisho Ngassa wakimbize, ambao hata hivyo walidhibitiwa kipindi cha pili. 
    Mabao yote sita Jumapili yalitokana na umakini mbovu wa wachezaji wa timu zote mbili, angalau kidogo bao la tatu la Yanga unaweza kumpa sifa Didier Kavumbangu aliyewapangua mabeki kabla ya kumpa pasi Kiiza akiwa kwenye nafasi nzuri, akafunga. Naam, hilo ndilo bao ambalo mtu yeyote anweza kupenda kuruida kulitazama kutoka mabao yote ya mchezo huo.
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Yanga SC, Ernie Brandts alikasirika mno na kuwaita wachezaji wake wazembe na ndiyo maana walikubali kutoka kuongoza kwa mabao 3-0 hadi kulazimishwa sare ya 3-3.
    Lakini mimi naweza kusema, kama ni uzembe unaanzia kwake mwenyewe kocha, kwa kushindwa kuchukua hatua za kulinda mabao, baada ya kuona mapungufu ya timu yake tangu dakika za mwishoni kipindi cha kwanza. 
    “Nafikiri sare tuliyopata tumejitakia wenyewe, wakati nimeona kipindi cha kwanza tumecheza vizuri sana, tumepata nafasi nyingi, tulikuwa tayari kiasi cha kutosha. Katika dakika 10 za mwisho tayari mchezo waliokuwa wanacheza wachezaji wangu ungeona ulikuwa wa kijinga, walifanya vitu vya kipumbavu, walikuwa wanacheza kwenye kiungo tu, wanakaa na mipira wanafanya mbinu fulani,”.
    “Kisha nikakasirika sana, tuliporudi vyumbani, wachezaji fulani wakawa wanapayuka, aaah tatu bila, tatu bila, ni ukanjanja sana, hivyo nikawaambia, kama hamtaelekeza akili zenu mchezoni, wanaweza wakafunga bao moja, la pili na la tatu. Niliwaambia katika chumba cha kubadilishia nguo, waulize wachezaji wangu,”. 
    “Na ndicho kilichotokea kipindi cha pili, wamerudi uwanjani, wakapoteza mwelekeo na Simba SC wakarudisha mabao yote. Haya ni matunda ya kukosa umakini, lakini bado tulipata nafasi nzuri kipindi cha pili, mwishowe nimesikitishwa sana, kwa sababu ni ukanjanja sana,” alisema Brandts baada ya mechi.
    Maelezo haya ya Brandts yanaonyesha yeye ni kocha dhaifu hata kama ni bora katika kufundisha- kwa sababu matatizo aliyaona mapema, lakini hakuyapatia ufumbuzi hadi athari zikatokea na baadaye ndio anakuja kutoa lawama. 
    Brandts pia alisema kwamba hali iliyojitokeza Jumapili Uwanja wa Taifa si mara ya kwanza katika timu yake, kwani mara kadhaa makosa kama hayo yamekuwa yakifanyika hata katika mechi zilizopta, ila siku hiyo waliruhusu mabao mengi ambayo ni mbaya kwa timu kama Yanga. Kumbe matatizo haya yapo siku nyingi, basi Brandts kama alizemebea kuziba ufa, sasa ukuta umedondoka. Alaumiwe nani?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BRANDTS ALIZEMBEA KUZIBA UFA YANGA, NANI ALAUMIWE UKUTA KUDONDOKA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top