• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 28, 2013

  COASTAL UNION YAZINDUKA, YAIBANJUA MTIBWA 3-0 MKWAKWANI

  Na Prince Akbar, Tanga
  COASTAL Union ya Tanga imezinduka baada ya sare na vipigo vilivyofuatana, leo hii ikiifunga Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 3-0 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Coastal ambayo sasa iko chini ya makocha wa muda, wachezaji wake wa zamani, beki Joseph Lazaro na mshambuliaji Razack Yussuf ‘Careca’ ilipata mabao yake leo kupitia kwa viungo Wakenya Crispin Odula dakika ya 20, Jerry Santo 38 kwa penalti na mshambuliaji mzawa, Danny Lyanga dakika ya 88.
  Coastal Union imeng'ara leo Mkwakwani

  Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Ruvu Shooting imetoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar ya Bukoba, Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.   
  Kagera Sugar ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mpachika mabao wake mahiri, Themi Felix dakika ya 36 na Said Dilunga akaisawazishia Ruvu dakika ya 72.
  Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, wenyeji JKT Oljoro wamelazimishwa sare ya bila kufungana wa ‘Watoto wa Jiji’, Ashanti United ya Ilala, Dar es Salaam. 
  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Azam FC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC ikitoka nyuma kwa bao 1-0.
  Shujaa wa Azam leo alikuwa ni mshambuliaji kutoka Ivory Coast na mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Kipre Herman Tchetche aliyefunga mabao yote ya timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa.
  Kwa matokeo hayo, Azam inatimiza pointi 23 na kujinafasi kileleni, ikiwazidi kwa pointi tatu Simba SC na Mbeya City katika nafasi ya pili.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Oden Mbaga aliyesaidiwa na Hamisi Chang’walu na John Kanyenye wote Dar es Salaam, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1. 
  Simba SC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 21 kupitia kwa Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyemalizia mpira ulioingizwa kutoka pembeni na Zahor Pazi.
  Bao hilo liliwaongeza kasi Simba SC na kushambulia zaidi langoni mwa Azam FC, lakini hawakufanikiwa kupata bao la pili.
  Azam ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 44 kupitia kwa Kipre Tchetche aliyemalizia mpira wa Erasto Nyoni kutoka pembeni kulia.
  Kipindi cha pili, timu zote zilishambuliana kwa zamu kabla ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kumpa pasi nzuri Kipre Tchetche upande wa kushoto, akamfunga tela William Lucian ‘Gallas’ kisha kumchambua Abbel Dhaira kwa ustadi wa hali ya juu.
  Katika kipindi hicho, Simba SC ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 60 kupitia kwa Sino Augustino aliyebaki yeye na kipa na kupaisha juu ya lango kufuatia pasi nzuri ya Ramadhani Singano ‘Messi’. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: COASTAL UNION YAZINDUKA, YAIBANJUA MTIBWA 3-0 MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top