• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 27, 2013

  AZAM TV KURUSHA 'LIVE' CHALLENGE YOOTE KUTOKA KENYA MWEZI UJAO

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  MTENDAJI Mkuu wa Azam Media Group, Rhys Torrington amesema kwamba wanatarajia kununua haki za kuonyesha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge itakayofanyika mwezi ujao nchini Kenya.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana katika mahojiano maalum, Torrington raia wa Uingereza alisema kwamba wapo katika mazungumzo na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) juu ya mpango huo.
  Torrington kulia akimueleekza jambo, mmoja wa Wakurugenzi wa Azam Media, Yussuf Bakhresa alipotembelea ofisi kuu za kampuni hiyo, eneo la Tazara, barabara ya Nyerere, Dar es Salaam juzi.

  Kwa muda sasa, mashindano yote ya CECAFA yamekuwa yakionyeshwa na Televisheni ya SuperSport ya Afrika Kusini, lakini wamekuwa hawalipi chochote kwa madai eti wanapromoti soka ya ukanda huu, lakini Azam Media kupitia Azam TV wanataka kuweka fedha.
  Pamoja na mpango huo wa kuonyesha Challnge, Torrington alisema pia watakuwa wanaonyesha mashindano mengine makubwa ya kimataifa, ili kuwapa burudani zaidi watazamaji wake.      
  Huduma kamili za Azam TV zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao na kwa mujibu wa Rhys Torrington kila kitu knaendelea vizuri.
  “Tutafungua milango ya Azam TV rasmi katikati ya Novemba kwa huduma ya chaneli 35 ambazo watu wajionea bure na uzinduzi utafanyika Novemba hiyo hiyo,”alisema.
  Torrington alisema kwamba king’amuzi cha Azam TV kitauzwa kwa Sh. 95,000 pamoja na dishi lake na pia mteja kupatiwa huduma za kufungiwa na kuunganishiwa bure nyumbani kwake.
  Alisema malipo ya mwezi yatakuwa ni Sh. 12,500 tu na mteja atapata chaneli zaidi ya 50 katika king’amuzi cha Azam TV.
  Alisema Azam TV pekee kwa kuanzia itakuwa na chaneli tatu ambazo ni Azam One itakayohusu habari za Afrika na zaidi za Kiswahili, Azam Two ambayo itakuwa ya kimataifa yenye vipindi mbalimbali duniani, na baadhi vya Kiswahili na Sinema Zetu itakayokuwa ikionyesha sinema za Kitanzania kwa saa 24 kila siku.
  Torrington akionyesha rimoti na king'amuzi cha Azam TV

  Alisema Azam TV imedhamiria kutoa huduma bora kwa bei nafuu kwa kuzingatia hali halisi ya Mtanzania na amewataka wananchi kujitokeza kununua ving’amuzi vya Azam TV mwezi ujao, mara tu huduma hizo zitakapoanza rasmi.
  Kwa sasa, Azam TV iliyonunua haki za matangazo ya Televisheni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaonyesha michezo ya ligi hiyo kupitia Televisheni ya Taifa, TBC1.
  “Mkataba wa sasa kati yetu na TBC1 unaisha mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na kuanzia mzunguko wa pili, Watanzania watapata moja kwa moja huduma za Azam TV kupitia ving’amuzi vyao watakavyonunua kuanzia mwezi ujao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM TV KURUSHA 'LIVE' CHALLENGE YOOTE KUTOKA KENYA MWEZI UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top