• HABARI MPYA

    Monday, October 28, 2013

    YUSSUF BAKHRESA AMMWAGIA PONGEZI MALINZI NA TIMU YAKE NZIMA, AMUAMBIA WATANZANIA WANA KIU YA MAFANIKIO

    Na Mahmoud Zubeiry, Mikocheni
    WAKALA wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Alhaj Yussuf Said Salim Awadh Bakhresa amempongeza rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na timu yake mpya aliyoingia madarakani jana.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo asubuhi, Mikocheni, Dar es Salaam, Yussuf amesema kwamba amekuwa akimsikia Malinzi siku nyingi katika michezo tangu akiwa Yanga wakati huo yeye bado anasoma, hivyo anaamini ni kiongozi mzoefu na ataleta maendeleo katika soka ya Tanzania.
    Alhaj Yussuf Bakhresa amempongeza Malinzi na kumtakia mafanikio katika uongozi wake TFF 

    “Nachukua fursa hii mimi binafsi kama mdau wa soka na wakala wa FIFA, mwanachama wa TFF kumpongeza Malinzi na timu yake, nawatakia mafanikio mema katika utawala wao. Watanzania tuna kiu ya mafanikio na maendeleo ya mpira wetu kwa ujumla, naamini wataweza,”alisema.
    Pamoja na kuwa wakala wa FIFA, Yussuf aliyewahi kuwapeleka wachezaji Mrisho Ngassa West Ham United ya England na John Bocco Israel kwa majaribio, pia ni Mjumbe wa bodi ya Ukurugenzi ya klabu ya Azam FC.
    Malinzi ameshinda Urais wa TFF baada ya kupata kura 72, dhidi ya 52 za mpinzani wake Athumani Jumanne Nyamlani.
    Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam, Walace Karia alifanikiwa kushinda nafasi ya Makamu wa Rais kwa kupata kura 67 akiwashinda Nassib Ramadhani kura 52 na Imani Madega sita.   
    Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera) aliyepata kura 102 za ndiyo na 17 za hapana. Kanda namba 2- Mara na Mwanza, mshindi ni Vedastus Lufano aliyepata kura 51 dhidi ya Jumbe Odessa Magati (11), Mugisha Galibona (24), na Samwel Nyalla (39).
    Epaphra Swai ndiye mshindi wa Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu kwa kura 63 dhidi ya Mbasha Matutu aliyepata 61. Kanda namba 4- Arusha na Manyara mshindi ni  Omali Walii Ali aliyepata kura 53 dhidi Elley Mbise (51), Ally Mtumwa (19).
    Kanda namba 4- Kigoma na Tabora, mshindi ni Ahmed Idd Mgoyi aliyepata kura 92 dhidi ya 28 za Hamisi Yusuf Kitumbo.
    Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo ameshinda Kanda namba 6- Katavi na Rukwa kwa kura 73 dhidi ya Ayubu Nyaulingo aliyepata 52. Ayoub Shaibu Nyenzi ndiye mshindi wa Kanda namba 7- Iringa na Mbeya kwa kupata kura 59 na kuwapiku David Samson Lugenge (8), John Exavery Kiteve (12) na Lusekelo Elias Mwanjala (46).
    Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma inawakilishwa na James Patrick Mhagama aliyepata kura 93 dhidi ya 31 za Kapteni mstaafu Stanley William Lugenge. Athuman Kingombe Kambi ndiye mshindi wa Kanda namba 9- Lindi na Mtwara kwa kura 84 akiwazidi Francis Kumba Ndulane (30) na Zafarani Mzee Damoder (11).
    Hussein Zuberi Mwamba ametetea ujumbe wa Kanda namba 10- Dodoma na Singida kwa kura 63 akiwapiku Stewart Masima (58) na Charles Komba (4). Geofrey Irick Nyange ameshinda Kanda namba 11- Morogoro na Pwani akipata kura 78 dhidi ya Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na Twahil Twaha Njoki (2).
    Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani, Khalid Abdallah Mohamed ndiye aliyeibuka kidedea kwa kura 69 dhidi ya 54 za mpinzani wake Davis Elisa Mosha.  Kidao Wilfred Mzigama ameshinda Kanda namba 13- Dar es Salaam kwa kupata kura 60 dhidi ya wapinzani wake Muhsin Said Balhabou (50), Omar Isack Abdulkadir (10) na Alex Crispine Kamuzelya (4).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YUSSUF BAKHRESA AMMWAGIA PONGEZI MALINZI NA TIMU YAKE NZIMA, AMUAMBIA WATANZANIA WANA KIU YA MAFANIKIO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top