• HABARI MPYA

  Thursday, October 24, 2013

  ACHANA NA SAID NDEMLA, DOGO NI HABARI NYINGINE KATIKA ‘DIMBA KUBWA’

  Na Mahmoud Zubeiry, Tanga
  SIMBA SC ilitoka nyuma kwa mabao 3-0 na kupata sare ya 3-3 Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya watani wa jadi, Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Baada ya mchezo huo, wataalamu wengi walisema mabadiliko yaliyofanywa na Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ mapema kipindi cha pili kuwaingiza William Lucian ‘Gallas’ na Said Hamisi Ndemla kuchukua nafasi za Haroun Chanongo na Abdulhalim Humud ndiyo yaliyoizindua Simba SC.
  Said Hamisi Ndemla, kiungo hodari anayechipukia Simba SC

  Naam, ni kweli kabisa. Lucian ambaye hucheza nafasi ya kiungo mkabaji na Ndemla ambaye huchezesha timu pale katikati, kwa sasa ni wachezaji muhimu mno ndani ya kikosi cha Simba SC na hazina ya taifa pia.
  BIN ZUBEIRY leo inamzungumzia Ndemla, kiungo chipukizi aliyepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana ya klabu hiyo, Simba B- kijana kwa sasa anawabeba sana Wekundu wa Msimbazi.
  Said Ndemla anakaba
  Anapasua kwenye misitu kama hivi


  Anaambaa na mipira

  Ni fundi namna hii

  Ndemla jana kwa mara nyingine aliendelea kudhihirisha ubora wake wakati Simba SC ikitoka sare ya 0-0 na Coastal Union ya Tanga, Uwanja wa Mkwakwani kwa kucheza soka maridadi yenye kumaanisha yeye ni kiungo hodari.
  Anakaba, anapitia mipira, anatoa pasi nzuri, anazuia mipira, anatembea na mpira, anapiga vyenga, ni fundi na mwili wake wote unaouna mpira, kiasi kwamba anaweza kuuchezea hata kama macho hayautazami.
  Anatoa pasi za kinyumenyume kama Ronaldinho wa Brazil enzi zake Barcelona


  Pasi inaelekea kwa mlengwa Jonas Mkude

  Mkude anapiga  mpira mrefu

  Hajawahi kuitwa timu ya taifa, lakini bila shaka kama ataendelea kucheza vyema katika mechi ya Jumatatu dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tarajia kocha Mdenmark, Kim Poulsen atamuita katika kikosi cha Bara kitakachokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwezi ujao. 
  Safu ya kiungo ya Coastal jana iliundwa na viungo wazoefu wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo na Crispin Odula, lakini ni sahihi kusema wote walifunikwa na Ndemla Uwanja wa Mkwakwani na picha zinazoambatana na makala hii zinathibitisha.
  Hapotezi mpira hata akidondoshwa chini


  Ramadhani Singano 'Messi' kulia hana wasiwasi anajua Ndemla atainuka na mpira

  Na kweli, huyo anainuka nao

  Anaambaa nao huku akiangalia aupeleke wapi kwa nani

  Huu ni mwanzo mzuri wa kiungo huyu, lakini anahitaji uendelezwaji ili atimize ndoto zake na hilo ni jukumu la viongozi wa Simba SC, vinginevyo muda si mrefu ataingizwa kwenye kundi la akina Haroun Chanongo, kurudishwa Simba B akaboreshe kiwango.
  Chanongo naye alikuwa moto msimu uliopita alipopandishwa kutoka timu B, lakini wiki hii amerudishwa kikosi cha pili akaboreshe kiwango. 
  Vijana kadhaa waliibuka vizuri kutoka Simba B siku za karibuni akiwemo Christopher Edward na Abdallah Seseme, lakini cheche zao zimepotea.
  Hayo ni mambo ambayo viongozi wa Simba SC wanatakiwa wayafanyie kazi- lazima kuna sehemu wanakosea katika malezi ya vijana hao. Yote kwa yote, Said Hamisi Ndemola ni habari nyingine. 
  Jerry Santo akimpiga teke la kinena Said Ndemla, lakini hata hakuugulia maumivu


  Crispin Odula anafunga tela kwa Ndemla

  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alishuhudia vitu vya Ndemla kwa mara nyingine, je wanamuendelezaje huyu kijana? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ACHANA NA SAID NDEMLA, DOGO NI HABARI NYINGINE KATIKA ‘DIMBA KUBWA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top