• HABARI MPYA

  Wednesday, November 14, 2018

  SAMATTA ASHINDWA KUJIUNGA NA TAIFA STARS AFRIKA KUSINI KWA SABABU YA MATATIZO YA KIFAMILIA, AREJEA DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta hatajiunga na kambi ya Taifa Stars mapema mjini Bloemfontein, Afrika Kusini kutokana na matatizo ya kifamilia.
  Hayo yamesemwa na Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi alipozungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu leo kutoka Bloemfontein ambako timu hiyo imeweka kambi kwa wiki moja sasa kujiandaa na mechi ya Jumapili dhidi ya wenyeji, Lesotho.
  Msangi amesema kwamba Samatta amekuja moja kwa moja nyumbani Dar es Salaam kutoka Ubeligiji, anakochezea KRC Genk kwa sababu mwanawe ni mgonjwa na hawajajua atajiunga lini na timu. 
  Inafahamika Samatta hatacheza Jumapili dhidi ya wenyeji Lesotho mjini Maseru mechi ya Kundi L kufuzu AFCON 2019 Cameroon kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano. 
  Mbwana Samatta hajajiunga na kambi ya Taifa Stars mjini Bloemfontein, Afrika Kusini kutokana na matatizo ya kifamilia 

  Wachezaji wote wengine wanaocheza nje, mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania na Thomas Ulimwengu aliyevunja mkataba na El Hilal ya Sudan wapo kambini.
  Mandawa pekee hakufanya mazoezi leo kutokana na maumivu ya nyonga na yupo chini ya uangalizi wa madaktari na Stars itaondoka Bloemfontein Ijumaa kwa basi, mwendo wa saa tatu kwenda Maseru tayari kwa mchezo wa Jumapili.
  Wachezaji wengine waliopo kambini ni makipa Aishi Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani.     
  Mabeki ni Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba SC, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zoyte za nyumbani.
  Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba SC zote za nyumbani na washambuliaji ni John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
  Kikosi hicho chini ya makocha Emmanuel Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18.
  Taifa Stars inahitaji ushindi dhidi ya Lesotho Jumapili ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu AFCON ya pili tu kihistoria kwao tangu ile ya mwaka 1980 nchini Nigeria.
  Kwa sasa, Stars inashika nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake tano baada ya kucheza mechi nne, ikishinda moja, sare moja na kufungwa moja, ikiizidi kwa pointi moja Cape Verde. 
  Uganda ambayo ni kama imekwishafuzu, inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi tano pia, wakati Lesotho yenye pointi mbili ni ya mwisho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA ASHINDWA KUJIUNGA NA TAIFA STARS AFRIKA KUSINI KWA SABABU YA MATATIZO YA KIFAMILIA, AREJEA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top