• HABARI MPYA

  Sunday, August 06, 2023

  GRACE MWAKAMELE AWEKA REKODI MASHINDANO YA NDONDI AFRIKA

  BONDIA wa Grace Joseph Mwakamele ameweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza wa Tanzania kutwaa Medali katika Mashindano ya Ndondi Afrika Jijini Yaoundé nchini Cameroon jana.
  Grace alipoteza pambano lake la fainali Ubingwa wa Afrika 2023 uzito wa Light Middle mbele ya Bingwa mtetezi na Mshindi wa pili Ubingwa wa Dunia Istanbul 2022, Alicida Panguane wa Msumbiji, hivyo kuambulia Medali ya Fedha.
  Kwa ushindi huo, Grace ambaye ni Mtanzania pekee kwa wanaume na wanawake kufika Fainali kwenye mashindano ya mwaka huu, amezawadiwa Fedha taslimu dola za Kimarekani 10,000.
  Timu ya Tanzania iliyowakilishwa na mabondia watatu, imefanikiwa kuliheshimisha Taifa kwa ushindi wa medali mbili, mbali na Fedha ya Grace, naye Yusuf Changalawe ameshinda Medali ya Shaba upande wa Wanaume.
  Kabla ya hapo, bondia wa mwisho kutwaa Medali kwenye mashindano hayo alikuwa ni Mbwana Matumla aliyeshinda Fedha baada ya kupigwa kwenye Fainali na Richard Sunee wa Mauritius nchini Afrika ya Kusini mwaka 1994.


  Grace Mwakamele (kushoto) na Mwalimu wa Timu ya Taifa ya Ngumi Samwel Kapungu "Batman" wakifurahia ushindi wa kuingia fainali baada ya kumchakaza Seynabou Ndiaye kutoka Senegal hatua ya nusu fainali._


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GRACE MWAKAMELE AWEKA REKODI MASHINDANO YA NDONDI AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top