• HABARI MPYA

  Saturday, August 19, 2023

  KOCHA WA ZAMANI WA YANGA SC, SAM TIMBE AFARIKI DUNIA


  ALIYEWAHI kuwa kocha wa Yanga, Mganda San Timbe (69) amefariki dunia leo katika Hospitali ya Nakasero Jijini Kampala, alipokuwa amelazwa wadi ya wagonjwa taabani (ICU).
  Sam Timbe amefariki akiwa kocha wa klabu ya URA FC ambayo imethibitisha msiba huo unaokuja siku moja kabla ya timu hiyo kumenyana na KCCA katika Nusu Fainali ya michuano ya Nane Bora ya Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) Super Eight Uwanja wa Lugogo.
  Na jana Timbe aliiongoza URA mazoezini kabla ya hali yake kubadilika ghafla baadaye na kukimbizwa hospitali ya Nakasero ambako aliwekwa ICU kwa matibabu makini, lakini jitihada za madaktari hazikuweza kunusuru maisha yake.
  Timbe alikuwa kocha wa Yanga msimu wa 2010 - 2011 akiipa timu hiyo mataji ya ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Kagame kabla ya kufukuzwa na nafasi yake kuchukua Mserbia, Kostadin Papic.
  Timbe aliyezaliwa Januari 1, mwaka 1954 kwa baba Stanley Wabuteya na Dorothy Wabuteya, alipata elimu yake katika shule ya Msingi Bupoto, kabla ya kwenda sekondari ya Nabumali na baadaye Chuo cha Tororo.
  Katika soka alianza kama kipa wa klabu ya Coffee FC ya kwao na alipostaafu akafundisha klabu mbalimbali na kwa mafanikio zikiwemo Coffee, Polisi, Lyantonde, Mbale Heroes, Simba FC, SC Villa zote za Uganda, Atraco ya Rwanda, Yanga ya Tanzania, Sofapaka na Tusker za Kenya, Sarawak ya Malaysia na URA.
  Amefundisha pia timu za taifa za Uganda kuanzia za Vijana, The Cobs hadi ya wakubwa, The Cranes kama Kocha Msaidizi na Kocha Mkuu.
  Mungu ampumzishe kwa amani Sam Timbe. Amin.

  Kutoka kulia Sam Timbe (RIP), Bin Zubeiry na Milutin Sredojevic ‘Micho’
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA WA ZAMANI WA YANGA SC, SAM TIMBE AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top