• HABARI MPYA

  Saturday, August 12, 2023

  GAMONDI NA ROBERTINHO WAZUNGUMZIA MCHEZO WA KESHO MKWAKWANI


  KOCHA wa Yanga, Muargentina Miguel Angel Gamondi amesema kwamba mchezo wa Fainali ya Ngao ya Jamii kesho dhidi ya Simba SC utakuwa mgumu kwa sababu zinakutana timu bora. 
  Watani hao wa jadi wanakutana kesho katika Fainali ya Ngao ya Jamii Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga kuanzia Saa 1:00 usiku, mechi  ambayo itatanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kati ya Azam FC na Singida Fountain Gate Saa 9:00 Alasiri.
  "Utakuwa mchezo mkubwa na mzuri kwetu hasa kwa mwanzo wa msimu na najua umuhimu wa mchezo huu kwa kila mmoja wetu," amesema Miguel Angel Gamondi na kuongeza.
  "Ni furaha kwangu kucheza mchezo huu mkubwa kesho, matarajio yetu ni kufanya vizuri na tumejiandaa bila presha yoyote, kwa sababu nimeshakutana na michezo ya aina hii mingi, tunaenda kupambana kwa ajili ya nembo ya Yanga na mashabiki wetu ambao wapo nasi kiła siku,".
  Kwa upande wake beki, Dickson Job amesema; "Kwa upande wetu wachezaji tuko tayari na mchezo wa kesho na tumejiandaa vizuri tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa nguvu uwanjani," amesema.
  Kwa upande wake, kocha wa Simba, Mbrazil Robert Oliveira 'Robertinho' amesema kwamba vijana wake wapo vizuri kwa ajili ya ushindi kesho.
  "Nimeiandaa timu yangu kucheza vizuri wakati hawana mpira, kucheza kwenye eneo la mpinzani, kushambulia kwa nguvu, kufunga magoli na kufurahia mchezo badala ya kucheza kwa stress, mwisho wa yote, ushindi ndilo lengo letu," amesema.


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GAMONDI NA ROBERTINHO WAZUNGUMZIA MCHEZO WA KESHO MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top