• HABARI MPYA

  Friday, August 11, 2023

  MO DEWJI: SIMBA INAHITAJI KIPA MWINGINE ZAIDI YA AISHI NA ALLY


  RAIS wa heshima wa Simba, Mohamed ‘Mo’ Dewji amesema kwamba japokuwa klabu ina makipa wawili wazuri, Aishi Salum na Ally Salum lakini inahitaji mlinda mlango mwingine hodari.
  “Ali ni mzuri na Aishi ni kipa namba moja Tanzania, pamoja na hayo ikiwa tunataka kushindana kwenye Ligi ya Mabingwa Simba inahitaji kipa mwingine hodari,” amesema Mo Dewji.
  Ally Salum amekuwa akiidakia Simba  tangu Aishi aumie kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Aprili 7, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Ally Salum aliiwezesha Simba kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na waliokuwa mabingwa watetezi, Wydad Club Athletic ya Morocco kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
  Kutokana na Aishi kitakiwa kuwa nje kwa muda mrefu, Simba ilisajili kipa Mbrazil Jefferson Luis Szerban de Oliveira Junior ambaye hata hivyo aliumia pia na kambini Uturuki wiki mbili zilizopita hivyo kusitisha mpango wa kumsajili.
  Kikosini ikiwa na makipa wawili, Ally Salum na Ally Ferouz ambao wote walipandishwa kutoka timu ya vijana, Simba ikasajili kipa mwingine, Hussein Abel wiki iliyopita kutoka KMC ya Dar es Salaam.
  Pamoja na Ally Salum kudaka vizuri jana na kupangua penalti moja Simba ikitinga Fainali ya Ngao ya Jamii kwa ushindi wa penalti 4-2 baada ya sare ya bila kufungana na Singida Fountain Gate Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga, bado Mo Dewji anaona wanahitaji kipa mwingine.
  Na tayari taarifa zinasema kipa Ayoub Lakred aliyewahi kudakia klabu za RS Berkane na FAR Rabat za kwao, Morocco amewasili nchini kukamilisha taratibu za kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MO DEWJI: SIMBA INAHITAJI KIPA MWINGINE ZAIDI YA AISHI NA ALLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top