• HABARI MPYA

  Friday, April 23, 2021

  RAIS MAMA SAMIAH SULUHU HASSAN AAHIDI KUSAIDIA MAANDALIZI YA TIMU ZA TAIFA ZIKAFANYE VYEMA KIMATAIFA

  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samiah Suluhu Hassan ameahidi kutenga bajeti ya kusaidia michezo kwa ujumla, ikiwemo timu zote za taifa soka za wanawake ili zifanye vizuri na kuepuka kuwa kichwa cha Mwendawazimu.
  "Sekta ya sanaa michezo na utamaduni inakuwa kwa kasi kubwa, vijana wetu wengi wamepata ajira kupitia sekta hii, hivyo basi kama ilivyoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi, kwenye miaka hii mitano tunakusudia kuikuza zaidi sekta hii, hususan kwa kuimarisha usimamizi wa masuala ya Hati Miliki, ili wasanii waweze kunufaika na kazi zao".
  "Tutahuisha mfuko wa utamaduni na sanaa ili kuwasaidia wasanii wetu, ikiwemo kupata mafunzo na mikopo," amesema Mama Samiah jana wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana Jijini Dodoma.
  Mama Samiah amesema Serikali yake itaanza kutenga fedha kwa ajili ya kuziandaa timu za taifa ili zifanye vyema kwenye mashindano ya kimataifa na kuepuka jina la Kichwa cha Mwendawazimu alilowahi kulitoa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi.
  "Aidha tutaanzisha kidogo kidogo kuanza kutenga fedha kwa ajili ya kuziandaa timu zetu za taifa, zikiwemo za wanawake. Tumechoka kuitwa lile jina alilolisema Mzee Mwinyi. Tunakwenda nje na ushabiki mkubwa, tukirudi Kichwa cha Mwendawazimu,"
  "Kwa hiyo tutajitahidi kuiangalia sekta hiyo angalau basi ipate msukumo na kupandisha ari za wachezaji ili Tanzania nasi tuingie kwenye ramani ya wacheza mpira wa miguu," alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS MAMA SAMIAH SULUHU HASSAN AAHIDI KUSAIDIA MAANDALIZI YA TIMU ZA TAIFA ZIKAFANYE VYEMA KIMATAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top