• HABARI MPYA

  Wednesday, November 04, 2020

  SIMBA SC YAWATUMIA SALAMU WATANI WA JADI, YAWATANDIKA MABAO 2-0 NA KAGERA SUGAR UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck inafikisha pointi 19 baada ya kucheza mechi tisa na kurejea nafasi ya tatu, sasa ikizidiwa ponti mbili na Azam FC na tatu na watani wao, Yanga SC wanaoongoza. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Raphael Ikambi wa Morogoro aliyesaidiwa na Sunday Komba wa Kilimanjaro na Hamdan Said wa Mtwara hadi mapumziko tayari Simba SC walikuwa wamekwishavuna mabao yao hayo mawili.


  Nahodha John Raphael Bocco alifunga la kwanza dakika ya 41 kwa penalti baada ya kiungo Hassan Dilunga kuangushwa na beki Erick Kyaruzi.
  Na kiungo aliyerejea kwenye ubora wake, Said Hamisi Ndemla akafunga bao la pili dakika ya 45 na ushei akimalizia kazi nzuri kiungo mwenzake, Mzambia Clatous Chota Chama.
  Baada ya mchezo huo, Simba SC wanarejea kambini kwa maandalizi ya mwisho mwisho kuelekea mechi dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Namungo FC imelazimishwa sare ya 2-2 na JKT Tanzania Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi na Mwadui FC imetoa sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Ibrahim Ame, Joash Onyango, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Said Ndemla, John Bocco/Chriss Mugalu dk65, Ibrahim Ajibu/Muzamil Yassin dk77 na Clatous Chama/Miraji Athumani dk77.
  Kagera Sugar; Benedicto Tinocco, Mwaita Gereza, David Luhende, Ally Mtoni ‘Sonso’, Erick Kyaruzi, Abdulswamad Kassim, Yussuph Mhilu, Abdallah Seseme/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk69, Mbaraka Yussuf/Nassoro Kapama dk51, Peter Mwalyanzi/Vitalis Mayanga dk51 na Ally Ramadhani ‘Kagawa’.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAWATUMIA SALAMU WATANI WA JADI, YAWATANDIKA MABAO 2-0 NA KAGERA SUGAR UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top