• HABARI MPYA

    Sunday, December 08, 2019

    MRITHI WA PATRICK AUSSEMS SIMBA SC KUTAMBULISHWA MAPEMA WIKI IJAYO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Mohammed ‘Mo’ Dewji amesema kwamba wiki ijayo wataleta kocha mpya mwenye kiwango kinachostahili kuwafundisha mabingwa hao Tanzania Bara. Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa klabu leo Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Dewji amesema kwamba mrithi wa Mbelgiji Patrick Aussems aliyefukuzwa wiki hii atakuwa kifaa’.
    Aidha, Dewji alisema kwamba baada ya jana kuonyesha viwanja vyao viwili vya mazoezi, wa nyasi bandia na halisi huko Bunju nje kidogo ya Jiji, huku mchakato wa kubadilisha muundo wa klabu ukiwa umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90, awamu ya pili ya ujenzi wa Bunju Complex, itakayohusisha hosteli yenye vyumba vya kulala, gym, ofisi za benchi la ufundi, jiko na kantini ya chakula na mambo mengine muhimu ya kitaalamu. 

    "Mradi huu unatarajiwa kuwa na thamani ya Tsh. Bilioni 2.5 na kwa kuanzia kama mwanachama na Mwenyekiti wa Bodi nitachangia kiasi cha Tsh. milioni 500. Wanasimba wanahamu yakuchangia ujenzi na upanuzi wa Bunju Complex. Kiasi kilichobaki tutafanya fundrising ili kupata fedha inayotakiwa, bila shaka tutafanikiwa ili kwenye msimu wa 2021/22 tuwe kwenye hostel zetu,”.  Amesema Mo Dewji. 
    Simba SC iliachana na Aussems baada ya beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Ubelgiji kushindwa kufikia malengo ya mwajiri wake na kwa sasa timu ipo chini ya Kocha Msaidizi, Dennis Kitambi hadi hapo atakapopatikana kocha mpya.
    Aussems alijiunga na Simba SC Julai 19 mwaka jana akitokea timu ya taifa ya Nepal, akichukua nafasi ya Mfaransa, Pierre Lechantre aliyeondoka Mei. 
    Katika kipindi miezi 16 ya klabu, Aussems ameiongoza Simba kucheza mechi 91, ikishinda 61, ikifungwa 13 na sare 17, ndani yake akiipa mataji mawili, ubingwa wa Ligi Kuu na Ngao ya Jamii pamoja na kufikisha Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.
    Hadi anaondolewa, Simba SC inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi zake 25 baada ya kucheza mechi 10, ikifuatiwa kwa mbali na Kagera Sugar yenye pointi 24 za mechi 13.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MRITHI WA PATRICK AUSSEMS SIMBA SC KUTAMBULISHWA MAPEMA WIKI IJAYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top