Na Khadija Khamis na Kijakazi Abdallah, ZANZIBAR
MUIGIZAJI na muaandaji maarufu wa filamu Tanzania Issa Mussa 'Cloud 112' anatarajiwa kuzindua filamu yake mpya yenye tamaduni za Kizanzibari katika ukumbi wa Ngome kongwe Desemba 8, 2017 ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Sanaa Raha Leo, Cloud 112 amesema filamu hiyo inayojulikana kwa jina la ‘USIJISAHAU’, imeigizwa katika misingi ya utamaduni halisi wa Kizanzibari.
Alisema filamu hiyo ambayo imeigizwa nchini Sweden na mkoani Tanga, imewashirikisha wasanii wa Kitanzania na imejaa vionjo na ladha ya kitanzania licha ya kuigizwa ulaya.
Aidha, amesema kuwa lengo kubwa la filamu hiyo kuingizwa Sweden ni kupanua wigo zaidi kwa wasanii wa kwetu na kuwapa fursa pana ya kupasua anga hasa katika nchi za ughaibuni.
Issa Mussa 'Cloud 112' (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi wa filamu yake mpya
Hata hivyo, alikiri kuwa waigizaji wengi wamezoea kutumia mazingira halisi ya nchi yao, lakini kuigiza katika mazingira mapya ambayo msanii hajayazoea kunamuimarisha zaidi katika kaziyake.
Alisema kuwa lengo kubwa la filamu hiyo kuzinduliwa Zanzibar ni kuwapa nguvu zaidi wasanii wa Kizanzibari katika tasnia ya filamu ya uigizaji kwa vile Zanzibar ni kitovu cha wasanii.
Hata hivyo, Cloud alisema kuwa filamuya USIJISAHAU ni ya mwanzo kuigizwa katika mazingira ya ughaibuni na itawahamasisha wasanii wengine wa Zanzibar kufanya maigizo yao nchi nyingine na kuondokana na mazingira ya kinyumbani.
Amewataka wasanii wa Zanzibar kuongeza ushirikiano ili kuona Sanaa ya maigizo inakuwa na inakubalika zaidi katika mataifa mbalimbali duniani.
Naye Katibu wa Chama cha Wasanii Waigizaji Zanzibar, Salum Stika amewaomba wananchi wa Zanzibar kumuunga mkono muigizaji huyo kwa hatua aliyochukua ya kufanya uzinduzi rasmi nyumbani kwa kushiriki kwa wingi kwenye uzinduzi huo.
Alisema muigizaji huyo ameuonyesha mfano na kuwapa hamasa wasanii wa Kitanzania kuweza kujitangaza kupitia fani ya Sanaa ya uigizaji ndani na nje ya nchi.
Alifahamisha kuwa Sanaa ili kuwepo tangu zamani na filamu za Kizanzibari ziliwahi kupatau maarufu mkubwa ikiwemo Ukombozi wa Mwafrika jambo ambalo linahitaji wasanii kuzidisha juhudi kuziendeleza.
0 comments:
Post a Comment