• HABARI MPYA

    Thursday, April 16, 2015

    YANGA HATARINI KUMKOSA TAMBWE MECHI NA ETOILE JUMAMOSI, MALARIA YAMLAZA MRUNDI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC iko hatarini kumkosa mshambuliaji wake tegemo, Amisi Tambwe (pichani kulia) katika mchezo wa kwanza Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Tambwe hakufanya mazoezi na wenzake leo, kutokana na kuugua ghafla ugonjwa wa Malaria na Daktari wa klabu hiyo, Sufiani Juma amesema Mrundi huyo ameanza kutumia dozi ya Malaria.
    “Bado haijajulikana kama tutamkosa, au tutakuwa  naye Tambwe Jumamosi, itategemea na maendeleo ya hali yake,”amesema Sufiani.
    Yanga imefika katika hatua ya 16 bora Kombe la Shirikisho baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao (3-2), kisha kuwaondoa FC Platinum ya Zimbabwe katika hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao (5-2).
    Ikifanikiwa kuwaondoa Etoile du Sahel, Yanga SC itacheza na moja ya timu nane zitakazotolewa 16 bora ya Ligi ya Mabingwa kuwania kupangwa kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho.
    Wapinzani wao, Etoile du Sahel wanatarajiwa kuwasili Saa 9:30 usiku kwa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair   bj 4870 wakiwa na msafara wa watu 56.  
    Maakocha wa Yanga, Hans van der Pluijm na Charles Boniface Mkwasa. Kulia ni beki na kiungo Mbuyu Twite katika mazoezi ya leo Uwanja wa Taifa
    Kpah Sherman kulia akiwania mpira dhidi ya Nadir Haroub 'Cannavaro'
    Beki Edward Charles kulia na kiungo Sadi Juma 'Makapu'
    Mrisho Ngassa akimiliki mpira mbele ya Haruna Niyonzima na Jerry Tegete

    Wakati Tambwe, akikosekana, wachezaji wengine waliokuwa majeruhi, kiungo Salum Telela na mshambuliaji Kpah Sherman wameendelea vizuri na mazoezi leo.
    Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amesema kwamba anaridhishwa na maendeleo ya wachezaji hao na anaweza akawaanzisha Jumamosi.
    “Kulikuwa kuna wasiwasi juu ya Telela na Sherman, lakini niseme nafurahishwa na maendeleo yao na bila shaka tutakuwa nao Jumamosi,”amesema.
    Yanga SC imeendelea na mazoezi yake leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo huo wa kwanza hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika na zaidi walimu wa timu hiyo Pluijm na Msaidizi wake, Mkwasa walionekana kufanyia kazi mbinu za kujilinda na kufunga.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA HATARINI KUMKOSA TAMBWE MECHI NA ETOILE JUMAMOSI, MALARIA YAMLAZA MRUNDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top