• HABARI MPYA

    Monday, April 20, 2015

    AKON AMWAGIA SIFA MTANZANIA MSHINDI WA AIRTEL TRACE MUSIC STARS NA KUSEMA; “MAYUNGA ANANIKUMBUSHA ENZI ZANGU”

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MWANAMUZIKI nguli, Aliaune Damala Bouga Time Bongo Puru Nacka Lu Lu Lu Badara Akon Thiam (pichani kulia), maarufu zaidi kwa jina la Akon, amesema uimbaji wa Mtanzania Nalimi Mayunga unamkumbusha enzi zake anatamba kwenye miondoko ya R&B.
    Akimtangaza Mtanzania huyo kuwa mshindi wa shindano la Airtel Trace Music Stars Africa, Mmarekani huyo mwenye asili ya Senegal, alisema; “Nimefurahishwa sana na Mwanamuziki huyu chipukizi kutoka Tanzania, kwani ana sauti nzuri iliyotulia na uwezo mkubwa wa kuimba,”. “Mayunga ananikumbusha enzi zangu, na ninaamini akiendelea hivi na kupata mfunzo zaidi atafika mbali kimuziki. Naahidi kumpa mafunzo yatakayomsaidia kupata mbinu mbalimbali za kimuziki na kurekodi naye wimbo mmoja, lakini akifanya vizuri nitampa zawadi ya kurekodi albamu pamoja nami,”amesema Akon.
    Malimi ameshinda Airtel Trace Music Stars Africa mbele ya washiriki wengine kutoka nchi 13 barani Afrika katika fainali ukumbi wa mjini Naivaisha, Kenya jana.
    Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Airtel, Sunil Colaso akizungumza katika halfa ya kumtangaza mshindi iliyofanyika ukumbi wa High Spirit, jengo la IT, Dar es Saalam, alisema; “Nampongeza sana Nalimi Mayunga kwa ushindi huu na tunaamini nafasi hii ya kupata mafunzo na kurekodi na Akon utakuwa mwanzo wa safari yake ndefu ya mafanikio na kuzifika ndoto zake”.
    Akaongeza; “Airtel tunajisikia furaha kuwa sehemu ya mafaniko ya vijana wengi kuzifikia ndoto zao kupitia programu zetu mbalimbali ikiwemo hii ya Airtel Trace Music Stars. Tunaahidi kuendelea kuwapatia fursa Watanzania kupitia programu zetu mbalimbali za kijamii huku tukiendelea kutoa huduma bora na za kibunifu na kuwafikishia watanzania mawasiliano bora nchini,”alisema Colaso.
    Shindano la Airtel Trace Music Star lilizinduliwa Oktoba mwaka jana, lengo likiwa ni kusaka, kukuza vipaji vya muziki na kuwawezesha wanamuziki chipukizi wa Kitanzania na Afrika kujulikana katika anga za muziki duniani. 
    “Leo tunayofuraha kutimiza dhamira yetu
    kwa vitendo kwa kuwaweezesha Watanzania kupata nafasi ya kushiriki na hatimaye moja kati yao kushinda,”alisema Colaso. K
    Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) Godfrey Mungereza alimpongeza Mayunga kwa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania na kurudi na ushindi.
    “Nimefuatilia mshindano haya, yalikuwa yana ushindani mkubwa sana, hii inaonyesha ni jinsi gani Tanzania tulivyo na vijana wenye vipaji, lakini hawajapata nafasi ya kuvionyesha, nawapongeza sana Airtel kwa kuja na mashindano haya yanayowawezesha vijana wa Kitanzania kupata fursa ya kuonyesha uwezo wao na kufanikiwa zaidi,”alisema Mungereza.

    Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mungereza (kushoto), akimkabidhi tuzo mwimbaji Mayunga Nalimi baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa Airtel Trace Music Stars Afrika, katika tafrija iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Anayeshuhudia (kulia), ni Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Sunil Colaso.

    Mayunga mwenyewe akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, alisema; “Najisikia furaha sana, kwa kweli namshukuru Mungu sana, kwani ushindani ulikuwa mkali sana, lakini nashukuru nilikabiliana nao kwa kufuata maelekezo ya walimu ya kupumzisha sauti na kufuata mbinu za kimuziki wakati wa kuimba na kuwa na ujasiri,”. “Nimefurahi sana kwa vile nafasi hii niliyoipata kupitia ushindi huu ni kubwa na ya kipekee. Nawashukuru sana Airtel kwa kuanzisha mashindano haya na ninawaahidi Watanzania
    kufanya vizuri zaidi na kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya nchi yetu sehemu mbalimbali nitakazokwenda katika shughuli zangu za kimuziki.”alisema Mayunga.
    Mashindano hayo yalishirikisha washiriki kutoka nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Madagascar, Malawi, Nigeria, Ghana, Burkina Faso, Chad,  Kongo Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Gabon na Tanzania huku yakisimamiwa na majaji mahiri akiwemo Akon, Devyne Stephens na Lynnsha.
    Washiriki hao 13 walichujwa na kupatikana 6 bora ambao ni wawakilishi toka Uganda, Madagscar, Malawi, Tanzania, Nigeria na Congo Brazaville, washiriki hao waliimba bila ala ili kuonyesha uwezo wa sauti zao,  ambapo Tanzania, Nigeria na Kongo Brazaville walifuzu kuingia tatu bora.
    Mwakilishi kutoka Tanzania aliibuka mshindi akifuatiwa na mshiriki kutoka Nigeria na mshindi wa watatu ni mwakilishi wa Kongo Brazaville. Mbali na kukabidhiwa Sh. Milioni 50 baada ya kuibuka mshindi hapa Tanzania, Mayunga amepata dili la kurekodi na kupata mafunzo nchini Marekani, yenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani 500,000.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AKON AMWAGIA SIFA MTANZANIA MSHINDI WA AIRTEL TRACE MUSIC STARS NA KUSEMA; “MAYUNGA ANANIKUMBUSHA ENZI ZANGU” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top