• HABARI MPYA

    Monday, April 14, 2014

    VODACOM WAIPONGEZA AZAM FC KWA UBINGWA BARA

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Bara, Vodacom imeipongeza timu ya Azam FC kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2013/2014.
    Aidha, Vodacom imeipongeza Yanga kwa kushika nafasi ya pili pamoja na kuonyesha upinzani mkali kwa Azam katika mbio za kuusaka ubingwa ambao walikuwa akiutetea.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari jana, mara baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Mbeya City na Azam FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Meneja Uhusiano wa Nje wa Kampumi ya Vodacom, Salum Mwalim amesema kwamba wakiwa wadhamini wameridhishwa na kiwango cha Azam FC na hivyo wanawapongeza kwa dhati.
    Hongereni sana; Salum Mwalim kushoto amewapongeza Azam FC

    “Tunachukua nafasi hii kuwapongeza Azam kwa kuwa mabingwa wapya wa Vodacom Premier League 2013/2014, wamekabiliana vyema na mikikimikiki ya ligi na hivyo ubingwa wao haukuwa mwepesi kuupata kutokana na ushindani uliokuwepo kwa timu zote shiriki,” alisema Mwalim.
    “Tumeifuatilia ligi na tuna imani kuwa, imetoa bingwa aliyestahili na ambaye yupo imara kutokana na kupitia safari ndefu na ngumu ya ligi, na ni imani yetu kwamba atakuwa mwakilishi mzuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiitangaza nchi na pia Vodacom Premier League,” alisema.
    Mwalim amesema Azam inabeba kwa mara ya kwanza ubingwa wa ligi tangu timu hiyo ilipoanza kushiriki Ligi Kuu mwaka 2008 na kwamba ushindi huo bila shaka utaongeza ushindani msimu ujao.
    “Ubingwa wao huenda ukaifanya ligi ya mwakani kuwa ngumu zaidi, kwani timu za Yanga na Simba ambazo zimekuwa zikipokezana ubingwa kwa takribani miaka 20 zitataka kurudisha heshima yao na nyengine zikipata nguvu kuwa yeyote anaweza kuwa bingwa, iwapo atajipanga vyema kumudu ushindani, hilo likitokea ubora wa ligi yetu utazidi kupaa,”alisema Mwalim.
    Mtangazaji huyo wa zamani wa Televisheni ya Channel Ten na mchambuzi wa soka, amesema Azam watakabidhiwa Kombe lao la ubingwa April 19 kwenye Uwanja wa nyumbani kwao, Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam wakati wa mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu.
    Akiizungumzia ligi, Mwalim amesema ilikuwa ya ushindani mkubwa na takribani kila mechi ilikuwa ngumu kwa kila timu, hali iliyolazimisha hata bingwa kujulikana kwenye mechi za mwishoni.
    “Tumefika mahala tunapoweza kuzungumza mazuri zaidi kuhusu ligi yetu, tofauti na tulikotoka, ni wazi kwamba ligi yetu imepiga hatua na Vodacom kama mdhamini Mkuu, tutaendelea kufanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuimarisha ubora huo,“ alisema Mwalim.
    Aidha Mwalim amezipongeza timu zote 14 zilizoshiriki ligi hiyo kwa kujituma na kutoa changamoto katika kila mechi, jambo lililofanya bingwa kutopatikana kwa urahisi na mapema.
    Aidha amezipongeza Mbeya City kuwa ni timu iliyoleta changamoto mpya kwenye ligi hiyona kuipa afya zaidi na anaamini itakuwa mfano tosha kwa timu nyingine msimu ujao.
    “Mbeya City wamecheza vizuri sana tangu mwanzoni mwa ligi, hadi wanapoelekea kumaliza mchezo wao wa mwisho, wameonyesha mfano kwa timu zinazopanda daraja namna gani wanavyoweza kuwa timu shindani badala ya kuwa timu shiriki,” aliongeza Mwalim.
    Amesema awali Mbeya City ilionekana kama imeingia na nguvu ya soda, lakini kadiri ligi ilivyokuwa ikosonga mbele, ilionyesha kuwa imedhamiria kufanya vyema huku ikihimili mikikimiki yote ya ligi na hivyo kuifanya kuwa timu inayohitaji kupewa sifa za kipekee kwa msimu huu.
    Vodacom imewapongeza pia wakazi na wenyeji wa mkoa wa Mbeya kwa kuiunga mkono timu yao kwa hali na mali na hivyo kuipatia mafanikio huku hatua yao hiyo ikinogesha pia joto la ligi ndani na nje ya mkoa wa Mbeya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VODACOM WAIPONGEZA AZAM FC KWA UBINGWA BARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top