• HABARI MPYA

    Sunday, April 27, 2014

    UMEWAHI KUTOKEA UONGOZI MBOVU YANGA SC KULIKO HUU WA SASA?- 2

    TUNAINGIA sehemu ya pili ya makala haya ya takafuri ya kina ndani ya klabu ya Yanga SC, tangu ikiwa chini ya Mwenyekiti marehemu Tarbu Mangara hadi Wakili Lloyd Baharagu Nchunga aliyeupisha uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti, Yussuf Manji je- ni wakati klabu hiyo ilipitia mikononi mwa viongozi bomu zaidi.
    Katika sehemu ya kwanza tulitazama zaidi uongozi wa kihistoria wa klabu hiyo chini ya marehemu Mangara na mgogoro wa kwanza ulioigawa klabu hiyo. Endelea.
    Yanga SC ilikuja kutulia baadaye na kurudi kutawala soka ya Tanzania na mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 wimbi la wafadhili wa Kiasia likiongozwa na watu kama Mohamed Viran, Abbas Gulamali (wote marehemu), Murtaza Dewji na wengine likaiteka klabu na neema ikarejea.
    Hata hivyo, baadaye wafadhili wote wakaondoka hadi Ngozoma Matunda anachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu mwaka 1997, Yanga SC ilikuwa ina hali mbaya kiuchumi.
    Pamoja na hayo, Matunda ambaye hakuwa msomi, wala mwenye uwezo wa kifedha aliweza kuiongoza klabu kwa mafanikio ya uwanjani, akiiwezesha kurudia historia ya kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998.
    Mafanikio hayo yalileta mgogoro mkubwa Jangwani, Tarimba Abbas na Abdul Sauko wakiongoza kampeni za kumng’oa Ngozoma hadi walipofanikiwa mwaka 2000. Mungu ampumzishe kwa amani Mzee Matunda, ambaye mwaka 2007 alirejea kama Makamu Mwenyekiti chini ya Mwenyekiti Wakili Imani Madega, unaweza kuona pamoja na kuongoza klabu katika wakati mgumu, bado aliweza kufanya kitu cha kukumbukwa.
    Wakili Nchunga alijijengea sifa moja kubwa pamoja na kuipa Yanga mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Kagame, aliweza kuifunga Simba SC iliyoonekana bora kuliko Yanga SC.
    Hata hivyo, mwisho wa siku kwa kutofautiana itikadi na mitazamo na Manji akiwa mfadhili wa klabu, Nchunga akajikuta kwenye wakati mgumu na hata kipigo cha mabao 5-0 ambacho timu hiyo ilifungwa chini yake mwaka juzi, watu wanaamini ni hujuma.
    Lilikuwa kama shinikizo la kumuondoa Nchunga madarakani na baada ya kipigo hicho cha 5-0 pamoja na kuvamiwa nyumbani kwake, hatimaye Wakili huyo maarufu akanyoosha mikono na kujiuzulu Mei 24, mwaka 2012.
    Wakati anatangaza kujiuzulu, Nchunga alisema; “Sipo tayari kuona klabu Yanga inahujumiwa kwa vile tu mimi ni kiongozi, Kamati ya Utendaji na wale walioteuliwa chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa mafaniko zaidi.”
    “Kwa hekima nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga, kwani ni klabu ninayoipenda hata kama mimi sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu,” alisema.
    Chokochoko zilianzishwa na Baraza la Wazee la klabu hiyo ambao walikuwa wakimshinikiza Nchunga ajiuzulu kabla hata mechi dhidi ya Simba ya 5-0 kwa madai kuwa ameisababisha madeni makubwa klabu hiyo ikiwa ni pamoja na mwenendo mbovu wa timu yao huku wakidai wachezaji wamekosa nidhamu.
    Baada ya kipigo cha 5-0, kuvamiwa nyumbani kwake na kuamua kujiuzulu, Nchunga alisema kitendo kinachofanywa na Baraza hilo la Wazee wakiongozwa na Ibrahimu Akilimali ni usaliti mkubwa ulioambatana na matukio mbalimbali ndani ya klabu hiyo hadi kuupindua uongozi wake.
    “Siwatuhumu wachezaji moja kwa moja, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo na Simba inaonyesha kulikuwa na usaliti mkubwa ambao hatukuweza kuubaini mapema,”alisema Nchunga.
    “Sioni mantiki kwa hoja kuwa tulifungwa kwa vile wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho, au eti mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao tano,”alisema Nchunga.
    “Kwa wanaoijua Yanga, wanafahamu Yanga imewahi kuwa na madeni makubwa katika hoteli mbalimbali, mawakala wa ndege na baadhi tumeyakuta sisi na kuyalipa, hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwapo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa pweke, na bado wachezaji walicheza kwa morali?.”
    “Uongozi wangu ndani ya mwaka mmoja tumechukua mataji matatu, ubingwa wa Ligi Kuu, 2011/2012, Kombe la Kagame na Ngao ya Jamii, ukiachia mechi ya Mei 6 ambayo tulifungwa magoli matano,”alisema Nchunga.
    “Tumefanikiwa kuboresha mkataba wetu na TBL, tumeingia mkataba na Nexus Ltd ambao inatutafutia wadhamini wa ndani na nje, tumefanya kampeni kupitia mitandao na kukusanya data za wanachama na kusajili wapya lengo likiwa ni kukusanya Sh3,000,000 hadi 8,000,000 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu.”
    “Hayo yote tulifanya ili kuondokana na utegemezi wa ufadhili wa mtu mmoja na tayari tulishatuma maombi kwa msajili Manispaa ya Ilala ya kuanzisha Saccoss ya Yanga.”
    “Utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatutafuna kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuondoa uongozi wa kidemokrasia,”alisema Nchunga.
    “Baada ya Mapinduzi kushindikana na TFF kuonya, wazee wakiongozwa na Akilimali wamesikika katika kipindi cha michezo cha radio moja wakidai ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza,”.
    Kwa maelezo haya na hali halisi iliyojitokeza wakati huo, kuna picha ya wazi kwamba watu waliokuwa tayari kuona Yanga inashushwa daraja kuliko kuendelea kuongozwa Nchunga hawakuona tatizo kufungwa 5-0 na mtani wake, ili Mwenyekiti huyowa wakati huo aonekane hafai.
    Walifanikiwa na Julai 14, mwaka 2012 Yanga SC ikapata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Yussuf Manji katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za viongzi waliojiuzulu wakiwemo Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha.
    Clement Sanga alishinda Umakamu Mwenyekiti wakati Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Aaron Nyanda na George Manyama walichaguliwa katika nafasi ya Ujumbe wa kamati ya  Utendaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UMEWAHI KUTOKEA UONGOZI MBOVU YANGA SC KULIKO HUU WA SASA?- 2 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top