• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 26, 2014

  TAMBWE AJIPIGA MNADA, ASEMA YUKO TAYARI KUONDOKA MSIMBAZI AKIPATA DILI ZURI

  Na Reantus Mahima, Dar es Salaam
  "BADO nina mkataba wa mwaka mmoja na Simba lakini timu ikija na dau kubwa niko tayari kujiunga nayo." Ni kauli ya mshambuliaji Amisi Tambwe wa Simba aliyoitoa katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY jijini Dar es Salaam muda mfupi uliopita.
  Aidha, Tambwe, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013/14, amesema amefuatwa kwa nia ya kufanya mazungumzo na baadhi ya watu waliojitambulisha kwake kama wawakilishi wa timu za Yanga na mabingwa wapya Azam FC.
  Amisi Tambwe yuko tayati kuondoka Simba SC akipata dili zuri zaidi

  "Kwa sasa ni mpenzi wa klabu ya Simba, lakini nikisajiliwa na Azam au Yanga, nazo nitazipenda tu," amesema.
  Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Burundi na michuano ya Kombe la Kagame la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati -- Tambwe, alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili Agosti mwaka jana akitokea klabu ya Vital'O ya kwao Burundi.
  Mkali huyo wa kufumania nyavu ameichezea Simba mechi 23 kati ya 26 za Ligi Kuu msimu huu akikosa mechi tatu walizotoka sare ya 2-2 na Rhino Rangers mjini Tabora Agosti 24 mwaka jana baada ya yeye na Mrundi mwenzake Gilbert Kaze kukosa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
  Tambwe pia alikosa mechi ya mzunguko wa kwanza waliyolala 2-1 dhidi ya wasiofungiika Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Oktoba 28 mwaka jana baada ya kuumia katika mechi ya utangulizi waliyotoka suluhu na mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union Oktoba 23.
  Tambwe pia hakuwamo kwenye msafara wa kikosi cha Mcroatia Zdravko Logarusic kilichosafiri kwenda mjini Bukoba, Kagera kumenyana na Kagera Sugar walikotoka sare ya bao moja Aprili 5.
  Wakati Tambwe akikaribisha ofa, tayari kocha wa Azam FC, Mcameroon Joseph Omog ameshaweka wazi kwamba atasajili viungo na washambualiaji kutoka timu za Yanga, Simba na Mbeya City.
  Katika msimu mmoja tu wa kuichezea Simba SC, Tambwe ameifungia mabao 21 klabu hiyo katika mechi 28 za mashindano yote, yakiwemo 19 ya Ligi Kuu yaliyompa ufungaji bora.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAMBWE AJIPIGA MNADA, ASEMA YUKO TAYARI KUONDOKA MSIMBAZI AKIPATA DILI ZURI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top