• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 24, 2014

  KAGAME KUFANYIKA RWANDA, CEFACA YALETA MICHUANO MIPYA YA KLABU, INAANZA MEI MWAKA HUU SUDAN

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limesema mashindano ya Kombe la Kagame yatafanyika Rwanda Agosti mwaka huu, lakini pia limeanzisha mashindano mapya ya klabu, ambayo yatakuwa yanashirikisha mabingwa wa Kombe la FA au washindi wa pili wa Ligi Kuu.
  Taarifa ya CECAFA kwa BIN ZUBEIRY, imesema kwamba mashindano hayo yanaanza mwaka huu na kwa mara ya kwanza yatafanyika nchini Sudan kuanzia Mei 20 hadi Juni 5.
  Safari Kigali; Yanga SC watakwenda kushiriki Kombe la Kagame nchini Rwanda

  Taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu wake, Nicholas Musonye imesema kwamba CECAFA na FA ya Sudan vitagharamia kila kitu kwa timu zitakazoshiriki michuano hiyo kuanzia tiketi, malazi, usafiri wa ndani na zawadi za washindi.
  Katika hatua nyingine, CECAFA imesema Rwanda wapo katika mchakato wa maandalizi Kombe la Kagame, michuano ambayo hushirikisha mabingwa wa Ligi Kuu za nchi wanachama wake.
  Aidha, Musonye amesema kwa kuwa Fainali za soka za Olimpiki zitafanyika mwaka 2016, ili kuzipa matayarisho nchi wanachama wake, CECAFA imeandaa mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 23, ambayo yatafanyika nchini Sudan pia Septemba mwaka huu.
  Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama CECAFA Challenge Musonye amesema yatafanyika Ethiopia kati ya Novemba na Desemba, wakati wiki iliyopita CECAFA ilisaini Mkataba wa miaka minne na Televisheni ya SuperSport kwa ajili ya kurusha mashindano yote ya Baraza hilo.
  Musonye pia amesema Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limewakubalia kuandaa kozi ya Wakurugenzi wa Mawasiliano wa nchi wanachama wa CECAFA, ambayo itafanyika Dar es Salaam kati ya Aprili 30 na Mei 3. 
  Wenyeviti na marais wote wa FA wanachama wa CECAFA pamoja na Makatibu wao na Maofisa Mawasiliano watashiriki kozi hiyo itakayofunguliwa na Katibu wa FIFA, Mfaransa Jerome Valcke atakayewasili Dar es Salaam Aprili 30, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAGAME KUFANYIKA RWANDA, CEFACA YALETA MICHUANO MIPYA YA KLABU, INAANZA MEI MWAKA HUU SUDAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top