• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 22, 2014

  NGASSA: MIMI NDIYE BORA TANZANIA, VITU VINAONGEA VYENYEWE

  Na Baby Akwitende, Dar es Salaam
  MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga na timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Mrisho Ngassa, amesema kuwa anastahili kuwa mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wa mwaka 2013/ 2014 uliomalizika kutokana na kuisaidia timu yake kumaliza ikiwa ya pili kwenye msimamo wa ligi.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo mjini Dar es Salaam, Ngassa, alisema kuwa katika mechi zote alizocheza ameonyesha kiwango cha juu na kufanikiwa kufunga mabao 13.
  Bora zaidi; Mrisho Ngassa amesema yeye ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Bara

  Ngassa alisema kwamba licha ya kucheza mechi chache za ligi kutokana na kufungiwa, bado aliweza kuisaidia Yanga kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho mwakani licha ya ushindani uliokuwepo kutoka kwa Mbeya City.
  "Nimefanya vizuri, nimecheza mechi chache ukilinganisha na Amisi Tambwe na Kipre Tchetche, lakini nimekuwa mfungaji bora katika timu yangu na nimetengeneza pasi 17 za mabao waliyofunga wenzangu," alisema Ngassa.
  Alieleza pia bado anaamini ametoa mchango kwa nchi kwa kuifungia timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) mabao muhimu kwenye mashindano ya Kombe la Challenge mwaka jana nchini Kenya.
  Mshambuliaji huyo amesema pia anatarajia kuonyesha makali yake kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame) yatakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu hapa nchini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NGASSA: MIMI NDIYE BORA TANZANIA, VITU VINAONGEA VYENYEWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top