• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 27, 2014

  MALINZI: KOCHA MPYA STARS HATAINGILIWA

  Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) amesema kwamba atahakikisha kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars Mholanzi Mart Nooij haingiliwi katika utendaji wake.
  Malinzi aliyasema hayo jana wakati akimtambulisha mwalimu huyo mpya kwa Waandishi wa Habari Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya mchezo dhidi ya Burundi ambao Taifa Stars ilitandikwa mabao 3-0.
  Akiwa amefuatana na Makamu wake Wallace Karia, amesema anafurahi kumtangaza Nooij na ana matarajio kuwa Tanzania itanufaika na uzoefu wake mkubwa wa ukocha, hasa katika bara la Afrika.
  Hataingiliwa; Kocha mpya wa Taifa Stars, Mart Nooij baada ya kuwasili Alfajiri ya jana

  “Nawaahidi Watanzania kuwa sitomuingilia kocha katika kazi yake. Kama mimi sitomuingilia kocha, basi hakuna mtu yeyote atakayemuingilia. Tumemwajiri yeye kwa vile ni mtaalamu, hivyo hakuna sababu ya kumuingilia,” amesema Rais Malinzi.
  Naye Nooij ambaye amepewa mkataba wa miaka miwili amesema yeye ni mtu wa maneno mafupi, hawezi kuahidi kitu lakini ana matarajio ya kuifanya Taifa Stars ifanye vizuri katika mashindano mbalimbali.
  Amesema kabla ya kukubalia kufundisha Taifa Stars alikuwa na klabu ya St. Georges ya Ethiopia, lakini vilevile amewahi kufundisha mpira wa miguu barani Afrika katika nchi za Burkina Faso, Mali na Msumbiji.
  Nooij alikuwa jukwaani jana wakati Stars inachapwa mabao 3-0 na kesho anatarajiwa kwenda na timu hiyo Mbeya kambini kuanza kazi ya kuleta mabadiliko. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MALINZI: KOCHA MPYA STARS HATAINGILIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top