• HABARI MPYA

    Wednesday, April 23, 2014

    UMEWAHI KUTOKEA UONGOZI MBOVU YANGA SC KULIKO HUU WA SASA?- 1

    TAFAKARI kwa kina tangu Mwenyekiti wa Yanga SC ni marehemu Tarbu Mangara hadi Wakili Lloyd Baharagu Nchunga aliyeupisha uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti, Yussuf Manji ni wakati klabu hiyo ilipitia mikononi mwa viongozi bomu zaidi.
    Anza na uongozi ambao ulipitia kwenye misukosuko mingi mfano wa Mzee Mangara mwenyewe na baadaye marehemu Ngozoma Matunda, tafakari wakati wao madarakani.
    Mwaka 1974 Yanga SC ilifanya ziara nchini Brazil, ambako ilikutana na marehemu Tambwe Leya, raia wa iliyokuwa Zaire, sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa anasomea ukocha nchini humo. Kukwepa gharama za kummiliki aliyekuwa kocha wao ghali, Profesa Victor Stanslescu, aliyefanya kazi ya kihistoria Jangwani, Yanga iliamua kumchukua Tambwe ambaye mshahara aliokuwa akilipwa haukufika hata nusu ya mshahara wa Mromania huyo.
    Victor alianzisha mpango wa kufundisha soka vijana. Alikuwa akichukua mipira yake mingi na kuwaita vijana, ili waonyeshe uwezo wao mbele ya macho yake. Waliomkuna kwa vipaji vyao aliwachukua na kwenda kuunda kikosi cha vijana kilichokuwa madhubuti cha klabu hiyo.
    Kwa mtaji huo, ndipo walipopatikana wanasoka nyota Tanzania kama Juma Pondamali 'Mensah', Mohamed Adolph Rishard, Mohamed Yahya 'Tostao', Kassim Manara, Mohamed Mkweche, Jaffar Abdulrahaman, Hamisi Swedi, Gordian Mapango na wengineo. Wakati huo, Mwenyekiti wa Yanga alikuwa ni marehemu Mangara.
    Baada ya Tambwe kutua Yanga, alitaka kufanya mabadiliko kwenye kikosi cha kwanza, akitaka kutumia wachezaji vijana, akisema kwamba wakongwe uwezo wao unaelekea ukingoni. Lakini ni kipindi hicho Yanga inatawala soka ya Tanzania, imetoka kutwaa ubingwa mfululizo tangu mwaka 1968 hadi 1972. Mwaka 1973 watani wao wa jadi, Simba, ndio waliotwaa taji hilo, lakini mwaka 1974 Yanga walitwaa tena ubingwa wa nchi.
    Mwaka 1975, Yanga ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame, ikiifunga Simba kwenye fainali mabao 2-0 visiwani Zanzibar. Wafungaji wa mabao hayo walikuwa wale wale wauaji wa fainali ya Klabu Bingwa ya Taifa mwaka 1974, Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, Sunday Manara na Gibson Sembuli (marehemu), katika ushindi wa 2-1, bao la Simba likifungwa na Adamu Sabu (sasa marehemu pia).
    Kwa sababu hiyo, ilikuwa ngumu kuwashawishi watu kwamba wachezaji wa Yanga wamezeeka.
    Kipindi hicho wakongwe wa Yanga walikuwa akina Elias Michael 'Nyoka Mweusi', Muhidini Fadhili na Patrick Nyaga, wote makipa, mabeki Boy Iddi Wickens, Athumani Kilambo 'Baba Watoto', Badi Saleh, Hassan Gobbos, Omar Kapera, viungo Abdurahman Juma, Abdurahman Lukongo, Sunday Manara 'Computer', Leonard Chitete, na washambuliaji Gibson Sembuli, Kitwana Manara 'Popat' na Maulid Dilunga.  
    Lakini pamoja na ubishi huo, baada ya kushindwa kutetea Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki mjini Mombasa, Kenya, uliibuka mgogoro mkubwa na wa kihistoria ndani ya klabu hiyo.
    Yanga ilianza vizuri tu katika kundi lake B, ikiifunga 2-1 Mseto SC ya Morogoro, kabla ya kuitandika Green Bufalloes ya Zambia 2-0, Bata Bullets ya Malawi 3-1, iliongoza kundi hilo, ikifuatiwa na Mseto, mabingwa wa Tanzania mwaka 1975.
    Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga 3-0 Express ya Uganda wakati Mseto iliona cha mtema kuni kwa Luo, baada ya kutandikwa 5-0. Yanga iliuacha ubingwa Mombasa, baada ya kulala 2-1 kwa Luo kwenye fainali.
    Timu iliporejea nyumbani, mgogoro ukaibuka, wanachama walikuja juu na kutaka kumpiga Mwenyekiti wao wakati huo, mzee Mangara, ambaye aliokolewa kwa kutoroshewa mlango wa nyuma. 
    Vyanzo vinasema kwamba, wanachama walifika na bakora Jangwani wakitaka kumchapa Mangara. Walikuwa wanataka hesabu za mapato na matumizi ya klabu, lakini walikuwa wenye ghadhabu wakifanya fujo, hivyo ili kuepuka balaa hilo, Mangara alitoroshwa na kuwaacha solemba waliokuwa wanamsubiri nje wamchape bakora. Mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni uliitafuna Yanga kwa miaka minne.
    Kipindi hicho Yanga ilikuwa safi kiuchumi, ilikuwa ina mabasi matano yaliyokuwa yakiingizia fedha klabu, Uwanja wa Kaunda uliojengwa kwa mkopo wa Sh 500,000 wa Benki ya Nyumba (THB) ulikuwa bado mpya unavutia watu wengi wakati wa mazoezi ya timu hiyo.  Yanga ilisaidiwa pia fedha na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Abeid Karume kiasi cha Sh milioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi.
    Aidha, Yanga ilikuwa ina mfadhili wake, aliyekuwa akiwasaidia fedha nyingi, Shiraz Sharrif, ingawa naye baada ya mgogoro alihamia Pan African, kwa sababu alikuwa ana imani na Mangara.
    Kutokana na jinsi Mangara alivyoishi vizuri na wachezaji wa klabu hiyo, alikuwa akiwapenda akiwafanya marafiki, basi wachezaji wote waliamua kumfuata na kuachana na Yanga. Walifikia hatua hiyo, baada ya jitihada za kushinikiza Mangara arejeshwe, ikiwemo kuandamana, kushindikana. Kwa jeuri, Yanga nayo ilisema acha waende na itaunda timu mpya.
    Hadi leo, ukiwauliza watu wa Yanga sababu za kugombana na mzee Mangara, wapo watakaosema wanachama walikuwa wakorofi na wengine watasema mzee huyo alikuwa akinufaika kwa kupitia mgongo wa Yanga. 
    Lakini unaweza kupata picha ya uongozi wa marehemu Mangara Yanga SC ulivyozalisha mafanikio klabuni- ingawa mwisho wake haukuwa mzuri. ITAENDELEA JUMAPILI.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UMEWAHI KUTOKEA UONGOZI MBOVU YANGA SC KULIKO HUU WA SASA?- 1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top