• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 24, 2014

  PIGO LINGINE STARS, NGASSA AUMIA NAYE ATAKOSA MECHI NA BURUNDI KESHOKUTWA

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  MSHAMBULIAJI tegemeo wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa ataukosa mchezo wa Jumamosi wa kimataifa dhidi ya Burundi baada ya kuumia mazoezini juzi.
  Ngassa aliumia nyama za paja baada ya kuteleza kutokana na mvua wakati wakiwa mazoezini Mbezi Beach, Stars ikijiandaa na mchezo dhidi ya int’hamba Murugamba keshokutwa.
  “Sitaweza kucheza mechi na Burundi, kesho natarajia kwenda kumuona Daktari kwa vipimo zaidi, nasikitika kuikosa mechi hii, lakini inabidi nikubali hali halisi,”alisema mshambuliaji huyo wa Yanga SC.
  Mrisho Ngassa kushoto ataukosa mchezo na Burundi baada ya mazoezini juzi

  Kukosekana kwa Ngassa ni pigo lingine kwa Stars kuelekea mchezo huo, kwani tayari washambuliaji wengine wawili tegemeo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya DRC hawatakuja.  
  Wachezaji hao wameomba udhuru kwa sababu ya majukumu ya kuipigania klabu yao katika vita ya ubingwa wa ligi ngumu ya DRC msimu huu.
  Wachezaji wanaobaki katika kikosi cha Salum Mayanga sasa ni makipa, Aishi Manula, Mwadini Ally wa Azam FC na Deogratias Munishi wa Yanga, mabeki Abdi Banda (Coastal Union), Aidan Michael (Ruvu Shooting), Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Kevin Yondani (Yanga SC) na Said Mourad (Azam).
  Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Frank Domayo (Yanga), Himid Mao (Azam) na Jonas Mkude (Simba) wakati washambuliaji ni Athanas Mdamu (Alliance), Haruna Chanongo (Simba), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Markhiya, Qatar), Ramadhan Singano (Simba), Simon Msuva (Yanga).
  Pia kuna chipukizi walioitwa kutoka katika kikosi cha maboresho ya timu ambao ni kipa Benedicto Tinoko Mlekwa (Mara), mabeki wa kati; Emma Namwondo Simwanda (Temeke) na Joram Nason Mgeveje (Iringa), mabeki wa pembeni Omari Ally Kindamba (Temeke), Edward Peter Mayunga (Kaskazini Pemba) na Shiraz Abdallah Sozigwa (Ilala).
  Viungo ni Yusuf Suleiman Mlipili (Temeke), Said Juma Ally (Mjini Magharibi), Abubakar Ally Mohamed (Kusini Unguja), Hashim Ramadhan Magona (Shinyanga), Omari Athumani Nyenje (Mtwara) na Chunga Said Zito (Manyara).
  Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ipo kambini kwenye hoteli ya Kunduchi Beach ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Kenya.
  Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa VIP A kiingilio kitakuwa sh. 20,000 wakati VIP B na C ni sh. 10,000. Mechi hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PIGO LINGINE STARS, NGASSA AUMIA NAYE ATAKOSA MECHI NA BURUNDI KESHOKUTWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top