• HABARI MPYA

    Thursday, April 17, 2014

    KINYANG’ANYIRO CHA KUCHEZA HATUA YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA CHAANZA WIKIENDI HII

    MECHI za kwanza za mchujo kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinatarajiwa kupigwa wikiendi hii kwa timu 16 kushuka viwanjani kuwania nafasi nane za makundi mawili.
    Inatarajiwa kuwa michuano mikali kutokana na timu madhubuti zilizopo kwenye hatua hiyo, inayojumuisha timu nane zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Kaizer Chief ni miongoni mwa timu hizo pamoja na mabingwa wa sasa wa Ligi ya Mabingwa, Al-Ahly ya Misri ambao watamenyana na Difaa El-Jadidi ya Morocco wikiendi hii katika Uwanja wa Jeshi la Anga wa Cairo.
    Safari ya Al Ahly katika michuano ya Afrika mwaka huu ilianzia Dar es Salaam ikaitoa Yanga SC ya Tanzania, kabla ya kutolewa na Al Ahly Benghazi ya Libya

    Ahly ni miongoni mwa timu saba zilizowahi kushinda mataji ya Afrika zinazowania nafasi hizo nane dhidi ya timu nane zilizofuzu katika mchakato wa Kombe la Shirikisho.
    AC Leopards ya Kongo na Etoile du Sahel ya Tunisia zimewahi kubeba taji hilo la Kombe la Shirikisho, michuano ambayo ni muunganiko wa iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi na Kombe la CAF iliyojumuishwa miaka 10 iliyopita.
    ASEC Mimosas imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika sawa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, wakati Horoya ya Guinea na CA Bizertin ya Tunisia zimewahi kubeba Kombe la Washindi.
    Ahly iliyotolewa katika Ligi ya Mabingwa kwa vipigo vya kustaajabisha vya nyumbani na ugenini kutoka kwa Al-Ahly Benghazi ya Libya, inapewa nafasi sasa ya kuzinduka katika Kombe la Shirikisho.
    Kaizer Chiefs imelazimishwa kuhamishia mechi yake na ASEC Mimosas kutoka Uwanja wa Soccer City hadi Uwanja mwingine Soweto, uitwao Dobsonvill.
    Wakati Chiefs ilitolewa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Ligi ya Mabingwa, ASEC iliitoa CS Constantine ya Algeria katika Kombe la Shirikisho.
    Klabu za Tunisia zimetawala miaka 10 ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa katika mashindano ya klabu barani, ikitoa mabingwa wanne na washindi wa pili watatu, na Etoile Sahel na Bizertin zinaanzia ugenini wikiendi hii.
    Etoile itaifuata Horoya, ambao ndoto zao za Ligi ya Mabingwa zilizimwa na klabu nyingine ya Tunisia, CS Sfaxien, na Bizertin itaivaa Nkana mjini Kitwe, Zambia.
    Bayelsa United, timu ya mwisho ya Nigeria katika mbio za ubingwa wa mataji ya CAF mwaka huu, itakuwa mgeni wa Sewe San Pedro ya Ivory Coast na Leopards itakuwa mwenyeji wa Medeama ya Ghana.
    Mechi baina ya timu za Mali tupu, Real Bamako na Djoliba itafanyika Bamako, wakati Coton Sport ya Cameroon itamenyana na Petro Atletico ya Angola mjini Garoua kukamilisha mechi nane za kwanza. Mechi za marudiano zitachezwa wikiendi ya kati ya Aprili 25 na 27 na droo ya makundi ya Kombe la Shirikisho itapangwa mjini Cairo Aprili 29.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KINYANG’ANYIRO CHA KUCHEZA HATUA YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA CHAANZA WIKIENDI HII Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top