• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 27, 2014

  KILA LA HERI NGORONGORO HEROES, YAMENYANA NA KENYA LEO KUWANIA TIKETI YA SENEGAL 2015

  Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
  TIMU ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo itamenyana na vijana wenzaao wa Kenya katika mechi ya marudiano Raundi ya Kwanza kuwania tiketi ya fainali za Afrika mwakani nchini Senegal.
  Mechi hiyo itakayochezewa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni ndiyo itakayoamua timu itakayocheza raundi inayofuata katika michuano hiyo dhidi ya Nigeria.
  Ngorongoro itatakiwa kuwapoza machungu Watanzania ya kaka zao, Taifa Stars (pichani) kufungwa 3-0 na Burundi jana

  Ngorongoro Heroes inayofundishwa na John Simkoko ilitoka suluhu na Kenya katika mechi ya kwanza iliyochezwa Machakos, Kenya wiki tatu zilizopita, na imekuwa kambini jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili kujiwinda kwa mechi hiyo.
  Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 na sh. 5,000 ambapo Kenya iliyowasili nchini jana (Aprili 25 mwaka huu) usiku imefanya mazoezi yake ya mwisho jana (Aprili 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa.
  Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Burundi wakiongozwa na Pacifique Ndabihawenimana wakati Kamishna ni Tarig Atta Salih kutoka Sudan. Kila la heri Ngorongoro Heroes.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KILA LA HERI NGORONGORO HEROES, YAMENYANA NA KENYA LEO KUWANIA TIKETI YA SENEGAL 2015 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top