• HABARI MPYA

    Wednesday, April 30, 2014

    UMEWAHI KUTOKEA UONGOZI MBOVU YANGA SC KULIKO HUU WA SASA?- 3

    TUNAINGIA sehemu ya tatu ya makala haya ya takafuri ya kina ndani ya klabu ya Yanga SC, tangu ikiwa chini ya Mwenyekiti marehemu Tarbu Mangara hadi Wakili Lloyd Baharagu Nchunga aliyeupisha uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti, Yussuf Manji je- ni wakati klabu hiyo ilipitia mikononi mwa viongozi bomu zaidi.
    Katika sehemu ya pili tulitazama zaidi misukosuko iliyoukuta uongozi wa Wakili Lloyd Baharagu Nchunga hadi timu kufungwa 5-0 na mtani wake Simba SC, hivyo akajiuzulu na kuchaguliwa viongozi wapya chini ya Yussuf Manji. Endelea.

    Kwa misimu miwili ya uongozi wa Manji Yanga SC, klabu imetumia fedha nyingi kusajili na maandalizi ya timu, lakini haijapata mafanikio makubwa zaidi ya taji moja la Ligi Kuu na moja la Kagame.
    Yanga SC imeweka kambi Uturuki mara mbili, imekuwa ni wastani wa matumizi yasiyopungua Sh. Milioni 300 kwa ajili ya usajili kila msimu, lakini uwanjani imeendelea kuwa timu ya kawaida.
    Alhaj Ismail Aden Rage alimtangulia Abdallah Bin Kleb Kigali katika kuwania saini ya beki Mbuyu Twite akiwa APR wakati huo na akafanikiwa kumsainisha.
    Bin Kleb akiwa anajua mchezaji huyo amesaini Simba SC, akaenda kumshawishi asaini na Yanga pia na wakaunda mkakati ‘mzuri’ wa kuondoa uhalali wake kutoka APR hadi FC Lupopo ya DRC.
    Yanga ililazimika kutumia zaidi ya dola 100,000 kutengeneza magumashi hiyo na pia Mbuyu akawapa sharti la kumsajili na ndugu yake, Kabange Twite ambaye hawakuwa wanamuhitaji.
    Mwisho wa siku, fedha za Simba SC ambazo alichukua Mbuyu zilirudishwa pamoja na gharama za safari ya Rage. Hasara gani walipata Simba SC zaidi ya muda aliopoteza Rage kwenda Rwanda. Na je, uko wapi ujanja au ushindi wa Bin Kleb kuiingiza klabu kwenye gharama kubwa, magumashi ya uhalali wa mchezaji kutoka APR hadi Lupopo na shinikizo la kumsajili mchezaji mwingine ambaye hawakuwa wakimuhitaji. Kabange alikula, kulala na kulipwa stahiki zake zote za Mkataba kwa msimu mzima kabla ya kutemwa, lakini hakuwahi kuitumikia katika mechi yoyote ya mashindano.     
    Kusajili wachezaji wa Simba SC kila unapowadia muda wa usajili, imekuwa desturi ya uongozi huu wa Yanga, ingawa baada ya muda mfupi tu wachezaji hao huonekana hawafai.
    Ally Mustafa ‘Barthez’ aliporuhusu mabao matatu Simba ikatoka nyuma kwa 3-0 na kupata sare ya 3-3, akasajiliwa Juma Kaseja, ambaye naye sasa wameshamuona wa kazi gani.
    Kevin Yondan wakati fulani ilielezwa hadi alifichua siri ya kutekwa na viongozi wa Simba SC, lakini sasa naye hafai. Okwi naye yale yale.
    Lakini haitakuwa ajabu katika usajili unaofuata viongozi hawa wakiendelea kuwapo madarakani wakamsaini mchezaji mwingine wa Simba SC.
    Yanga SC ilipokwenda Cairo, Clement Sanga aliporudi akajisifu eti yeye ni kiongozi wa kwanza kupewa bajeti ya matumizi na akarudi na salio kubwa.
    Sanga anataka kumdanganya nani? Mwaka huu ndiyo mara ya kwanza kihistoria Yanga SC inakwenda kucheza mechi ya ugenini kwa gharama zake- miaka ya nyuma zaidi ya posho kwa wachezaji, klabu hiyo haina rekodi ya kutumia fedha nyingine, bali hugharamiwa na wenyeji wao kwa mujibu wa kanuni za CAF.
    Mwaka huu Manji aliwekeza kwenye ushindi zaidi, akatoa fedha timu ikajigharimie ili kukwepa kile wanachoamini fitina za wenyeji, lakini kwa kuwa viongozi waliokwenda si wa mpira na hawajui mipango, wakashindwa kushinda mechi moja nyepesi sana.
    Tuchukulie kama matokeo yale ni bahati mbaya, lakini timu iliporejea Dar es Salaam haikurudishwa katika kambi nzuri, wachezaji walikusanyika makao makuu ya klabu kwa safari ya Morogoro kwenda kucheza na Mtibwa Sugar.
    Matokeo yake wakatoa sare na Mtibwa pungufu baada ya mchezaji wake mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu, lakini bado halikuwa fundisho, uzembe ukaendelea na timu ikapoteza pointi saba ndani ya mechi tatu, pamoja na sare ya Azam pungufu na kukosa penalti juu na kufungwa na Mgambo JKT pungufu.
    Desturi ya kuwatoa kafara wachezaji baada ya matokeo mabaya imeendelea chini ya uongozi wa Manji na baada ya mchezo wa Mgambo kuna wachezaji waliondolewa kabisa kambini bila sababu za msingi wala kujali klabu iliwekeza fedha kiasi gani. 
    Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Athumani Iddi ‘Chuji’ na David Luhende hawakucheza mechi nyingine yoyote tangu mchezo na Mgambo, je nini sababu?
    Uongozi wa Yanga SC umekuwa ukizusha propaganda dhidi ya Azam, wakati uwanjani imeendelea kuwa timu dhaifu na matokeo ya kunusurika kulala mbele ya Simba SC dhaifu katika mechi ya mwisho ya msimu ni kielelezo tosha.
    Jiulize, kama aliondolewa Nchunga kwa gharama ya 5-0 na Yanga inashindwa kuifunga japo 1-0 Simba SC iliyomaliza Ligi katika nafasi ya nne, je wapinzani wao wakijipanga baada ya uchaguzi wa mwezi ujao, tutarajie nini? 
    Wakati wa kampeni za kuomba uongozi Manji aliwaahidi wanachama kujenga Uwanja, kukarabati jengo la makao makuu, kuanzisha vitegauchumi kama duka kubwa la vifaa vya michezo na kuweka wapangaji zikiwemo ofisi za taasisi za kifedha. Leo kuna nini pale Jangwani? ITAENDELEA JUMAPILI
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UMEWAHI KUTOKEA UONGOZI MBOVU YANGA SC KULIKO HUU WA SASA?- 3 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top