• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 25, 2014

  TAIFA STARS, BURUNDI ZAAHIDI SOKA MARIDADI

  Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
  MAKOCHA wa timu za Taifa za Tanzania (Taifa Stars) na Burundi (Intamba Mu Rugamba), Salum Mayanga na mwenzake Niyungeko Alain Olivier wameahidi burudani ya nguvu kwenye mechi yao itakayochezwa kesho (Aprili 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mechi hiyo ya kirafiki ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar itachezeshwa na refa Anthony Ogwayo kutoka Kenya na itaanza saa 10 kamili jioni. Ogwayo atasaidiwa na Gilbert Cheruiyot na Oliver Odhiambo wote pia kutoka Kenya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Israel Mujuni wa Tanzania wakati Kamishna ni Charles Ndagala.
  Taifa Stars mpya italeta raha kesho?

  Mayanga amesema wanatumia mechi hiyo kama sehemu ya maandalizi ya mechi za mchujo za Kombe la mataifa ya Afrika, na ameahidi kuchezesha baadhi ya wachezaji waliopatikana kwenye mpango wa maboresho ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager.
  Naye Niyungeko amesema amekuja na kikosi imara ambacho pia kitakuwa na washambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe na Didier Kavumbagu wa Yanga, lengo lao ni kuhakikisha wanapata ushindi kwa vile Taifa Stars imekuwa ikiwasumbua kila wanapokutana nayo.
  Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa VIP A kiingilio kitakuwa sh. 20,000 wakati VIP B na C ni sh. 10,000.
  Wakati huo huo, Kocha Mkuu mpya wa Taifa Stars, Martinus Ignatius Maria maarufu kama Mart Nooij atatambulishwa kwa waandishi wa habri kesho Jumamosi (Aprili 26 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAIFA STARS, BURUNDI ZAAHIDI SOKA MARIDADI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top