• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 29, 2014

  AFRICAN LYON WAALIKWA BARCELONA, WATAJIFUA JIRANI KABISA NA CAMP NOU

  Na Dina Ismail, Dar es Salaam
  KLABU ya African Lyon inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, imepata mwaliko wa kwenda kuweka kambi mjini Barcelona nchini Hispania.
  Taarifa ya African Lyon iliyotumwa BIN ZUBEIRY jana, imesema kwamba, mwaliko huo wamepewa na kampuni ya Aspire Management, inayojishughulisha na masuala ya michezo na ushauri wa kibiashara.
  Tunakwenda Hispania; Mmiliki wa African Lyon, Rahim Kangezi 'Zamunda' amesema wamealikwa Barcelona 

  Taarifa hiyo imesema Lyon iliyoteremka kutoka Ligi Kuu misimu miwili iliyopita, itafanya mazoezi katika viwanja vya Centre Esportiu na Aristides Mallol ambavyo vimesifiwa ni vizuri na kwamba wachezaji watafanya mazoezi na pia kuuona Uwanja wa FC Barcelona.
  Taarifa imesema kutoka viwanja vya mazoezi watakavyofanyia African Lyon inachukua dakika mbili tu kufika Uwanja wa Camp Nou kwa kutembea na kwamba Aspire wataiandalia mechi nne za kirafiki timu hiyo ya Tanzania.
  “Pia wataandaliwa walimu wa Katalunya kutoka klabu kubwa kuja kuwafundisha wachezaji wa African Lyon,”imesema taarifa ya timu hiyo inayomilikiwa na mjanja wa mjini Rahim Kangezi ‘Zamunda’ aliyeinunua kwa mfanyabiashara mkubwa na mwanasiasa Mohammed ‘Mo’ Dewji miaka minne iliyopita, ambaye naye aliinunua kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wa soko la Mbagala, enzi hizo ikiitwa Mbagala Market.
  Hata hivyo, taarifa ya African Lyon, klabu iliyoibua wachezaji kadhaa nyota nchini akiwemo Mbwana Samatta, ambaye sasa anacheza TP Mazembe ya DRC haijasema watakwenda lini Katalunya na watakuwa huko kwa muda gani.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AFRICAN LYON WAALIKWA BARCELONA, WATAJIFUA JIRANI KABISA NA CAMP NOU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top