• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 25, 2014

  AZAM YATOA SHARTI MOJA TU KUSHIRIKI MICHUANO MIPYA YA CECAFA SUDAN

  Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
  AZAM FC itashiriki michuano mipya ya klabu inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) iwapo tu itasogezwa mbele.
  Tovuti ya klabu hiyo, imemnukuu Katibu Mkuu wake, Nassor Idrissa Mohammed ‘Father’ akisema kwamba wamepata mwaliko wa CECAFA kuombwa kushiriki michuano hiyo ya Mei mwaka huu, lakini wametoa jibu kwa muda uliopangwa, hawataweza.
  “Tumewasiliana na CECAFA baada ya kutuomba tutume orodha ya watakaokwenda Sudan, na tumewaambia wazi kwamba muda ambao michuano imepangwa kufanyika, hatutaweza, ila kama watasogeza mbele, tunaweza kujipanga na kwenda,”alisema Father.
  Wachezaji wa Azam FC wamepewa likizo hadi Juni 15, hivyo uwezekano wa kushiriki mashindano mapya ya CECAFA Mei mwaka huu nchini Sudan ni mdogo

  Father alisema kwa sasa wachezaji wa Azam FC wapo likizo hadi Juni 15 baada ya kumaliza msimu vizuri na ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakati michuano hiyo mipya itakayoshirikisha mabingwa wa Kombe la FA au washindi wa pili wa Ligi Kuu itafanyika nchini Sudan kuanzia Mei 20 hadi Juni 5.
  Azam imemaliza Ligi Kuu na pointi 62 dhidi ya 56 za waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC na kuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo.
  Hata hivyo, kwa kuwa Yanga SC atashiriki Kombe la Kagame nchini Rwanda Agosti mwaka huu, washindi wa pili ya msimu uliopita, Azam FC ndio watashiriki michuano hiyo mipya ya CECAFA.
  Iwapo CECAFA haitakuwa tayari kusogeza mbele michuano hiyo, kuna uwezekano Tanzania ikawakilishwa na washindi wa tatu wa msimu uliopita, Simba SC au wa mwaka huu Mbeya City- itategemea na maamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na utayari wa timu mojawapo kati ya hizo.
  Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM YATOA SHARTI MOJA TU KUSHIRIKI MICHUANO MIPYA YA CECAFA SUDAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top