• HABARI MPYA

    Friday, April 18, 2014

    OMOG: UBINGWA SI LELEMAMA, AWAPA PONGEZI WACHEZAJI WAKE

    Na Baby Akwitende, Dar es Salaam
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Azam ya jijini Dar es Salaam, Joseph Omog, amesema kwamba kikosi chake kilikabiliwa na changamoto mbalimbali lakini walipambana na kuhakikisha wanakuwa mabingwa wapya ya Ligi Kuu ya Bara msimu huu.
    Azam imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Bara kwa mara ya kwanza baada ya juzi kuigunga Mbeya City mabao 2-1 na kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY, Mcameroon Omog, alisema kuwa haikuwa kazi rahisi timu yake kufikia mafanikio hayo lakini juhudi na kujituma kwa wachezaji wake ndio siri pekee ya mafanikio waliyoyapata.
    Wachezaji wa Azam FC katika picha ya pamoja na benchi la Ufundi la timu hiyo. Hawa ndiyo mabingwa wapya wa Tanzania Bara

    Omog alisema kuwa kila siku walikuwa wakijipanga kusaka ushindi ili watimize malengo yao na wanajisikia furaha kwa kuibuka mabingwa wapya.
    "Haikuwa kazi rahisi kupata mafanikio haya, tumepambana kwa nguvu zetu zote katika kila mechi tuliuocheza...tuna furaha sana kwa kuwa mabingwa msimu huu," alisema Omog.
    Kocha huyo aliwashukuru wachezaji, viongozi na wadau wa timu hiyo kwq kufanikisha ushindi katika mechi mbalimbali walizocheza.
    "Ni mafanikio makubwa na tunajivunia kuyafikia, tulipambana sana na tunashukuru tumepata majibu ya juhudi zetu," aliongeza.
    Alisema kwamba watahakikisha wanashinda katika mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu ili kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa bila kufungwa.
    Mabingwa hao wapya watakabidhiwa kikombe chao krsho Jumamosi baada ya mechi hiyo kumalizika itakayofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini.
    Waliokuwa wapinzani wao katika mbio hizo, Yanga wenye pointi 55 nao wamekata tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho mwakani wakati Azam itacheza kwa mara ya kwanza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OMOG: UBINGWA SI LELEMAMA, AWAPA PONGEZI WACHEZAJI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top