• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 29, 2014

  REAL YAISUKUTUA ‘KAVU KAVU’ BAYERN MUNICH, YAITANDIKA 4-0 NA KUIVUA UBINGWA WA ULAYA

  KWISHA habari yao! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kuhusu Bayern Munich baada ya usiku huu kutandikwa mabao 4-0 na Real Madrid katika Nusu Fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Uwanja wa nyumbani kwao, Allianz Arena mjini Munich, Ujerumani.  
  Maana yake- Bayern wamevuliwa ubingwa wa Ulaya kwa kipigo cha jumla cha mabao 5-0, baada ya awali kuchapwa 1-0 Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid katika Nusu Fainali ya kwanza na Real inaingia Fainali kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12, ambako itakutana na ama Chelsea au majirani zao Atletico Madrid ya Hispania pia.
  Tumewaangamiza; Ronaldo kushoto akishangilia baada ya kufunga bao la tatu lililoikata maini kabisa Bayern Munich
     

  Shujaa wa Real alikuwa ni Sergio Ramos aliyefunga mabao mawili, la kwanza dakika ya 16 pasi ya Luka Modric na la pili dakika ya 20 pasi ya Pepe kabla ya Mwanasoka wa Bora Dunia, Cristiano Ronaldo kumaliza kazi kwa kufunga mabao mawili dakika ya 34 pasi ya Gareth Bale na dakika ya 90.
  Kipindi cha pili, Bayern inayofundishwa na kocha Mspanyola, Pep Guardiola ilijikaza na kukataa kuruhusu mabao zaidi, hivyo kukubali kutema taji kwa kichapo cha 5-0. 
  Real inayofundishwa na Mtaliano Carlo Ancelotti sasa inasubiri mshindi wa jumla wa Nusu Fainali ya pili kesho Uwanja wa Stamford Bridge kati ya wenyeji Chelsea na Atletico Madrid, baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza Hispania ili kukutana nayo katika fainali Jumamosi ya Mei 24, mwaka huu Uwanja wa Sport Lisboa mjini Benfica Ureno.
  Kikosi cha Bayern Munich kilikuwa: Neuer, Lahm, Dante, Boateng, Alaba, Schweinsteiger, Kroos, Ribery/Gotze dk73, Muller/Pizarro dk73 na Robben, Mandzukic/Martinez dk46.
  Real Madrid: Casillas, Carvajal, Pepe, Ramos/Varane dk75, Coentrao, Alonso, Modric, Di Maria/Casemiro dk84, Ronaldo, Bale na Benzema/Isco dk80.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: REAL YAISUKUTUA ‘KAVU KAVU’ BAYERN MUNICH, YAITANDIKA 4-0 NA KUIVUA UBINGWA WA ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top