• HABARI MPYA

    Friday, April 18, 2014

    SIMBA NA YANGA KESHO KIINGILIO 7,000 HADI 30,000

    Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inafikia tamati kesho (Aprili 19 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani, huku mabingwa wapya Azam wakikabidhiwa kombe lao Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu.
    Mechi zote saba zitachezwa kuanzia saa 10:00 jioni ambapo Yanga na Simba zitakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mechi ambayo viingilio vyake ni sh. 7,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
    Mrundi Amisi Tambwe wa Simba SC anatarajiwa kuvutia mashabiki wengi kesho Uwanja wa Taifa

    Tayari tiketi zimeanza kuuzwa leo (Aprili 18 mwaka huu) katika vituo saba vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kariakoo (Kidongo Chekundu), Buguruni Shell, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Ubungo OilCom, Dar Live Mbagala na Uwanja wa Taifa.
    Mechi nyingine zitakuwa kati ya Tanzania Prisons na Ashanti United (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Rhino Rangers na Ruvu Shooting (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Mgambo Shooting (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Oljoro JKT na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Coastal Union na Kagera Sugar (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga).
    Wakati huo huo; Michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (Beach Soccer) inazinduliwa rasmi keshokutwa (Aprili 20 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni, Dar es Salaam na kushirikisha timu 13.
    Uzinduzi huo utaanza saa 5 asubuhi na mechi zitachezwa hadi saa 11 jioni. Michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini inashirikisha timu 13 kutoka vyuo mbalimbali vya jijini Dar es Salaam.
    Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Ardhi (AU), Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
    Michuano hiyo itakuwa inachezwa Jumamosi na Jumapili kwenye fukwe za Escape One na Gorilla Beach iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA KESHO KIINGILIO 7,000 HADI 30,000 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top