• HABARI MPYA

    Wednesday, February 26, 2014

    ZAMBIA WATUA KUIKABILI TWIGA STARS, SYMBION KUSAIDIA PROGRAMU ZA VIJANA TFF

    Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
    TIMU ya taifa ya Zambia (Shepolopolo) inatua nchini kesho mchana (Februari 27 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Tanzania (Twiga Stars) itakayochezwa keshokutwa (Februari 28 mwaka huu).
    Shepolopolo yenye msafara wa watu 29 itawasili kwa ndege ya Fastjet ikitokea Lusaka na itafikia kwenye hoteli ya Accomondia kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi hivi karibuni alikutana na Rais wa CAF, Issa Hayatou mjini Cairo, Misri

    Waamuzi wa mechi hiyo kutoka Burundi wakiongozwa na Ines Niyosaba wamewasili nchini leo asubuhi wakati Kamishna Fran Hilton-Smith kutoka Afrika Kusini atawasili kesho (Februari 27 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya South African Airways.
    Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Symbion Power Tanzania Limited zimesaini makubaliano ambapo kampuni hiyo itasaidia kwenye maeneo matatu ya mpira wa miguu wa vijana.
    Makubaliano hayo yametiwa saini leo (Februari 26 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam. Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesaini kwa niaba ya shirikisho wakati upande wa Symbion aliyesaini ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Peter Gathercoles. Maeneo ambayo Symbion itasaidia ni ujenzi wa vituo viwili vya kuendeleza vipaji vitakavyojengwa Kidongo Chekundu na Kinondoni mkoani Dar es Salaam, mashindano ya Taifa ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 12 (U12) yatakayofanyika mwaka huu na kuisaidia timu ya U17 ya Tanzania (Serengeti Boys).
    Serengeti Boys itacheza na Afrika Kusini, Julai mwaka huu katika mechi za mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa wachezaji wa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Niger.
    Hivyo Symbion imetoa dola 60,000 (zaidi ya sh. milioni 96) kwa ajili ya mashindano ya U12, na dola 50,000 (zaidi ya sh. milioni 80) kwa ajili ya maandalizi ya Serengeti Boys kwa mechi dhidi ya Afrika Kusini.
    Rais Malinzi ameishukuru Symbion kwa kukubali kushirikiana na TFF katika mpira wa miguu wa vijana, lakini vilevile amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwani ndiye chachu ya kampuni hiyo kuamua kujishirikisha na mpira wa miguu wa vijana.
    Katika hatua nyingine, Rais wa TFF, Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari juu ya benchi la ufundi la timu ya Taifa ya wakubwa (Taifa Stars), kesho (Februari 27 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya 3 katika Jengo la PPF Tower, mtaa wa Garden na Ohio.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZAMBIA WATUA KUIKABILI TWIGA STARS, SYMBION KUSAIDIA PROGRAMU ZA VIJANA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top