• HABARI MPYA

  Jumatano, Februari 19, 2014

  HAYA NI MATATIZO YA KUJITAKIA, SIMBA NA YANGA

  KILIO cha muda mrefu cha wadau wa soka nchini kuhusu klabu kongwe, Simba na Yanga ni kwa nini vigogo hao baada ya takriban miaka 80 wanashindwa kujimudu kiuchumi, licha ya kujaaliwa rasilimali watu kubwa.
  Wiki iliyopita nilikuwa mkoani Mbeya kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba SC na wenyeji Mbeya City.
  Nikiwa huko, nilishuhudia jezi za Mbeya City zikiuzwa kama njugu mitaani na zinanunuliwa mno na zinavaliwa sana, hususan siku ambazo timu hiyo inacheza.
  Hii ni timu mpya kabisa siyo tu katika Ligi Kuu, bali kwenye ramani ya soka nchini kwa ujumla.

  Imepata mwamko wa kuridhisha, inashabikiwa na kupendwa karibu na kila mkazi wa Mbeya.
  Niliuliza kuhusu zile jezi, nani anatengeneza na fedha zinazopatikana zinakwenda wapi- nikaambiwa zinatayarishwa na wamiliki wa timu, Halmashauri ya Jiji la Mbeya (MCC) na fedha wanazokusanya ndizo zinazosaidia kwa kiasi kikubwa katika uendeshaji wa timu yao.
  MCC wana mikakati mipana zaidi ya kutumia rasilimali watu waliyojaaliwa pale mkoani Mbeya kujinufaisha zaidi kwa kipato ambacho kitaendelea kuisaidia timu hiyo.
  Kwa ujumla, mikakati ya MCC ni kuifanya Mbeya City iwe moja ya timu gumzo barani Afrika miaka michache ijayo na sina shaka wanaweza kwa sababu wana wataalamu wa masuala ya masoko pale Halmashauri, ambao wameufanya mkoa huo uwe moja kati ya mikoa bora Tanzania.
  Lakini Mbeya City si timu pekee ambayo jezi zake zinavaliwa na mashabiki- kwa kiasi kikubwa sana Simba na Yanga ndizo ambazo jezi zake zinavaliwa zaidi.
  Na si jezi tu, tunashuhudia bidhaa nyingi zenye nembo za Simba na Yanga zinamilikiwa na watu mitaani, tena nchi nzima, ukiachilia mbali jezi, kuna skafu, kofia, kanga za akina mama, fulana na vibendera vidogo vidogo vinavyopambwa kwenye gari.
  Pamoja na ukweli huo, lakini ukienda kwa Katibu Mkuu wa Simba SC au wa Yanga ukamuuliza ni kiasi gani kinachopatikana kutokana na mauzo ya bidhaa hizo, utaambiwa hakuna kitu bali watu wanafanya kinyume cha sheria.
  Wanafanyaje kinyume cha sheria wakati hawa watu wanaouza hizo bidhaa husafiri na timu kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani na wanajulikana ni akina nani wanafanya biashara hiyo?
  Tatizo ambalo naliona, Simba na Yanga zimeshindwa kuitumia vizuri fursa ya kuajiri watendaji wa kufanya shughuli za kila siku za klabu.
  Ama zilikubali kwa kuwa lilikuwa agizo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tena ambalo wao walilipokea kutoka FIFA (Shirikisho la Soka la Kmataifa) au walitaka tu kuwa na wasimamizi wa ofisi.
  Inaonekana kabisa, watu wanaoajiriwa Simba na Yanga bado hawajazisaidia klabu hizo na zaidi wanakuwa kama matarishi tu ofisini.
  Yapata miaka mitano sasa tangu klabu hizo zianze kuajiri Watendaji, lakini kwa kweli hawana cha maana walichofanya- zaidi ya Makatibu kufanya shughuli za kawaida mno za kiofisi.
  Hawana ubunifu wowote, wanaingia ofisini kusubiri kutekeleza majukumu ya kawaida mno mwisho wa siku wapewe mishahara wakakidhi mahitaji yao na familia zao, lakini klabu hazina lolote.
  Na mbaya zaidi viongozi waliopewa dhamana na wanachama hawajaliona hilo, japokuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kiuchumi.
  Angalau Yanga SC pale, Mwenyekiti wake Yussuf Manji na baadhi ya Wajumbe kama Mussa Katabaro, Seif Ahmed ‘Magari’ na Abdallah Bin Kleb ni wafanyabiashara wanaojitolea fedha kuongezea zile zinazotolewa na wadhamini, Bia ya Kilimanjaro. 
  Simba SC mtu ambaye anajitolea fedha zake ni mmoja tu, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe na zaidi ya hapo ni udhamini wa Kilimanjaro.
  Matokeo yake hali ni mbaya katika klabu hiyo, wachezaji wanakata miezi miwili bila kulipwa mishahara, wengine wanadai fedha zao za usajili na kadhalika na bado hao hao unawategemea wakakupiganie kwenye vita ya mataji.
  Inasikitisha Simba na Yanga zinanunua hadi maji ya kunywa wakati wa mechi na mazoezi, wakati nchi hii ina kampuni kibao zinazouza maji ambazo naamini zingependa kutangaza biashara zao kupitia klabu zenye mashabiki wengi kama hizo Simba na Yanga.
  Lakini nani aliwaandikia mapendekezo, kuwashawishi namna watakavyonufaika kwa kuwekeza kwenye timu zao?
  Naikumbuka jezi ya Simba SC ya mwaka 2003, ilikuwa ina matangazo ya kampuni za MeTL, Benki ya NBC na Simba Cement, ukiondoa tangazo la wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom. 
  Mohamed Enterprises Limited inayomilikiwa na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohamed Dewji ilikuwa kampuni ya kwanza kuidhamini Simba SC mwaka 1998.
  Kwa jitihada zake mwenyewe, wakati Simba SC inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, Mo Dewji akawavuta NBC na Simba Cement kujitangaza kupitia jezi za Simba SC. 
  Wakati ule, Yanga walishindwa kuifuata kampuni nyingine ya Cement na benki nyingine kuomba nao wajitangaze kwenye jezi zao.
  Baada ya Mo Dewji kujitoa Simba SC, NBC na Simba Cement nao wakaondoka, lakini hadi leo Simba SC imeshindwa kupata wadhamini zaidi.
  Historia ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), watengenezaji wa bia ya Kilimanjaro kuzichukua Simba na Yanga ni kwamba ni wao wenyewe waliamua, wakatafuta namna ya kuzifikia, lakini bila ya hivyo sijui leo hali ingekuwaje kwenye klabu hizo.
  Katika kipindi cha takriban miaka mitano ya kuwa chini ya udhamini wa TBL, Simba na Yanga zimekwishavuna mabasi matatu kila moja, Hiece, Coaster na Yutong.
  TBL inalipa mishahara ya wachezaji na gharama za uendeshaji ofisi pamoja na kutoa ruzuku nyingine nyingine kila mwaka.
  Kwa ujumla TBL inazibeba haswa Simba na Yanga na siku itakapoamua sasa basi, hakika itakuwa kilio.
  Lakini Simba na Yanga SC zinaweza kupata makampuni zaidi ya kujitangaza kwenye jezi zao, iwapo watendaji wa kuajiriwa wa klabu hizo watalifanyia kazi hilo.
  Ila kama wameajiriwa watu wasio na sifa na uwezo huo, tu kukidhi agizo la TFF kutoka FIFA, maana yake wataendelea kufanya kazi za kitarishi tu ofisini.  Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HAYA NI MATATIZO YA KUJITAKIA, SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top