• HABARI MPYA

    Wednesday, February 26, 2014

    KUTOKA KINYAIYA GESTI HADI BAHARI BEACH, YANGA SC IMEPIGA HATUA KUBWA

    MWAKA 2009, Yanga SC ilitolewa mapema tu katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa nyumbani na ugenini na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora.
    Ilifungwa 3-0 Cairo katika mchezo wa kwanza kabla ya kuja kufungwa 1-0 katika mchezo wa marudiano Dar es Salaam. 
    Baada ya kutolewa na Ahly Machi mwaka huo, mwezi uliofuata Yanga SC ilikutana na wapinzani wa jadi, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu Aprili 19, mwaka 2009.
    Mechi hiyo iliisha kwa sare ya 2-2, mabao ya Simba SC yakifungwa na Ramadhani Chombo ‘Redondo’  na Haruna Moshi ‘Boban’, wakati ya Yanga yalifungwa na 
    Ben Mwalala na Jerry Tegete.

    Baada ya mchezo huo, aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga SC wakati huo, Mkenya Boniphace Ngairah Ambani akasema; “Kama maandalizi kwa ajili ya mchezo huu (dhidi ya Simba) tungeyapata pia wakati tunataka kucheza na Al Ahly, sidhani kama tungetolewa,”.
    Yanga SC ilikwenda Cairo kumenyana na Ahly bila maandalizi ya maana na kadhalika iliingia Uwanja wa Taifa kurudiana na Waarabu hao ikiwa haina maandalizi ya maana.
    Lakini kuelekea mchezo na Simba SC, Yanga iliwekwa kambini hoteli ya New Africa katikati ya Jiji na ilikuwa inafanya mazoezi kwenye Uwanja mzuri wa kukodi katika shule ya IST, Masaki. 
    Alichokisema Ambani wakati huo ni kitu ambacho muda mrefu tumekuwa tukikipigia kelele, aina ya maandalizi ya timu zetu kabla ya michezo hii mikubwa ya Afrika.
    Mwaka 1999 Yanga ilicheza Kombe la Shirikisho na mechi ya kwanza ilichezwa Nigeria dhidi ya wenyeji Kwara United ambako walipokewa vizuri, wakawekwa hoteli nzuri, wakapata lishe nzuri na kufanya mazoezi katika Uwanja mzuri, wakaenda kufungwa bao 1-0 katika mechi ambayo hata wao wangeweza kushinda.
    Sasa katika mchezo wa marudiano, Kwara walipofika Dar es Salaam wakaikataa hoteli ya Yanga wakakodi hoteli yao wenyewe ya nyota tano, White Sands na wakapata Uwanja mzuri wa kufanyia mazoezi.
    Yanga waliweka kambi katika gesti moja maarufu sana Ubungo enzi hizo, ilikuwa inaitwa Kinyaiya na walikuwa wanafanya mazoezi kwenye Uwanja wa UDSM (Chuo Kikuu Dar es Salaam).
    Haikuwa ajabu Yanga wakafungwa 3-0 na Kwara Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano.
    Kwa muda mrefu, kufanya vibaya kwa Yanga kwenye michuano ya Afrika kunatokana na aina ya maandalizi yake- lakini kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya Al Ahly, tumejionea tofauti kubwa ya maandalizi.
    Yanga SC wameonyesha dhamira ya kutaka kushindana na Ahly kuwania nafasi ya kusonga mbele kwa kuwekeza kwenye maandalizi mazuri na makini.
    Wiki iliyopita wakati Ahly inaifunga CS Sfaxien mabao 3-2 katika mechi ya Super Cup, Charles Boniface Mkwasa kocha Msaidizi wa Yanga alikuwepo Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
    Yanga iliweka kambi Uturuki mapema mwaka huu na tangu imerudi imekuwa kambini Bagamoyo hadi jana ilipohamia Bahari Beach Hotel.
    Imehamia Bahari Beach kwa kufuata ushauri wa kocha wao, Mholanzi Hans van der Pluijm kwamba Uwanja ambao walikuwa wanafanyia mazoezi  Bagamoyo haufai kwa maandalizi ya mechi na Ahly.
    Sasa wakiwa Bahari Beach, Yanga SC watakuwa wanafanya mazoezi kwenye Uwanja mzuri eneo la Boko, unaofaa kwa maandalizi dhidi ya Ahly.
    Kwa maandalizi ya aina hii, kwa nini tusiupongeze uongozi wa Yanga SC, kwani umecheza vizuri katika idara yake na sasa imebaki benchi la ufundi na wachezaji nao kutuonyesha watafanya nini katika idara yao. Kila la heri Yanga SC kuelekea mchezo wa Jumamosi.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUTOKA KINYAIYA GESTI HADI BAHARI BEACH, YANGA SC IMEPIGA HATUA KUBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top