• HABARI MPYA

  Monday, February 24, 2014

  MATATIZO MAKUBWA SIMBA SC NI HAYA HAPA HATA TIMU INAVURUNDA LIGI KUU

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  UKALI wa kocha Zdravko Logarusic na kutosikiliza ushauri wa wenzake katika benchi la Ufundi na matatizo ya uongozi vimetajwa kama vitu vikuu vinavyosababisha matokeo mabaya katika timu ya Simba SC kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hivi sasa.
  Simba SC ilicheza mechi ya nne mfululizo bila ushindi, ikiambulia pointi mbili kati ya 12 na sasa siyo tu imepoteza matumaini ya ubingwa, bali hata nafasi ya pili ambayo hutoa mwakilishi wa nchi kwenye Kombe la Shirikisho la Afrika.
  Tatizo? Kocha Zdravko Logarusic ukali wake unatajwa kuwa moja ya sababu za timu kufanya vibaya katika Ligi Kuu  

  Maana yake, mwakani Simba SC wanaweza kuwa nje ya michuano ya Afrika kwa mara ya pili mfululizo, baada ya mwaka huu pia kuzidiwa kete na Yanga SC na Azam FC.
  Katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY, wachezaji wa Simba SC wamesema kwamba morali yao imeshuka kwa kiasi kikubwa kutokana na hali halisi ndani ya timu na wanacheza tu kwa sababu soka ni ajira yao.
  Wakizungumza kwa mashari ya kutotajwa majina, wachezaji hao walisema mambo mawili makubwa yanawakwaza, kwanza uongozi chini ya Mwenyekiti Alhaj Ismail Aden Rage ambao umefeli kwenye suala la maslahi yao.
  La pili wamesema ni kocha Mcroatia, Zdravko ambaye katika wakati huu mgumu badala ya kuwafariji wachezaji, yeye ndiye amekuwa akiwavuruga zaidi.
  Wamesema walitarajia kwa kuwa Loga anafahamu hali halisi ya timu, angekuwa karibu na wachezaji kuwafariji na kuwahamasisha wasahau matatizo yao na kucheza mpira, lakini badala yake yeye ndiye amekuwa akiwavuruga zaidi.
  Wamesema kitendo cha Logarusic kuwafokea na kuwatukana wakati morali yao imeshuka kinazidi kuwaondoa mchezoni na matokeo ndiyo haya yanayoendelea hivi sasa.
  Wamesema Logarusic amemfanya kila mchezaji ndani ya Simba SC hivi sasa apoteze hali ya kujiamini, kutokana na namna ambavyo anawafayia baadhi ya wachezaji.
  “Mtu kama Baba Ubaya (Issa Rashid), tangu msimu umeanza amekuwa mchezaji muhimu ndani ya timu, ila kwa sasa mbele ya Loga hapangwi tena. Hata huyo Mombeki (Betram) anayemuona leo hafai, lakini alikuwa anaifungia timu mabao muhimu tena katika mechi ngumu, kama na Yanga,”alisema mmoja wa wachezaji hao.
  Wanasema Logarusic anapaswa kushikamana na wachezaji katika wakati huu mgumu, kuwahamasisha wacheze kwa bidii, badala ya kuwakaripia  kama anavyofanya hivi sasa.    
  Upande wa pili wa shilingi, Logarusic analalamikiwa pia kutosikiliza ushauri wa wenzake katika benchi la Ufundi na kwamba amekuwa ana maamuzi binfasi, ambayo yamechangia kuigharimu timu mfano katika kufanya mabadiliko ya wachezaji.
  “Jana sisi pale, anataka kumtoa Ndemla (Said), wenzake wanamuambia muache, hakusikia. Matokeo yake kamtoa timu imefanya vibaya, huwezi kumtoa mchezaji kwa kukosea mara moja au mara mbili. Saa ngapi umempa nafasi ya kurekebisha makosa yake?”alihoii mchezaji mwingine.
  Wachezaji hao wamesema kwamba pia timu inakabiliwa na hali ngumu ya kifedha na sasa wao ndiyo wanageuzwa mtaji, hali ambayo inawasikitsha sana.
  “Tunakwenda mikoani, tukifika hoteli tunawekwa kwa mkopo, hadi mechi ichezwe ndipo fedha zipatikane, yalipwe madeni ndiyo zinazobaki tugawiwe, wakati mwingine tunapata mgawo hadi aibu kusema,”alisma mchezaji meingine.
  Wamesema hali hiyo ngumu kifedha imechangiwa na wadau wakiwemo watu wa kundi la Friend of Simba kujitenga kutokana na kile wanachoskia kutoelewana na uongozi chini ya Rage.
  “Wale watu (Friends of Simba) wanapokuwa karibu na timu wanasaidia sana wachezaji. Lakini kwa sasa hawapo kila mchezaji analia njaa ndani ya timu. Kwa kweli hii inazidi kutuweka katika wakati mgumu,”alisema mchezaji mwingine.
  Matokeo ya jana yanaifanya Simba SC ibakiwe na pointi zake 32 baada ya kucheza 19 ikibaki nafasi ya nne, nyuma ya Mbeya City pointi 35 mechi 19, Azam FC pointi 37 mechi 17 na Yanga SC pointi 38 mechi 17 pia kileleni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MATATIZO MAKUBWA SIMBA SC NI HAYA HAPA HATA TIMU INAVURUNDA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top