• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 20, 2014

  MATAJIRI YANGA WACHANGA MILIONI 200 PIGA, UA WAARABU WAFE DAR

  Na Somoe Ng'itu, Dar es Salaam
  KATIKA kuhakikisha Yanga inasonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa kuwatoa mabingwa wa zamani wa michuano hiyo barani Afrika, timu ya Al Ahly ya Misri jumla ya Sh. milioni 200 zimechangwa imefahamika.
  Habari kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam zinasema kwamba kiasi hicho cha fedha kimechangwa na viongozi wa tano wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara inayoendelea hapa nchini.
  Mwarabu lazima afe; Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed 'Magari' katikati akiwa na Makamu wake, Mussa Katabaro kushoto

  Chanzo hicho kiliwataja baadhi ya viongozi hao wa Yanga waliofanikisha fedha hizo zinapatikana ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Seif Ahmed 'Magari', Mwenyejiti wa Kamati ya Usajili, Abdallah Binkleb na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga na Kamati ya Mashindano, Mussa Katabaro.
  Mjumbe mwingine ambaye yuko katika kamati hiyo maalumu ya kuisambaratisha Al Ahly ni Isack Chanje na waliamua kuandaa fedha kwa sababu wanajua zitawasaidia kufanya kila jambo linalowezekana ili kufanikisha malengo yao.
  Chanzo hicho kiliongeza kwamba klabu ya Yanga imejipanga kuhakikisha mwaka huu inaweka rekodi ya kumuwaondoa Waarabu katika mashindano hayo na kusonga mbele.
  Aliongeza kuwa wanafahamu mechi hizo mbili ( nyumbani na ugenini) zitakuwa ngumu na wapinzani wao wamejipanga kusaka ushindi ili wasonge mbele.
  "Tunajua ni mechi itakayokuwa na ushindani na changamoto mbalimbali, tunataka kuweka historia na tunajua wazi tukishinda, dunia nzima itajua na tutasimama kifua mbele," alisema mmoja wadau hao wa Yanga.
  Alieleza kuwa Yanga imejipanga kuhakikisha inapata matokeo mazuri hapa nyumbani ili mechi yao ya marudiano itakayofanyika Cairo iwe nyepesi.
  "Kila mtu anatakiwa kupata ushindi usio na mashaka nyumbani ili ugenini unaenda kumalizia, tunawajua waarabu wanavyokuwa ugenini na wanavyobadilika nyumbani kwao, kikubwa tunataka kufanya kila kinachowezekana ili tusonge mbele," aliongeza.
  Alisema wakati wanapambana kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, pia wanahakikisha wanashinda mechi za ligi ili waweze kutetea ubingwa wao. 
  Wawakilishi hao wa Tanzania watacheza mechi za hatua ya kwanza baada ya kuwapa kichapo cha aibu timu ya Komorozine ya Comoro cha mabao 12-2.
  Yanga pia baadaye mwaka huu itaiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).
  mwisho.
  (Habari hizi zimeandikwa na Somoe Ng’itu wa gazeti la NIPASHE) 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MATAJIRI YANGA WACHANGA MILIONI 200 PIGA, UA WAARABU WAFE DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top