• HABARI MPYA

    Monday, February 24, 2014

    MECHI YA TWIGA STARS, ZAMBIA BURE

    Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
    MASHABIKI wa mpira wa miguu nchini watashuhudia bure mechi ya timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) dhidi ya Zambia (Shepolopolo).
    Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) itachezwa Ijumaa (Februari 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili alasiri.
    Njooni mtuunge mkono; Wachezaji wa Twiga Stars katika moja ya mechi zao zilizopita

    Twiga Stars ambayo ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Lusaka, Februari 14 mwaka huu kwa mabao 2-1 iko kambini chini ya Kocha Rogasian Kaijage na msaidizi wake Nasra Juma ikijiwinda kuwakabili Wazambia wanaotarajiwa kutua nchini Alhamisi (Februari 26 mwaka huu).
    Waamuzi wa mechi hiyo Ines Niyonsaba, Jacqueline Ndimurukundo, Axelle Shikana na Suavis Iratunga kutoka Burundi kutoka Burundi wanatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa (Februari 26 mwaka huu). Kamishna Fran Hilton Smith kutoka Afrika Kusini yeye atatua nchini Februari 27 mwaka huu kwa ndege ya South Africa Airways.
    Wakati huo huo: Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred Rwiza Kishongole kuwa Kamishna wa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya TP Mazembe na Asres De Douala ya Cameroon.
    Mechi hiyo ya hatua ya 16 itafanyika kati ya Machi 7, 8 au 9 mwaka huu jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuchezeshwa na waamuzi kutoka Uganda.
    Mwamuzi wa kati atakuwa Denis Batte wakati wasaidizi wake ni Mark Ssonko, Samuel Kayondo na Mashood Ssali.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MECHI YA TWIGA STARS, ZAMBIA BURE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top