• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 20, 2014

  FUFA WATAKA KUIVURUGIA YANGA KWA OKWI MECHI NA AL AHLY

  Na Prince Akbar, Dar es Salaam
  YANGA SC itacheza mechi ya marudiano na Al Ahly ya Misri mjini Cairo kati ya Machi 7 na 9 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mchezo wa kwanza Dar es Salaam Machi 1, mwaka huu.
  Na kikosini mwake ina wachezaji wawili tegemeo wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes ambao ni washambuliaji Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza.
  Uganda imetangaza itacheza mechi ya kirafiki na Zambia, Chipolopolo iliyo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) Machi 5, mwaka huu Uwanja wa Ndola, Zambia.
  Emmanuel Okwi kulia akiwa na jezi ya Uganda, The Cranes. Je Micho atamuita kwa ajili ya mechi na Zambia?

  Hiyo imethibitishwa na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Edgar Watson baada ya kufikia makubaliano na wenzao, Chama cha Soka Zambia (FAZ).
  Kocha Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ bado hajataja kikosi ambacho kitacheza na Zambia, lakini wakati wote amekuwa hawaachi Okwi na Kiiza na bila shaka ataendelea na utamaduni huo.
  Kama Micho atawaita Kiiza na Okwi dhahiri ataathiri maandalizi ya Yanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Ahly, kwani watalazimika kwenda Uganda mara tu baada ya mechi ya kwanza na mabingwa hao wa Afrika na kwa kuwa watacheza mechi Ndola Machi 5, maana yake wanaweza kuondoka huko Machi 6 wakati tayari mabingwa wa Bara wakiwa Cairo.
  Wakiitwa Cranes, Okwi na Kiiza hawatapata fursa ya kushiriki mazoezi ya Yanga kujiandaa na mchezo wa marudiano na Ahly, pia watachoka na safari na mechi ngumu mfululizo.
  Tanzania pia itakuwa na mechi katika tarehe ya FIFA na kama kocha Mdenmark Kim Poulsen ataita wachezaji wa Yanga kwa utaratibu wake wa kambi ya wiki nzima kabla ya mechi, ina maana kambi ya maandalizi ya klabu hiyo itapata pigo kubwa, kwa kuwa kwa sasa wachezaji wengi wa Stars hutokea timu hiyo ya Jangwani. 
  Kitu kizuri kwa Yanga SC na kusikia vikosi vya Uganda, Tanzania, Burundi na Rwanda kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa mwezi ujao vinatajwa bila ya wachezaji wao kujumuishwa. Mbali na Waganda Okwi na Kiiza, Yanga ina Wanyarwanda Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima kikosini.  

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: FUFA WATAKA KUIVURUGIA YANGA KWA OKWI MECHI NA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top