• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 20, 2014

  POLISI HAIKAMATIKI LIGI KUU ZANZIBAR, YAILAMBA 2-0 MIEMBENI

  Na Ameir Khalid, Zanzibar
  MAAFANDE wa timu ya Polisi, wamedhihirisha nia ya kulirejesha taji la ubingwa wa soka Zanzibar ambalo limewaponyoka miaka kadhaa iliyopita kwa kuifunga timu yenye majigambo mengi Miembeni SC mabao 2-0.
  Pambano hilo lililochezwa jana Jumatano uwanja wa Amaan, na ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kisiwani hapa, lilikuwa na ushindani kwa muda wote.
  Wanaume hao walioingia dimbani wote wakiwa na pointi 28, walikamiana sana hali iliyosababisha mchezo huo kukosa ladha iliyotarajiwa.
  Wachezaji wa Polisi wakishangilia moja ya mabao ya jana

  Licha ya kushambuliana kwa zamu, timu hizo zilikwenda mapumziko kukiwa hakuna mlango uliokubali kufunguka.
  Baada ya kila timu kufanya mabadiliko ya wachezaji kadhaa, zilikianza kipindi cha pili kwa kuendelea kukamiana ambapo majaribio ya kufunga yalikuwa machache milangoni.
  Hata hivyo, Polisi walipata dawa ya ushindi dakika 15 za mwisho na kufanikiwa kuzichana nyavu za wapinzani wao mara mbili.
  Mshambuliaji hatari wa maafande hao Khalid Kheri alifunga bao la kwanza katika dakika ya 76 baada ya kupiga shuti lilowababatiza mabeki wa Miembeni na mpira kwenda nyavuni moja kwa moja.
  Jitihada za Miembeni kujitutumua ili kurejesha bao hilo zilirejeshwa nyuma kufuatia Polisi kuongeza la pili katika dakika ya 90 mara hii likiwekwa kimiani na Haule Innocent, mtoto wa mchezaji wa zamani wa Miembeni, Simba SC, Zanzibar Heroes na Taifa Stars, Innocent Haule.
  Kwa matokeo hayo Polisi wamejidhatiti kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayodhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt, ikifikisha pointi 31, ikifuatiwa na Miembeni yenye pointi 28 na Mtende Rangers iliyo katika nafasi ya tatu kwa pointi zao 27.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: POLISI HAIKAMATIKI LIGI KUU ZANZIBAR, YAILAMBA 2-0 MIEMBENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top