• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 17, 2014

  KAPOMBE SASA AKUBALI KUREJEA UFARANSA, LAKINI SI AS CANNES TENA, AZAM WASEMA...

  Na Somoe Ng'itu, Dar es Salaam
  WAKATI beki wa zamani wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Shomary Kapombe, anadaiwa kukataa kurejea katika timu yake ya AS Cannes ya Ufaransa, habari zaidi zimeelezwa kwamba wakala wake amewaambia Azam kuwa mchezaji huyo thamani yake ni Dola za Marekani 150,000.
  Habari kutoka kwa watu wa karibu wa mchezaji huyo zinasema kwamba nyota huyo amemueleza wakala wake, Denis Kadito, atakuwa tayari kurejea Ufaransa kucheza katika timu nyingine na si hiyo ya awali ambayo ilimpokea akitokea Simba.
  Anarudi Ufaransa; Shomary Kapombe amekubali kurejea Ufaransa, lakini akachezee timu nyingine si AS Cannes

  Chanzo cha gazeti hili kinaeleza kwamba tayari mazungumzo kati ya Kapombe na Azam yamefikia katika hatua za mwisho na ni moja ya sababu iliyomfanya beki huyo wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) kukataa kurejea Ufaransa.
  "Tayari Kapombe ameshamueleza wakala wake (Denis Kadito) kwamba hana nia ya kurejea AS Cannes, na hata kama akirejea Ufaransa iwe ni kwenye klabu nyingine," kilisema chanzo chetu.
  Hata hivyo, Kapombe, alikataa kuzungumza chochote kuhusiana na taarifa za yeye kukataa kurejea Ufaransa na kuelezea maamuzi yake ya kuendelea kukaa hapa nchini.
  "Kwa sasa siwezi kusema chochote, mtafute wakala wangu ndio atakayekueleza, nisamehe sana," alisisitiza beki huyo ambaye Simba ilimsajili akitokea Polisi Morogoro iliyowahi kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Kwa sasa beki huyo anafanya mazoezi binafsi katika viwanja tofauti hapa jijini Dar es Salaam ili kulinda kiwango chake kisishuke.
  Afisa Habari wa Azam, Jaffer Idd, alisema kwamba ni mapema mno kuzungumzia usajili wa wachezaji katika muda huu ambao bado timu yao iko katika harakati za kuwania ubingwa wa Bara.
  Idd alisema kuwa muda muafaka utakapofika na dirisha la usajili litakapofunguliwa rasmi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndio wataanza zoezi hilo.
  Azam iliyokuwa inashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho imeondolewa na Ferroviario de Beira baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 juzi huko ugenini.
  Kadito hakupatikana jana katika simu yake ya mkononi kueleza mikakati ya kumrejesha Kapombe Ufaransa kama ilivyotarajiwa baada ya kumaliza tofauti za mchezaji huyo na AS Cannes.
  (Habari hii imeandikwa na Mwandishi Somoe Ng’itu wa gazeti la NIPASHE)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAPOMBE SASA AKUBALI KUREJEA UFARANSA, LAKINI SI AS CANNES TENA, AZAM WASEMA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top