• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 25, 2014

  KAMBI YANGA SC YAHAMIA DAR ES SALAAM, AHLY WAKO NJIANI KUJA DAR NA KIKOSI HATARI TUPU

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  YANGA SC imefuta mpango wa kurejea Bagamoyo kuweka kambi kwa ajili ya mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly au National ya Misri na sasa itabaki Dar es Salaam.
  Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm amesema Uwanja wanaofanyia mazoezi Bagamoyo haufai kwa maandalizi ya mechi hiyo ya kwanza, Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika anahitaji Uwanja mzuri ambao Bagamoyo haupo kabisa.
  Kikosi cha Yanga SC kilichoifunga 7-0 Komorozine Dar es Salaam. Al Ahly itapigwa ngapi? 

  Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed ‘Magari’ tangu jana yuko ‘bize’ na kutafuta Uwanja mzuri na kambi nzuri na kuna uwezekano, klabu hiyo ikafanyia mazoezi Uwanja wa Taifa kuanzia leo.
  Wachezaji wa Yanga jana walifanya mazoezi mepesi makao makuu ya klabu Jangwani na kisha kila mmoja kurejea nyumbani kwake, lakini leo wameambiwa waje kikamilifu kwa ajili ya kuingia kambini.
  Yanga SC itamenyana na Ahly Jumamosi ikiwa katika kiwango kizuri kimchezo, imeweza kushinda mabao 19 ndani ya mechi tatu, 14 katika mechi mbili mfululizo za nyumbani 7-0 dhidi ya Komorozine ya Comoro hatua ya Awali ya Ligi ya Mabingwa na 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika Ligi Kuu Jumamosi.
  Yanga SC ambayo iliifunga 5-2 Komorozine kwenye mchezo wa marudiano Moroni, katika mechi na Ruvu ilionyesha soka ya kiwango cha juu ambayo imeibua matumaini kwamba inaweza kufurukuta mbele ya Ahly.     
  Mara ya mwisho Ahly iliifunga CS Sfaxien katika mchezo wa Super Cup ya Afrika, lakini haina rekodi ya kuvutia sana kwenye ligi ya Misri msimu huu.
  Ahly inatarajiwa kutua Dar es Salaam kuanzia leo na haitahitaji msaada wa Yanga kwa sababu mapema mwezi huu ilituma wawakilishi wake kushughulikia masuala ya kambi na Uwanja wa mazoezi.
  Waarabu hao wanaweza kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana, uliopo kando ya bahari ya Hindi na wapi wataweka kambi, haijajulikana ila inaweza kuwa kwenye moja ya hoteli za nyota tano Dar es Salaam.
  Kikosi cha Ahly kinachotarajiwa kuja Dar es Salaam ni makipa; Sherif Ekramy, Ahmed Adel Abdel-Monem na Mahmoud Abou El-Sooud, wakati mabeki ni; Wael Gomaa, Sherif Abdel-Fadil, Ahmed Fathi, Mohamed Naguib, Saad El-Din Samir, Sayed Moawad na Ahmed Shedid Qenawy.
  Viungo ni; Hossam Ashour, Shehab El-Den Ahmed, Ahmed Nabil Manga, Ahmed Shokry, Mahmoud ‘Trezeguet’, Rami Rabia, Walid Soliman, Abdullah El-Said na Mohamed Abou-Treika na washambuliaji El-Sayed Hamdy, Dominique  Da Silva, Emad Meteb na Amr Gamal ambaye ndiye tegemeo la mabao la timu hiyo kwa sasa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAMBI YANGA SC YAHAMIA DAR ES SALAAM, AHLY WAKO NJIANI KUJA DAR NA KIKOSI HATARI TUPU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top