• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 24, 2014

  OKWI NA KIIZA WOTE WARUDISHWA UGANDA KUITUMIKIA TIMU YA TAIFA, NI PIGO MAANDALIZI YANGA DHIDI YA AL AHLY

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  KOCHA Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ amewaita wote washambuliaji wa Uganda waliopo kwenye kikosi cha Yanga SC ya Dar es Salaam, Emmanuel Arnold Okwi Hamisi Friday Kiiza ‘Diego’ kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Zambia, Chipolopolo ulio katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) utakaofanyika Machi 5, mwaka huu Uwanja wa Ndola, Zambia.
  Katika taarifa aliyoituma BIN ZUBEIRY leo, Micho amewachunia beki wa Simba SC, Joseph Owino na washambuliaji Brian Umony wa Azam FC na Yayo Lutimba wa Coastal Union, Waganda wengine wanaocheza Tanzania.  
  Emmaneul Okwi ameitwa The Cranes

  Kikosi kamili kwa ajili ya mechi hiyo alichoteua Micho ni makipa; Onyango Dennis wa Bidvest Wits ya Afrika Kusini, Odonkara Robert wa Saint George ya Ethiopia na Watenga Ismail wa Vipers.
  Mbakei ni Iguma Denis wa Victoria University, Wadada Nicholas wa Vipers, Walusimbi Godfrey wa Gor Mahia ya Kenya, Kakuba Alex wa Covilha ya Ureno, Kalungi Henry wa Richmond Kickers ya Marekani, Isinde Isaac wa Saint George, Mwesigwa Andrew wa Ordabasy ya Kazakhstan, Kassaga Richard wa Kira Young na Ochaya Joseph wa Asante Kotoko ya Ghana.
  Viungo ni Mawejje Tony wa Haugesund ya Norway, Aucho Khalid wa Tusker, Kizito Geoffrey wa Gor Mahia za Kenya na Ntege Ivan wa KCC, wakati viungo wa pembeni na washambuliaji ni Oloya Moses, Kizito Luwagga William wa Covilha ya Ureno, Matovu Sula wa BK Hacken ya Sweden, Majwega Brian wa KCC, Massa Geoffrey wa University of Pretoria ya Afrika Kusini, Okwi, Kiiza, Sserunkuma Dan wa Gor Mahia na Odour Tony wa KCC.
  Ikumbukwe Yanga SC itacheza mechi ya marudiano na Al Ahly ya Misri mjini Cairo kati ya Machi 7 na 9 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mchezo wa kwanza Dar es Salaam Machi 1, mwaka huu.
  Hamisi Kiiza ameitwa pia na kocha Milurin Stredojevic 'Micho'

  Kwa Micho kuwaita Kiiza na Okwi dhahiri itaathiri maandalizi ya Yanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Ahly, kwani watalazimika kwenda Uganda mara tu baada ya mechi ya kwanza na mabingwa hao wa Afrika na kwa kuwa watacheza mechi Ndola Machi 5, maana yake wanaweza kuondoka huko Machi 6 wakati tayari mabingwa wa Bara wakiwa Cairo.
  Okwi na Kiiza hawatapata fursa ya kushiriki mazoezi ya Yanga kujiandaa na mchezo wa marudiano na Ahly, pia watachoka na safari na mechi ngumu mfululizo.
  Tanzania pia itakuwa na mechi katika tarehe ya FIFA na kama kocha Mdenmark Kim Poulsen ataita wachezaji wa Yanga kwa utaratibu wake wa kambi ya wiki nzima kabla ya mechi, ina maana kambi ya maandalizi ya klabu hiyo itapata pigo kubwa, kwa kuwa kwa sasa wachezaji wengi wa Stars hutokea timu hiyo ya Jangwani. 
  Hali itakuwa mbaya zaidi kwa Yanga iwapo na Rwanda itawaita Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima kwa ajili ya mechi za wiki ijayo za kalenda ya FIFA.  

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: OKWI NA KIIZA WOTE WARUDISHWA UGANDA KUITUMIKIA TIMU YA TAIFA, NI PIGO MAANDALIZI YANGA DHIDI YA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top